Gakpo sala nyingii Salah abaki Anfield
Muktasari:
- Mo Salah mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na dili jipya bado halijafikia mwafaka jambo linaloibua wasiwasi mkubwa wa mshambuliaji huyo kuondoka.
LIVERPOOL, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Cody Gakpo anapiga sala zote kuomba Mohamed Salah asaini mkataba mpya wa kubaki kwenye kikosi chao huko Anfield.
Mo Salah mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na dili jipya bado halijafikia mwafaka jambo linaloibua wasiwasi mkubwa wa mshambuliaji huyo kuondoka.
Kutokana na hilo, Salah, 32, atakuwa na ruhusa ya kusaini mkataba wa awali na klabu ya ng’ambo wakati dirisha la usajili wa majira ya baridi litakapofunguliwa Januari Mosi.
Licha ya kutotambua hatima ya maisha yake, Mo Salah amekuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu huu, akifunga mara mbili kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu England, ambapo Liverpool iliichapa Tottenham Hotspur mabao 6-3. Mabao hayo yalimfanya afikishe 15 kwenye ligi hiyo msimu huu na hivyo kushika namba nne kwenye orodha ya vinara wa mabao wa muda wote kwenye kikosi cha Liverpool.
Na sasa Mdachi Gakpo alisema: “Hiki tunachokishuhudia ni spesho sana. Idadi ya mabao anayofunga na asisti anazotupata, namna anavyocheza anawafanya washambuliaji na viungo kufurahia kucheza naye. Natumaini ataendelea kuwa na sisi kwa muda mrefu. Tuna bahati sana kuwa naye. Anatusaidia kuwa bora.”
Gakpo naye yupo kwenye kiwango bora kabisa cha soka lake, akifunga mabao tisa msimu huu, yakiwamo saba kwenye mechi 12 za mwisho. Ni kipindi bora kabisa kwenye maisha yake ya huko Anfield tangu alipojiunga na miamba hiyo baada ya fainali za Kombe la Dunia 2022.
“Nafurahia kila dakika ninayokuwa hapa,” alisema Gakpo, 25 na kuongeza. “Nimekuwa na miaka miwili safi kabisa. Mambo mengi yametokea, nyakati nzuri zimetokea, mbaya zimetokea, lakini kubwa ni kwamba tunajifunza. Nina furaha kuwa kwenye hii klabu.”