Prime
Fei Toto anavyoipitisha Azam kwenye ‘chuma cha moto’
DIRISHA kubwa la usajili kwa ajili ya msimu wa 2026/27 lilifungwa rasmi usiku wa Jumamosi, Agosti 15 kuamkia Jumapili, Agosti 16, 2016.
Kufungwa kwa dirisha hilo kulihitimisha harakati ndefu za usajili zilizogubikwa na tetesi zilizomhusu Feisal Salum Abdallah maarufu kama Feitoto au Failasufi, yaani hariri laini.
Katika historia ya mpira wa Tanzania hakuna mchezaji ambaye ametawala tetesi za uhamisho kwa kila dirisha zaidi ya Feisal Salum wa Azam FC.
Tangu ajiunge na kikosi hicho cha Chamazi 2023, Feitoto amekuwa akihusishwa kuondoka kikosini humo kila dirisha na mara zote tetesi zake zimekuwa zikitawala harakati za uhamisho na kuwasisimua mashabiki wa timu zinazohusishwa naye.
Lakini, katika nyakati zote, hakuna kipindi ambacho tetesi zilikuwa kubwa na mambo yalikaribia kuwa kweli kama safari hii. Klabu ya Simba ambayo mara zote ndiyo imekuwa ikihusishwa naye sana ndiyo iliyopigana kiume zaidi safari hii. Hata hivyo, wapinzani wao wa jadi, Yanga nao hawakuwa nyuma kwenye hili.
Kimsingi ni kwamba mambo yote yaliyokuwa yakisemwa kuhusu uhamisho wa Feitoto hayakuwa yakizushwa kutoka kusikojulikana. Ni mambo ambayo yalikuwa na chanzo halisi na yakitoka kimkakati. Kwanza Feisal Salum mwenyewe huenda ndiye aliyekuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hali yake ya kimkataba.
Kila wakati hali ilipokuwa ikionekana imetulia, inawezekana yeye huwatafuta waandishi waseme kitu ili kuongeza presha kwa mabosi wake. Lengo ni kuwaweka roho juu ili ukifika wakati wa mazungumzo ya mkataba mpya awe kwenye nafasi nzuri ya kuvuna pesa nyingi.
Lakini, pili ni kutoka kwenye klabu zinazohusishwa naye, nazo pia hutoa taarifa kwa malengo tofauti. Kwa mfano, safari hii taarifa nyingi zilitoka Simba, na lengo hasa inawezekana ilikuwa kuuza jezi. Mkakati huo uliamsha soko... na walifanikiwa kwa kiasi fulani. Lakini kubwa ya hayo yote zilikuwa saa 24 za mwisho kabla kabla dirisha halijafungwa.
SAA 24 ZA MOTO
Azam FC ilikuwa Arusha kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2026/27. Wakiwa kambini kwao kwenye Hoteli ya Corridor Springs, taarifa zikawafikia kwamba Simba na Yanga wapo Arusha kuiwinda saini ya Feitoto. Taarifa zikadai kwamba wababe hao wa Kariakoo wanataka Feisal Salum asaini tu mkataba na kitakachoendelea awaachie wao.
Yanga walituma watu wao wakafikia hoteli moja ambayo ipo jirani na hoteli waliyofikia Azam kwa ajili ya kufanikisha hilo. Azam FC wakafanya uchunguzi na kubaini kweli kuna mtu wa Yanga alikuwepo. Mtu huyo ni kiongozi mkongwe wa Yanga ambaye amehudumu klabuni hapo kwa muda mrefu.
Kwa upande wa Simba pia Azam FC walipata taarifa kwamba nao wapo kazini na wanamtumia kiongozi mmoja mkubwa wa serikali ambaye ni shabiki wao mkubwa aliyekuwapo mjini Arusha. Na hili lilipata nguvu kwao baada ya kigogo mmoja wa Wekundu hao kupiga simu kwa mmoja wa wamiliki wa Azam FC, kutangaza nia rasmi ya kumnunua Feitoto. Kigogo huyo wa Simba alitoa ofa ya Sh4 bilioni.
Mmiliki huyo wa Azam FC alimkatalia kistaarabu kwa kumwambia kwamba uamuzi wa kumuuza Feisal Salum hauzingatii tu pesa iliyopo mezani, bali utashi wa bodi ya klabu kwa ushauri wa kiufundi wa kocha Florent Ibenge.
HOFU KAMBINI
Taarifa za kwamba kuna mkataba unaoweza kupenyezwa kwa siri kambini ili Feisal asaini ziliwavuruga Azam FC na kumuwekea ulinzi mkali. Na tabia fulani za mchezaji huyo pale kambini ziliwatia shaka. Feisal hakuwa sehemu ya kikosi cha mechi dhidi ya Polisi Tanzania siku hiyo kutokana na adhabu ya kufungiwa kufuatia kadi nyekundu aliyoipata kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kule Pemba.
Kwa hiyo alikuwa na programu yake maalumu ya mazoezi, lakini siku ile akaamka akisema hawezi kufanya mazoezi hayo kwa sababu anaumwa.
Kengele ya tahadhari ikalia vichwani mwa watu waliopewa jukumu la kuhakikisha kila kitu kinakuwa salama. Wakahisi kwamba labda anataka asiende uwanjani jioni ili abaki hotelini na mkataba uletwe.
Papo hapo ukawekwa ulinzi mkali zaidi ndani ya kambi na kwenye hoteli aliyoonekana mtu wa Yanga. Ulinzi ulikuwa mkali sana kuepuka yasitokee ya Selemani Mwalimu na Simba. Ulipofika wakati wa kwenda uwanjani, Feisal akasema anajisikia vizuri na hatabaki hotelini, ikawa nafuu.
Na kweli akaenda uwanjani na ndipo alipoonekana akiwa kwenye chumba cha mtangazaji wa Azam TV akiwa kama mtangazaji namba mbili.
HATIMA YAKE BADO TETE
Japokuwa Azam FC wamefanikiwa kumbakisha Feisal, lakini yawezekana hatabaki klabu hapo baada ya mkataba wake na zadi yawezekana hata mkataba huu asiumalize. Taarifa zinadai Azam FC ilikataa ofa kubwa kutoka Libya ya Dola 5 milioni (Takriban zaidi ya Sh13 bilioni).
Ofa hii pia ilikuja na maslahi makubwa kwa mchezaji mwenyewe. Baada ya kuikataa, Feisal anataka Azam FC wampe kiasi kilekile ambacho angepata Libya. Nacho ni mshahara wa Sh100 milioni kwa mwezi na bilioni tatu za kusaini mkataba. Azam haipo tayari kulipa kisasi hicho na sasa inafikiria kuikubali ofa ile ili wamuuze. Hii ni kwa sababu madai yake hayana afya ya kiuchumi kwa klabu.
Mkataba wake wa sasa aliosaini Julai 2025 umeleta shida kwa wachezaji wengine. Kila mchezaji ambaye mkataba wake umeisha anataka malipo makubwa kama Feisal na wakikubali matakwa ya sasa hali itakuwa mbaya zaidi, na ndipo wanapoona bora aondoke. Bodi ipo kwenye majadiliano kuona hili linawezekanaje. Lakini, hata hivyo, saa 24 za mwisho za usajili zilikuwa za moto sana kwa Azam FC.