Ghana, Afrika Kusini kuna mechi za mtoano WAFCON
Muktasari:
- Ivory Coast itaikaribisha Ghana saa 2 usiku katika Uwanja wa Larbi Zaouli na saa 4 usiku Afrika Kusini ikiminyana na Nigeria mechi itakayopigwa Uwanjwa wa Moulay Rachid, katika vita ya kuwania nafasi za kucheza mchujo wa mabara ili Kombe la Dunia la Wanawake 2027 nchini Brazil.
BAADA ya jana kupigwa mechi mbili za nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) leo kuna mechi mbili za hatua ya mtoano zitachezwa kwenye viwanja tofauti ili kutafuta timu mbili zitakazofuzu kucheza Kombe la Dunia.
Ivory Coast itaikaribisha Ghana saa 2 usiku katika Uwanja wa Larbi Zaouli na saa 4 usiku Afrika Kusini ikiminyana na Nigeria mechi itakayopigwa Uwanjwa wa Moulay Rachid, katika vita ya kuwania nafasi za kucheza mchujo wa mabara ili Kombe la Dunia la Wanawake 2027 nchini Brazil.
Ivory Coast na Ghana, hii ni vita ya Afrika Magharibi baada ya timu hizo kushindwa kufuzu nusu fainali ya WAFCON. Ivory Coast imeonyesha kiwango kizuri katika mashindano ya mwaka huu, huku Ghana ikiwa miongoni mwa timu zenye historia na uzoefu mkubwa katika soka la wanawake barani Afrika.
Mchezo mwingine unaobeba uzito wa aina yake ni Afrika Kusini dhidi ya Nigeria, unaoweza kuwa moja ya vita ya mabingwa. Timu hizo mbili zilizotwaa mataji mawili yaliyopita ya WAFCON, lakini zote zimeondolewa katika hatua ya robo fainali mwaka huu.
Nigeria, mabingwa watetezi, walifungwa na Cameroon, wakati Afrika Kusini ilipoteza 1-2 dhidi ya wenyeji Morocco. Sasa moja kati ya timu hizo itapata nafasi ya kuendelea kupigania tiketi ya Kombe la Dunia.
Mshindi wa mechi hizo mbili ataingia kwenye mchujo wa mabara
Katika mchujo huo wawakilishi wa Afrika wataungana na timu kutoka mabara mengine kama Asia, Marekani na mengineyo katika mashindano maalumu yatakayotoa nafasi za mwisho.
Akizungumzia mchezo huo Kocha wa Nigeria, Justine Madugu alisema “Tunajua hii ni moja ya mechi ngumu kwetu lakini hatuna namna zaidi ya kupambana kuwania nafasi hii ya mwisho.”
Kocha wa Ghana, Kim Lars alisema “Tunaamini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo ingawa haitakuwa rahisi kutokana na mshindani tunayekutana naye.”