Prime
Ibrahim Doumbia ana kesi ngumu dhidi ya Jamhuri ya soka
IBRAHIM Doumbia sijui kama aliambiwa Tanzania ni nchi ya namna gani. Sijui anajisikiaje popote alipo. Sijui kama anaambiwa ukweli mtupu kuhusu kinachoendelea kuhusu yeye. Sijui. Ninachojua ni kwamba ana kesi ngumu dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa mashabiki wa mpira Tanzania. Sijui atavuka vipi.
Jina lake linaweza kuwa maarufu zaidi katika mpira kwa sasa, lakini limekuwa maarufu kwa sababu hasi. Sio sababu chanya. Mashabiki wa timu zote mbili kubwa za Kariakoo wamemgeuza kuwa kichekesho. Timu anayochezea Simba na timu pinzani Yanga. Anaonekana kama vile ni mzaha uliokuja katika mpira wetu.
Kuna nadharia tatu hadi nne tofauti. Simba wamekuwa wakipitia katika nyakati ngumu za kurudisha makali na utawala wao. Wanapambana sana. Inategemewa kwamba walete wachezaji wakali wa kupambana na Yanga. Hata hivyo katika hisia za mashabiki wa Simba inaonekana kama vile Doumbia sio mchezaji sahihi. Simba wanahisi kwamba wamepigwa kwa kumleta Doumbia.
Sijui nani anafuatilia masuala ya ubora wa wachezaji watarajiwa pale Simba. Hata hivyo, kwa yeyote ambaye aliamua achukuliwe itakuwa ana sapoti nzuri za namba za Doumbia kutoka alikotoka. Alifunga mabao 17 ya Ligi Kuu Mali katika mechi 24 alizocheza. Mchezaji wa Afrika Magharibi akifunga mabao hayo ujue ana kitu. Na pia alipika mabao matano.
Katika ligi yetu Doumbia amegeuzwa kuwa kichekesho. Mashabiki wa Simba na baadhi ya viongozi hawajaridhishwa na ubora wake. Presha imekuwa kubwa. Kuna nyakati najiuliza kwamba baada ya takwimu zake katika Ligi Kuu Mali ina maana ligi yetu imekuwa bora sana kiasi kwamba mshambuliaji wao bora anaweza kugeuka kuwa kichekesho katika ligi yetu? Nafungua mjadala.
Hapo hapo watani wa Simba ambao ni Yanga wamekuwa wakitumia nafasi hii kuwavuruga kisaikolojia Simba. Wanawacheka zaidi watani kwa ajili ya kuwavuruga kiasi kwamba watani wenyewe hawataki kusimama na mchezaji wao na wameamua kumshambulia mchezaji wao. Hapa ndipo ninaposema Doumbia ana kesi ngumu dhidi ya Jamhuri. Kule wanamshambulia na huku wanamshambulia.
Haya yanatokea wakati Simba inapitia nyakati ngumu. Sio kwamba Yanga inapatia sana katika usajili. Hapana. Ni kwa sababu inapitia nyakati nzuri ndani ya uwanja. Inaweza kumsajili mchezaji wa ovyo na asisemwe sana kwa sababu tu timu inapata matokeo ambayo wanayataka.. kesi kwa injinia Hersi Said inakuwa nyepesi. Ni kama ilivyo kwa kesi ya Buba Jammeh.
Buba angekuwa ameenda Simba ingekuwa kesi ngumu, lakini kwa sababu alikwenda Yanga inaonekana ni kesi nyepesi. Ni kwa sababu tu Yanga wanapitia nyakati nzuri. Kama Doumbia angeenda Yanga tusingemsema sana, lakini kwa vile amekwenda kwa wakubwa wenye kiu ya kurudisha ufalme tunajiuliza mambo mengi dhidi ya walioamua kumleta.
Na sasa tuna Doumbia mkononi. Nikimtazama kama mchezaji nagundua kwamba sio mchezaji mbaya kama inavyotajwa. Niliambiwa kwamba ni hodari wa mipira ya vichwa na niliona hilo katika bao alilofunga mechi ya pili ya Simba kule Kigali katika michuano ya Kagame. Kama Doumbia ni bora kama vile, basi Simba hawachezi kwa kutumia uwezo wake bali wanacheza kwa kutumia upungufu wake.
Doumbia ni mzuri juu, lakini Simba ni wazuri chini. Kina Anicet Oura, Libasse Gueye na Ellie Mpanzu wao ni watu wa kukokota chini na kutafuta nafasi za chini. Doumbia ni wale washambuliaji wa kizamani wanaovizia kufunga kwa vichwa katika boksi kama kina Abeid Mziba. Simba walimsajili wakijua hili? Sijui kama tuna usajili wa kisayansi. Ninachojua ni kwamba waliangalia namba zake bila kujua wao huwa wanacheza vipi.
