Galatasaray yaingilia dili la Waarabu kwa Mohamed Salah
Muktasari:
Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Galatasaray kujaribu kumsajili Salah lakini changamoto kubwa ni ofa yao ya mshahara inaonekana kuwa ndogo tofauti na ile ya timu za Saudia ambazo pia zinahitaji saini yake.
VIGOGO wa Uturuki, Galatasaray, wanapanga kuingilia mipango ya timu za Ligi Kuu ya Saudi Arabia kwa kumshawishi mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah kukubali ofa yao ya mshahara wa Pauni 16 milioni kwa mwaka na kujiunga nao katika dirisha lijalo la majira ya baridi au kiangazi.
Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Galatasaray kujaribu kumsajili Salah lakini changamoto kubwa ni ofa yao ya mshahara inaonekana kuwa ndogo tofauti na ile ya timu za Saudia ambazo pia zinahitaji saini yake.
Salah ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2027, amekuwa katika shinikizo kubwa la kuondoka Liverpool kwa sababu kiwango anachokionyesha kwa sasa hakiwaridhishi wengi.
Katika mechi mbili zilizopita za Liverpool staa huyu amejikuta akianzia benchini ikiwa ni uamuzi wa benchi la ufundi baada ya mwendelezo wake wa kuonyesha kiwango kibovu msimu huu.
Mwaka 2023, Al Ittihad ya Saudia ilikuwa tayari kutoa Pauni 150 milioni ili kuvunja mkataba wa Salah kisha kumpa mshahara wa takribani Pauni 60 milioni kwa mwaka, lakini Liverpool ilikataa.
Kwa sasa mambo yanaonekana kuwa tofauti na taarifa za ndani zinadai baadhi ya vigogo wa majogoo hao wanaona ni bora kumuuza Salah Januari au mwisho wa msimu kwa sababu haonekani kuwa na mchango katika timu kwa sasa wakati huohuo akiwa ndio mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi katika timu.
Matajiri wa Saudi wanamwona fundi huyu kama sehemu ya ushawishi mkubwa wa soko la Afrika ya Kaskazini, hivyo akitua kutakuwa na faida kubwa kibiashara.
CHRISTOS MOUZAKITIS
REAL Madrid inataka kuingia kwenye vita dhidi ya timu nyingine barani Ulaya kwa ajili ya kumsajili kiungo chipukizi wa Olympiakos na timu ya taifa ya Ugiriki, Christos Mouzakitis, mwenye umri wa miaka 18, ambaye pia anahitajika na Manchester United.
Madrid inaamini staa huyu ataingia vizuri katika kikosi chake kutokana na umri wake mdogo sawa na ilivyo kwa wachezaji wengi wa kikosi chao.
JAN PAUL VAN HECKE
TOTTENHAM Hotspur inapanga kuwasilisha ofa ya takriban Pauni 40 milioni kwenda Brighton kwa ajili ya kumsajili beki wa timu hiyo, Jan Paul van Hecke mwenye umri wa miaka 25.
Hata hivyo, mabosi wa Brighton wanadaiwa kuhitaji kiasi kikubwa zaidi cha pesa tofauti na kile ambacho Spurs inapanga kukiwasilisha.
Hecke mwenyewe ameonyesha kuwa tayari kujiunga na Spurs lakini hatolazimisha badala yake atasubiri timu hizo zifikie makubaliano.
JEAN-PHILIPPE MATETA
MSHAMBULIAJI wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, 28, ameiambia timu yake kuwa anataka kuondoka Januari.
Taarifa kutoka tovuti ya Teamtalk zinaeleza kwamba Mateta anaamini sasa ni muda sahihi wa kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Mateta ameanza msimu na hdi sasa tayari amefunga mabao tisa.
Mkataba wake Palace unamalizika 2027 na inahitajika zaidi ya Pauni 40 milioni ili kumuuza.
AC Milan ni miongoni mwa timu zinazohitaji saini yake, ikiwa pamoja na Olympique Lyon, Marseille na Eintracht Frankfurt.
SANTIAGO GIMENEZ
LEEDS United ina mpango wa kuingia katika vita ili kumsajili mshambuliaji wa AC Milan na timu ya taifa ya Mexico, Santiago Gimenez, 24, katika dirisha lijalo la Januari.
Gimenez aling’aa sana akiwa na Feyenoord kabla ya kuhamia AC Milan, akipachika mabao 26 katika msimu wa 2023/24. Leeds inataka kumsajili fundi huyu kutokana na upungufu ambao ipo nao katika kikosi chao tangu kuanza kwa msimu huu.
FER LOPEZ
WOLVES ipo tayari kumruhusu kiungo wao raia wa Hispania Kihispania, Fer Lopez, mwenye umri wa miaka 21, kuondoka kwa mkopo Januari baada ya kuomba kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Lopez amecheza mechi chache msimu huu, kiasi cha kuomba kuondoka. Klabu kadhaa za Ligi Daraja la Kwanza England zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kwa mkopo wa nusu msimu.
ALLAN ELIAS
NEWCASTLE United inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Palmeiras Allan Elia, 21, katika dirisha lijalo la majira ya baridi. Allan Elias ana uwezo mkubwa wa kucheza kama kiungo mchezeshaji na Newcastle.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Msimu uliopita alicheza mechi 55 za michuano yote na kutoa asisti nane.
RODRIGO MENDOZA
ARSENAL Imekuwa ikimfuatilia kiungo wa Elche na timu ya taifa ya vijana ya Hispania, Rodrigo Mendoza, mwenye umri wa miaka 20.
Ripoti kutoka Sky Sports, zimefichua kwamba mabosi wa Elche wanahitaji kiasi kisichopungua Pauni 15 milioni ili kumuuza mchezaji huyo.
Mendoza ameonyesha uwezo mkubwa wa kutawala dimba na kupiga pasi ndefu. Arsenal unamwona staa huyu kama hazina ya baadae. Mkataba wa Mendoza unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.