Prime
Mbinu tano zinazoweza kumwokoa Ibrahim Doumbia
Wakati mwingine matarajio makubwa husababisha timu ihahe kupata matokeo mazuri, au mchezaji ahangaike kudhihirisha uwezo wake baada ya kusajiliwa kwa mbwembwe na sifa nyingi.
Wakati Fiorentina Perez alipoingia Real Madrid na sera yake ya kuwafanya vigogo hao wa Hispania wawe chapa ya dunia na si barani Ulaya pekee, aliahidi kuunda kikosi kilichojaa nyota kutoka sehemu mbalimbali.
Na kweli, pamoja na kuwa na nyota kama Iker Casillah, Roberto Carlos, Raul na Guti, Perez alianza kukusanya nyota hao kwa kumsajili Luis Figo ambaye alimtumia katika kampeni yake ya urais, Ronaldo Nazario, David Beckham, Zinedine Zidane, Michael Owen na Robinho.
Lakini hakuwa na wakati mzuri licha ya kuwa na kikosi kilichojaa nyota. Real ilihangaika kutwaa ubingwa wa Hispania na haikuweza kutwaa kombe la Ligi ya Mabingwa, hadi sera ya Perez ikaanza kupondwa.
Aliporejea katika kiti cha urais kwa mara ya pili, Perez alikuwa amepata dawa ya kufanikisha ndoto yake. Katika awamu yake ya pili inayoendelea hadi sasa, Perez ameshatwaa kombe la Ligi ya Mabingwa mara saba, zikiwemo tatu alizotwaa mfululizo.
Kwa hiyo, si kila wakati matamanio yanakutana na mafanikio hata kama juhudi kubwa zimefanyika.
Ni kipindi ambacho hata wachezaji nyota duniani hupitia.
Wakati Chelsea ikianza kuibuka kuwa moja ya timu kali barani Ulaya, mmiliki wa wakati huo, Roman Abromovic alisukuma usajili wa mshambuliaji hatari wa kimataifa wa Ukraine, Andriy Shevchenko kutoka AC Milan ambako alikuwa akifunga mabao atakavyo.
Mambo yalimgeuka alipotua Chelsea kwa ada ya Pauni milioni 30.8 za Kiingereza, kiwango ambacho kilikuwa rekodi ya usajili ghali nchini Uingereza.
Katika msimu wake wa kwanza alifunga mabao manne tu na akasakamwa na majeraha kwa muda kabla ya kurudi uwanjani na kushindwa kufikia kiwango cha mshambuliaji mwenza, Didier Drogba. Baadaye kocha Jose Mourinho alisema kuwa Shevchenko hakuwa chaguo lake la kwanza.
Pamoja na kwamba soka lake lilitibuliwa na majeraha, Shevchenko hakuweza kurejesha makali yake ya AC Milan yaliyotarajiwa yaiwezeshe Chelsea kutwaa ubingwa wa Ulaya. Akapotea. Matarajio ya klabu na mashabiki yakageuka kuwa huzuni na lawama.
Ndiyo hali anayopitia mshambuliaji chipukizi wa Simba, Ibrahim Doumbia baada ya mashabiki kumshuhudia akishindwa kutikisa nyavu katika mechi nne za mwanzoni mwa msimu, licha ya kuwaonjesha uwezo wake alipofunga mabao mawili katika michuano ya Kombe la Kagame nchini Rwanda.
Kocha Steve Becker anaonekana bado hajamkatia tamaa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Mali na amemuanzisha katika mechi tatu.
Lakini kwa mashabiki Doumbia hatakiwi uwanjani kwa sasa labda aanzie benchi na kuingia baadaye kumuwezesha kutuliza akili na kurudia makali yake yaliyomfanya afunge mabao 21 msimu uliopita nchini Mali, 17 yakiwa ya ligi, huku akitoa pasi tano za mwisho katika mechi 24 alizoichezea FC Korofina katika mashindano tofauti.
Maana yake, katika umri mdogo wa miaka 22, Doumbia ameshatwaa taji la mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Mali na kushinda tuzo ya Chipukizi Bora anayeibukia.
Amejikuta akionekana kama kituko katika mechi alizocheza kutokana na kosakosa zilizosababisha mpira kwenda mwelekeo tofauti na goli, au kutumia vibaya nafasi za wazi anazotengenezewa na viungo.
Mashabiki washaanza kusema waziwazi kuwa hawamtaki au asiwe anaanza, hasa baada ya kushindwa kutumia vyema nafasi alizopata katika mechi dhidi ya Coastal Union, wakati walioingia baada ya kutolewa waliiwezesha timu kushinda bao 1-0 katika mechi ambayo mabeki wa Coastal walihakikisha Doumbia haachiwi nafasi kubwa wala muda wa kufikiria kufanbya jambo sahihi.
Katika umri wa miaka 22 na kimo kizuri, bado Doumbia anahitaji kuaminiwa zaidi na benchi lake la ufundi na mashabiki ili aweze kurejesha makali yake.
Si rahisi kwa mshambuliaji mwenye umri mdogo kama wake kuibeba timu mabegani mwake, akicheza kama mshambuliaji wa kati. Nafasi hiyo inahitaji uzoefu wa kutosha kjweza kustahimili mikikimikiki ya mabeki wa kati na akili ya kuwakwepa.
Ukiangalia historia yake huoni timu nyingi zaidi ya hiyo Korofina aliyochezea msimu uliopita na hivyo bado hajapata uzoefu wa kutosha wa kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati ambayo wanaoishika hulipwa mamilioni ya fedha wanapofanya vizuri.
Kwa umri wake, anaweza kuwa na vita kubwa kichwani kutokana na kushindwa nyavu. Na hilo linaweza kuwa linamzidishia matatizo kisaikolojia na uwanjani na kujikuta akifanya mambo ambayo yanasababisha azidi kuonekana wa ajabu.
Hapo ndipo wanapohitajika watalaamu wa saikolojia na busara za kocha kumjenga kiakili na kumuonmyesha Imani yake kwake kwa kuongea naye na kuendelea kumpa nafasi kwa nyakati tofauti ili ajishushe na kukubali kuwa wanapitia kipindi kigumu kinachohitaji kutuliza akili.