Doumbia sio mzuri miguuni. Anaonekana kuwa kichekesho katika mipira ya miguuni. Kwa mipira ya juu pia nimeendelea kuwa shabiki wake kwa sababu ya bao alilofunga Kigali, lakini hata hivyo hajaendelea kunishawishi sana baada ya kumtazama mechi dhidi ya Yanga na mechi ya juzi dhidi ya Kagera Sugar. Hakuonekana kama ataendelea kunishawishi tena na tena.
Kinachonishangaza ni kitu kimoja. Msimu uliopita kocha wa Simba, Steve Barker alipendelea kumtumia Mpanzu kama mshambuliaji feki wa mbele badala ya kumtumia Selemani Mwalimu ambaye ni mshambuliaji asilia. Mwalimu alikuwa akiishia benchi zaidi katika mechi nyingi kubwa na ndogo.
Licha ya ukweli kwamba ukiwauliza watu wengi watakwambia kwamba Mwalimu ni bora zaidi ya Doumbia, lakini msimu huu Barker amekuwa akimtumia zaidi Doumbia kama mshambuliaji asilia na Mpanzu amekuwa akikaa benchi.
Je kocha amebadili mbinu au kumekuwa na shinikizo la nje la kumpanga Doumbia? Kwanini alikuwa hampangi Mwalimu na alikuwa anampanga Mpanzu lakini sasa hivi hampangi Mpanzu na amekuwa akimpanga Doumbia?
Kwamba aliyemleta Doumbia anashinikiza Doumbia apangwe ili yeye ajiokoe sina uhakika na hilo. Kwamba kocha anampanga kila mara Doumbia kwa sababu ana uhakika na uwezo wake na amekuwa akimuongezea uwezo wa kujiamini hili pia ni jambo la kufikirika na makocha wengi wa wamekuwa wakitumia mbinu hii kila kukicha. Unasimama nyuma ya mchezaji wako bila ya kujali kelele za jukwaani.
Vyovyote ilivyo Doumbia ana kesi ngumu ya kujibu kwa Jamhuri. Katika mpira wetu sijawahi kuona mchezaji aliyedharauliwa kisha akasimangwa, kisha akakejeliwa katika kiwango hiki cha Doumbia halafu akaibuka kuwa shujaa na kutufumba midomo.
Iliwahi kuwatokea wachezaji kadhaa lakini haikufika kiwango hiki cha Doumbia. Kwamba mashabiki wa timu yake na timu pinzani wote wameibuka kumkejeli kisha akawafumba midomo mashabiki wote. Sijawahi kuona.
Doumbia ana kazi ngumu ya kufanya. Inapotokea mashabiki wa timu yako wanasubiri ukosee ili walaumu maisha yanakuwa magumu kwako. Binafsi namtazama katika jicho la kuwafumba midomo wote ambao wanamtazama kwa jicho hilo.
Kitakuwa kitu cha kuvutia kama baada ya miezi michache Doumbia ataibuka shujaa. Itakuwa kama filamu nzuri ya kusisimua ya mtu aliyetokea jalalani kuja kuwa rais wa nchi.
Yote haya yapo katika mikono yake. Dirisha la usajili limefungwa na hofu yangu imetoweka. Nilikuwa na hofu kwamba huenda jina lake lingekatwa kabla ya kufungwa kwa dirisha majuzi. Simba na Yanga hawahofii hasara hizi. Na tayari nilisikia mahala kwamba wazo hilo lilikuwepo.
Kama akiendelea kufanya vibaya, basi atakuwa amemdhalilisha mtu ambaye alipambana kumleta. Itakuwa hadharani kwamba Simba wanajihujumu wenyewe. Wakati Yanga wakiwa katika ubora wao huku Simba wakiwa wamekosea mara nyingi katika madirisha ya uhamisho ya miaka ya karibuni inakuwaje unamleta mchezaji kama yeye?
Ni Doumbia tu ndiye ambaye anaweza kumtetea mtu ambaye alimleta. Bahati nzuri anapata nafasi kwa kocha wake. Inabidi amtetee aliyemleta lakini pia amtetee kocha Steve Berker.
Doumbia ana kesi nyingi za kujibu dhidi ya Jamhuri. Kila mtu yupo dhidi ya yeye. Simba na Yanga wote wapo dhidi ya yeye. Inabidi awafunge watu midomo. Sio kazi rahisi kwa sababu kuna washambuliaji wengi wazuri wanaisubiri nafasi yake Msimbazi.
Tusubiri na kuona mambo anayoweza kufanya ndani ya mechi kumi zijazo pale Msimbazi. Vinginevyo Simba kama walivyo watani zao Yanga au mdogo wao Azam huwa hawaoni aibu ya kuingia hasara ndogo ndogo kama hizi.