Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyemkosoa Infantino atimuliwa

Muktasari:

  • FIFA imethibitisha kuwa uhusiano wa kikazi kati yake na Lamour ulikoma rasmi Agosti 17, 2026, baada ya mtendaji huyo kuhudumu kwa takribani miaka miwili tangu alipoteuliwa Novemba 2024.

ZURICH, USWISI: AFISA Mkuu wa Uendeshaji wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Kevin Lamour, ameondoka madarakani wiki chache baada ya kukosoa hadharani uongozi wa Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kuhusu mpango wa kuuza hisa katika Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.

FIFA imethibitisha kuwa uhusiano wa kikazi kati yake na Lamour ulikoma rasmi Agosti 17, 2026, baada ya mtendaji huyo kuhudumu kwa takribani miaka miwili tangu alipoteuliwa Novemba 2024.

Katika taarifa yake, FIFA ilisema Lamour na taasisi hiyo wamekubaliana kutengana baada ya mazungumzo na kuzingatia kwa makini suala hilo.

“FIFA inamshukuru Kevin kwa miaka yake miwili ya utumishi na inamtakia kila la heri katika maisha yake ya baadaye,” ilisema taarifa hiyo, huku ikisisitiza kuwa haitatoa maelezo zaidi kuhusu kuondoka kwake.

Lamour alijikuta kwenye mgogoro baada ya kuvunja ukimya na kuupinga vikali mpango wa Infantino wa kutafuta wawekezaji binafsi ambao ungehusisha uuzaji wa hisa katika mashindano ya Kombe la Dunia.

Mpango huo uliokuwa ukikosolewa kwa muda, hatimaye uliachwa, huku Lamour akisema wafanyakazi wa FIFA walikuwa “wamedanganywa” kuhusu mpango huo.

Akizungumza na Associated Press (AP), Lamour alisema mpango huo ulikuwa wa mtu mmoja na kwamba viongozi wa kisiasa wa soka walipaswa kujiuliza maswali sahihi na kuchukua maamuzi yanayofaa.

“Ni mradi wa mtu mmoja. Mradi huu haupaswi kuendelea na wakati umefika kwa viongozi wa kisiasa wa soka kujiuliza maswali sahihi na kufanya maamuzi sahihi,” alisema.

Lamour pia alionyesha kuwa alikuwa tayari kupoteza kazi yake kutokana na msimamo wake.

“Ikiwa hiyo inamaanisha nitapoteza kazi yangu, basi iwe hivyo. Nitaelewa na kuheshimu uamuzi huo. Angalau nitalala kwa amani usiku huu,” alisema.

Kuondoka kwa Lamour kumeibua maswali zaidi ndani ya FIFA, hasa kwa kuwa kunafuatia pia kuondoka kwa mshauri mwandamizi wa Infantino, Carlos Cordeiro, ambaye alijiuzulu Julai akieleza kutofautiana na mpango huo wenye utata.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, wafanyakazi wa FIFA walipewa taarifa kuhusu kuondoka kwa ghafla kwa Lamour kupitia barua pepe iliyotumwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafström, Jumanne usiku.

Pia kumekuwa na madai Grafström ndiye aliyemfukuza Lamour badala ya Infantino, ingawa FIFA bado haijatoa maelezo ya wazi kuhusu madai hayo.

Lamour alijiunga na FIFA Novemba 2024 na katika kipindi chake alisimamia mabadiliko kadhaa ndani ya taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano na wadau pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali muhimu.

Kuondoka kwake kunakuja wakati FIFA ikiendelea kukabiliwa na mjadala kuhusu namna mashindano ya Kombe la Dunia yanavyopaswa kuendeshwa kibiashara na nani anayepaswa kunufaika na mapato yake.