Fenerbahce yamtaka Rashford
Muktasari:
- Rashford amerejea Old Trafford baada ya kumaliza kipindi cha mkopo cha mafanikio akiwa Barcelona, huku kocha wa miamba hiyo ya Hispania, Hansi Flick, akikiri kuwa atamkosa nyota huyo baada ya klabu hiyo kuamua kutomnunua moja kwa moja.
LONDON, ENGLAND: KLABU ya Fenerbahce ya Uturuki ipo tayari kuvunja benki ili kumsajili mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford, katika moja ya usajili mkubwa unaotarajiwa kufanyika dirisha hili la kiangazi.
Rashford amerejea Old Trafford baada ya kumaliza kipindi cha mkopo cha mafanikio akiwa Barcelona, huku kocha wa miamba hiyo ya Hispania, Hansi Flick, akikiri kuwa atamkosa nyota huyo baada ya klabu hiyo kuamua kutomnunua moja kwa moja.
Kwa mujibu wa taarifa, Rashford ni mmoja wa wachezaji watatu waliopo kwenye orodha ya vipaumbele ya Fenerbahce. Wengine ni winga wa AC Milan, Rafael Leao, na mshambuliaji wa Crystal Palace, Ismaila Sarr.
Inaelezwa kuwa Fenerbahce tayari imeanza mazungumzo na Leao, lakini bado haijafikia makubaliano, huku pia ikiwa imewasiliana na wawakilishi wa Sarr na Rashford ili kuchunguza uwezekano wa kuwanasa nyota hao.
Uongozi wa Fenerbahce unataka kumpa kocha mpya, Ismail Kartal, kikosi imara kitakachoweza kushindana na wapinzani wao wakubwa, Galatasaray, katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Uturuki.
Baada ya kuisaidia England kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia 2026, Rashford anatarajiwa kuchukua muda kabla ya kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wake.
Hata hivyo, Fenerbahce inaelezwa kuwa ipo tayari "kuvunja benki" ili kumshawishi nyota huyo wa England kuhamia nchini Uturuki.
SARR PIA AWANIWA
Mbali na Rashford, Ismaila Sarr pia ameivutia Fenerbahce baada ya kuwa na msimu bora akiwa Crystal Palace.
Mshambuliaji huyo wa Senegal alifunga mabao 21 na kuisaidia Palace kutwaa ubingwa wa UEFA Europa Conference League, huku pia akifunga mabao manne kwenye Kombe la Dunia 2026 na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Senegal katika historia ya mashindano hayo.
Hata hivyo, Crystal Palace inataka kumbakiza nyota huyo na ipo tayari kuanza mazungumzo ya kumpa mkataba mpya, ingawa haitazuia kuondoka kwake endapo atapata nafasi nzuri ya kucheza katika klabu nyingine barani Ulaya.