Financial Fair Play na umuhimu wake kwenye soka - 1
UEFA Financial Fair Play. Kifupi chake ni (FFP). Ni kanuni ya udhibiti iliyotungwa na Umoja wa Mashirikisho ya Vyama vya Soka Ulaya – UEFA ili kuzidhibiti klabu za kulipwa za mchezo wa soka kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato yao kwa ajili ya kufukuzia mafanikio ya muda mfupi mchezoni.
Lengo lake kuu la udhibiti huo ili kuzifanya klabu hizo kuwa na maendeleo endelevu na si kufanya matumizi makubwa kwa wakati fulani kuzidi mapato yakayotishia usalama wa klabu husika katika kujiendeesha.
Mfano rahisi tu, kaka wewe mwanaume kipato chako halisi kinakizi kumudu kugharimia wake wawili, basi usiongeze wawe wanne hautakuwa na maendeleo endelevu, utakufa.
Udhibiti huo lengo lake ni kuzifanya klabu zisiingie kwenye tatizo la kipesa ambayo yatatishia usalama wao wa kudumu kwa muda mrefu.
Baadhi wanadai kwamba kanuni hiyo imeanzishwa ili kudhibiti utakatishaji pesa unaoweza kufanyika kwenye klabu ndogo. Kanuni hiyo ilikubalika Septemba 2009 na Kamati ya Udhibiti wa Fedha iliyopo chini ya UEFA.
Kanuni hiyo inajumuisha adhabu mbalimbali zinazoweza kuchukuliwa kama kutakuwa na klabu iliyozidisha matumizi kuliko mapato kwa misimu kadhaa kwa kuzingatia bajeti yao.
Kanuni hizo za udhibiti zilianza kufanya kazi katika msimu wa soka wa 2011–12. Adhabu maarufu zaidi ni ya kuondolewa kwenye michuano ya Ulaya. Adhabu nyingine ni kutozwa fainali, kuondolewa zawadi ya pesa na kufungiwa kufanya usajili wa wachezaji wapya.
Adhabu nyingine pia zinaweza kutofautiana kulingana na chama cha soka cha nchi husika, lakini nchi zote kama wanachama wa Uefa watafuata msingi mkuu wa kudhibiti matumizi yasiwe makubwa kuzidi uwezo na kipato.
Klabu zimekuwa zikiingia kwenye madeni makubwa kutokana na kutumia pesa nyingi kuliko kiwango inachoingiza. Hivyo, Uefa katika kuzilinda klabu zake ilikuja na kanuni hiyo huku ikitaka kuweka usawa pia kusiwepo na pengo kubwa baina ya timu moja na nyingine kwenye soko la usajili.
Timu zote zinazoshiriki michuano ya Uefa hazina budi kukubaliana na misingi hiyo, ziishi kwenye uwezo wa mapato yao hasa kwa kipindi hiki ambacho klabu nyingine zimekuwa zikimilikiwa na mabilionea wenye pesa ndefu, ambao wanaweza kutumia pesa zao za biashara tofauti kwenye soka.
Wamiliki wa klabu wenye pesa nyingi wanafahamu wazi utaratibu unaopaswa kufuatwa na sio kuwekeza pesa nyingi tu kwenye klabu, la watalazimika kuuza wachezaji iliyowasajili ili iwe timu yenye faida iweze kuendelea na mambo mengine.
Mpango huo uliibuka wakati Uefa ilipokuwa chini ya rais Michel Platini na ulikubalika na sehemu kubwa ya wamiliki wa klabu kwamba kamati huru ya majaji itaundwa kuzungumza kama kutakuwa na klabu imevunja sheria za udhibiti.
Licha ya lengo kubwa ilikuwa kuzidhibiti klabu zenye wamiliki mabilionea wenye pesa nyingi zisitumie pesa za biashara zao tofauti kwenye soka na imekubalika vyema, FFP inashutumiwa pia imeshindwa kuleta ahueni kwenye masoko ya usajili wa ndani, inashindwa kuzipunguzia klabu madeni.
Mwaka 2015, UEFA ilitangaza FFP ingerahisishwa zaidi, huku ikielezwa hiyo imetokana na kuwamo kwa kesi kadhaa zilizofunguliwa juu ya utaratibu wa kanuni hiyo.
FFP ilivyoanza
Mwaka 2009 UEFA taarifa yake ilifichua kwamba zaidi ya klabu 655 za Ulaya zilipata hasara katika mwaka uliopita, licha ya kuwapo kwa kundi dogo ambalo liliweza kuvumilia upotevu mkubwa wa pesa kutokana na utajiri wa wamiliki wao, huku asilimia 20 ya klabu zilizowekwa kwenye utafiti zilizonyesha kuwa kwenye hatari ya kipesa. Jambo hilo lilikuja kuwekwa sawa kuanzia mwaka 2010 hadi 2012 kwenye ripoti za mabingwa ya Ulaya juu ya utawala kwenye soka.
Wamiliki wa klabu walikuwa na maono tofauti na uwezo wa mameneja wao katika kutimiza malengo ya klabu. Jambo hilo limezisukuma timu hiyo wamiliki wake kuwa na kawaida ya kwenda kukopa ili kutengeneza vikosi ambavyo inajikuta inavilipa mishahara mikubwa tofauti na pointi wanazovuna.
Wamemiliki wa timu wamekuwa wakikopa kwa ajili ya kupata mafanikio na kwamba si timu zote zinaweza kufanikiwa.
Kumekuwa na mifano mingi ya kuhusu klabu ambazo wakurugenzi wake, ambao ni mashabiki wakubwa wa klabu hiyo wamekuwa wakikimbizia ndoto zao kwa kucheza kamali ya kuwekeza kwenye mipango ya muda mfupi au kukopa pesa kuwekeza kwenye miradi ya aina hiyo kwa madhumuni ya kuwa na maendeleo ya muda mrefu.
Msukumo wa wakurugenzi wa klabu kutaka kuwekeza kwenye klabu, kusajili wachezaji mastaa limekuwa jambo ambalo wakati mwingine linakera mashabiki wa muda mrefu kwa sababu timu zao zinashindwa kuwa na maendeleo ya muda mrefu.
Hata miongoni mwa klabu kubwa za Ulaya, kuendeleza matumaini makubwa yanatazamwa na wakuu wa klabu hiyo kama jambo muhimu la kuzifanya kuendelea kuwa washindani.
Jambo hilo limekuwa likilalamikiwa kwamba kuna klabu zimekuwa zikifanya matumaini makubwa kuliko vipato na kuwa na nguvu kubwa kwenye michuano ya Ulaya. Usawa haupo.
Sehemu kubwa ya madeni makubwa kwenye soka la Ulaya yapo kwenye Ligi Kuu tatu kubwa: Ligi Kuu England (England), Serie A (Italia) na Ligi Kuu ya Hispania maarufu La Liga.