Frank Lampard airejesha Coventry City EPL baada ya miaka 25
Muktasari:
- Kikosi cha Frank Lampard kilionekana kuzidiwa kwa muda mrefu wa mchezo, lakini pointi moja ilitosha kuhakikisha wanapata nafasi hiyo ya kihistoria kurejea EPL.
Coventry City imefanikiwa kurejea Ligi Kuu England (EPL) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2001 iliposhuka, baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Blackburn Rovers katika mechi ya Championship iliyochezwa jana Ijumaa.
Kikosi cha Frank Lampard kilionekana kuzidiwa kwa muda mrefu wa mchezo, lakini pointi moja ilitosha kuhakikisha wanapata nafasi hiyo ya kihistoria kurejea EPL.
Mshambuliaji wa pembeni wa Blackburn, Ryoya Morishita, aliitanguliza timu yake dakika ya 54, kabla ya Bobby Thomas kusawazisha dakika sita kabla ya mwisho wa mchezo na kuwafurahisha mashabiki wa Coventry.
Matokeo hayo yameifanya Coventry kuwa na tofauti ya pointi 11 dhidi ya Ipswich Town iliyopo nafasi ya pili, na pointi 13 mbele ya Millwall inayoshika nafasi ya tatu.
Timu mbili za juu hupanda moja kwa moja, huku zile za nafasi ya tatu hadi ya sita zikicheza mechi za mtoano kuamua timu ya mwisho kupanda.
Kikosi cha Lampard kimeonyesha ubora mkubwa msimu mzima kikiwa na safu bora ya ushambuliaji na ulinzi imara zaidi. Coventry ilishiriki ligi kuu kwa miaka 34 kuanzia 1967 hadi 2001, huku taji lao pekee kubwa likiwa ni FA Cup walilolitwaa mwaka 1987.
Kwa upande wa Blackburn, sare hiyo imeiacha katika nafasi ya 16, ikiwa juu kwa nafasi tatu na pointi tano dhidi ya mstari wa kushuka daraja.