Manchester City yaweka Sh292bil kwa Gakpo
Muktasari:
- Awali, iliripotiwa kuwa Manchester City ilikuwa imeingia kwenye kinyang’anyiro cha kumsajili Gakpo mwenye umri wa miaka 27, huku ikihofia mshambuliaji huyo huenda akahamia Tottenham.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City imeanza tena harakati za kumsajili mshambuliaji wa Liverpool, Cody Gakpo huku klabu hiyo ikiwa tayari imeanza mazungumzo na wapinzani hao wa Ligi Kuu England kuhusu uhamisho unaoweza kugharimu Pauni85 milioni (Sh292 bilioni).
Awali, iliripotiwa kuwa Manchester City ilikuwa imeingia kwenye kinyang’anyiro cha kumsajili Gakpo mwenye umri wa miaka 27, huku ikihofia mshambuliaji huyo huenda akahamia Tottenham.
Kutokana na hali hiyo, City ilianza pia kumfuatilia mshambuliaji wa Everton, Iliman Ndiaye kama chaguo jingine iwapo ingeshindwa kumpata Gakpo.
Hata hivyo, Gakpo anaonekana kutaka kuhamia Etihad, huku viongozi wa City sasa wakifanya mazungumzo rasmi na Liverpool kuhusu uhamisho huo wa kushangaza.
Gakpo alijiunga na Liverpool mwaka 2023 akitokea PSV Eindhoven kwa Pauni35 milioni. Msimu uliopita alisaini mkataba mpya wa miaka mitano, lakini kiwango chake kilishuka katika msimu ambao Liverpool ilipitia kipindi kigumu.
Liverpool pia tayari imeanza kutafuta mbadala wake, huku kocha mpya Andoni Iraola akifanikiwa kumsajili winga wa Paris Saint-Germain, Bradley Barcola, kwa ada inayodaiwa kufikia Pauni123 milioni.
Barcola anatarajiwa kufika Merseyside wakati wowote kwa ajili ya vipimo vya afya kabla ya kukamilisha uhamisho wake.
Licha ya uvumi wa kuondoka, Gakpo alikuwa tayari kuendelea kubaki Liverpool baada ya kuanza msimu huu vizuri, akifunga bao moja na kutoa pasi ya mwisho iliyozalisha bao katika mechi mbili za mwanzo.
Tottenham pia ilikuwa ikimuwania mshambuliaji huyo, lakini baada ya Manchester City kuweka wazi nia yake ya kumsajili, Gakpo anaonekana kupendelea kuhamia Etihad.
Gakpo alicheza katika sare ya mabao 2-2 kati ya Liverpool na Nottingham Forest Jumamosi, akitoa pasi ya mwisho kwa Alexander Isak aliyefunga bao la kwanza la kusawazisha.
Pia alifunga bao katika mchezo wa kwanza wa Liverpool wa msimu huu dhidi ya Newcastle, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Msimu uliopita, Gakpo alicheza mechi 52 katika mashindano yote, akifunga mabao tisa na kutoa pasi sita za mwisho.
LIVERPOOL YATAKA WINGA MWINGINE
Kuwasili kwa Barcola hakutakuwa mwisho wa matumizi ya fedha kwa Liverpool katika kipindi hiki cha usajili.
Liverpool bado inatarajiwa kumsajili winga mwingine kuziba pengo lililoachwa na Mohamed Salah upande wa kulia wa safu ya ushambuliaji.
Yankuba Minteh wa Brighton na Ismaila Sarr wa Crystal Palace ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwa kwenye orodha ya Liverpool.
Brighton tayari imekataa ofa zinazofikia Pauni60 milioni kwa ajili ya Minteh, ambaye thamani yake imewekwa karibu Pauni80 milioni.
Kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler, alipoulizwa kuhusu nia ya Liverpool kumsajili Minteh amesema,“uvumi, uvumi. Tusubiri tuone kitakachotokea.
“Ni muhimu kwa wachezaji kuelewa kile walicho nacho hapa klabuni. Mashabiki walivyo karibu na timu na namna tunavyofanya kazi kwa pamoja.
“Ni vigumu kupata mazingira yanayofanana au yaliyo bora zaidi kwa wachezaji vijana wenye uwezo.
“Ukinuliza kama nitajaribu kumshawishi abaki, ndiyo, nitafanya hivyo. Lakini siwezi kudhibiti kila kitu.
“Kwa mtazamo wangu, Minteh ni mchezaji wa Brighton na anapaswa kujikita katika kuichezea klabu hii.
“Uvumi huu umetokana na mafanikio aliyopata akiwa hapa. Tumefanya vizuri kama timu na hilo limemfanya aonekane zaidi, hivyo tusubiri tuone kitakachotokea.”
Kwa upande mwingine, Sarr anaaminika kuwa chaguo la bei nafuu zaidi kwa Liverpool kati ya wachezaji hao wawili.
Crystal Palace hivi karibuni ilimuuza beki Daniel Munoz kwenda Nottingham Forest kwa Pauni22 milioni.