Fenerbahce yamkomalia Rashford
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo ambaye amesharudi kikosini na kuanza kucheza mechi ya maandalizi ya msimu mpya, anadaiwa kuwa na ofa nyingi mezani lakini mwenyewe anataka kusalia katika ligi tano bora Ulaya zenye ushindani mkubwa Ulaya.
FFENERBAHCE imerudi tena Manchester United ikimtaka mshambuliaji wa timu hiyo na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, mwenye umri wa miaka 28.
Mshambuliaji huyo ambaye amesharudi kikosini na kuanza kucheza mechi ya maandalizi ya msimu mpya, anadaiwa kuwa na ofa nyingi mezani lakini mwenyewe anataka kusalia katika ligi tano bora Ulaya zenye ushindani mkubwa Ulaya.
Rashford ambaye msimu uliopita aling’ara akiwa na Barcelona kwa mkopo, kwa sasa amerejea Manchester United akisikilizia ofa kutoka timu kubwa za Ulaya baada ya Barca kugoma kumnunua kwa zaidi ya Pauni 35 milioni ambazo waajiri wake wamemwekea kwenye ofa kwa klabu inayomtaka.
Mchezaji huyo ambaye ni zao la akademi ya Manchester United ameendelea kushawishiwa na timu mbalimbali kujiunga nazo kutokana na kiwango alichoonyesha alipokuwa Barcelona, ambapo Bayern Munich na Atletico Madrid ni miongoni mwa zile zilizoonyesha nia ya kumtaka awali, ingawa hazijarudi tena.
Hata hivyo, Man United imeendelea kuonyesha nia ya kuendelea kumtumia kwa msimu ujao, ambapo kocha mpya, Michael Carrick ameshazungumza na wawakilishi wa mchezaji huyo kuwaelezea yupo kwenye mipango yake.
Marc Bernal
ASTON Villa inapanga kutoa ofa ya Pauni 30 milioni kwa ajili ya usajili wa kiungo wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Marc Bernal, mwenye umri wa miaka 19. Hata hivyo, mchezaji huyo anadaiwa kuuambia uongozi wa Barca usimuuze ili abakie kupigania namba katika kikosi cha kwanza msimu ujao.
Curtis Jones
INTER Milan inaendelea kumfukuzia kiungo wa Liverpool, Curtis Jones, lakini italazimika kuongeza dau baada ya Liverpool kuweka thamani ya euro milioni 40. Jones hakuwamo kwenye kikosi cha Liverpool wiki hii, hali iliyoongeza tetesi kuhusu mustakabali wake. Inter iliwahi kujaribu kumsajili Januari, lakini ofa yake ilikataliwa na Liverpool.
Robbie Ure
SEVILLA iko hatua za mwisho kumsajili mshambuliaji wa Scotland U21, Robbie Ure, kutoka IK Sirius ya Sweden. Dili hilo linaweza kufikia Euro 9.2 milioni, huku Ure, 22, akitarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusaini mkataba wa miaka mitano. Sevilla inaamini nyota huyo ataongeza nguvu katika safu yake ya ushambuliaji.
Endrick
MSHAMBULIAJI wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Endrick, 20, ameanza kuvutia macho ya AS Roma katika dirisha hili la usajili wa kiangazi, ingawa Lyon pia inataka kumbakiza Ufaransa. Wawakilishi wa mchezaji huyo wanataka kumbakiza Real Madrid ambako alianza kutengeneza jina kabla ya kutimkia Lyon.
Wilson Isidor
SUNDELAND haitamuuza mshambuliaji wa Haiti, Wilson Isidor, mwenye umri wa miaka 25, msimu huu wa kiangazi licha ya kuvutiwa na klabu kadhaa hasa West Ham United. Isidor anataka kuondoka Sundeland ili aende timu atakayopata namba katika kikosi cha kwanza baada ya kuingia mara chache chache kikosini msimu uliopita.
Nahuel Molina
BEKI wa Atletico Madrid, Nahuel Molina, anatarajiwa kusafiri kwenda Italia kwa ajili ya vipimo vya afya kabla ya kukamilisha uhamisho wake kwenda AS Roma. Roma itamlipa Atletico euro milioni 13 kama ada ya awali, huku kukiwa na nyongeza ya euro milioni nne kulingana na vigezo vya mkataba, hivyo dili kufikia euro milioni 17.
Mykhailo Mudryk
COVENTRY City ni miongoni mwa timu tatu za Ligi Kuu England zinazomtaka winga wa Chelsea na timu ya taifa ya Ukraine, Mykhailo Mudryk, mwenye umri wa miaka 25. Mchezaji huyo alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na tuhuma za matumizi ya dawa zilizopigwa marufu michezoni, lakini ameshinda kesi.
Cody Gakpo
LIVERPOOL haina mpango wa kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa Uholanzi, Cody Gakpo, mwenye umri wa miaka 27, licha ya Tottenham Hotspur kuonyesha nia ya kumsajili. Gakpo ameelezea nia ya kubaki Liverpool, lakini klabu yake imefungua milango kusikiliza ofa kutoka timu mbalimbali.
Adam Wharton
MANCHESTER United imeanza kumfukuzia kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton. United inataka kumuongeza ili kuimarisha safu ya kiungo, lakini Palace imeweka bei kubwa. Klabu hiyo inataka karibu euro milioni 100 kwa mchezaji huyo anayeweza kucheza nafasi ya kiungo mkabaji.