Rodri atua Barcelona
Muktasari:
- Rodri, ambaye alizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua Barcelona, alisema amefurahia kurejea nchini kwao na kujiunga na Barcelona.
BARCELONA, HISPANIA: NAHODHA wa Hispania, Rodri, amewasili jijini Barcelona tayari kukamilisha uhamisho wake wa Pauni 65.4 milioni (takriban Sh bilioni 220) kutoka Manchester City.
Rodri, ambaye alizungumza na waandishi wa habari baada ya kutua Barcelona, alisema amefurahia kurejea nchini kwao na kujiunga na Barcelona.
“Nina furaha kuwa hapa. Zimekuwa siku chache zenye presha kubwa, lakini ninafuraha sana kuwa hapa. Kuichezea Barcelona ni ndoto. Tunakwenda kupigania Ligi ya Mabingwa na kila kitu kingine kitakachokuja,” alisema Rodri.
Kiungo huyo anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya leo kabla ya kutambulishwa rasmi kama mchezaji wa Barcelona, tukio linaloweza kufanyika leo mchana.
Rodri atasaini mkataba wa miaka minne utakaomuweka Barcelona hadi 2030, ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya kuiongoza Hispania kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.
Uhamisho huo unahitimisha kipindi chake cha miaka saba akiwa Manchester City, kabla ya sasa kurejea nchini Hispania.
Rodri alikubaliana kujiunga na Barcelona wiki mbili zilizopita baada ya kuijulisha Real Madrid kwamba hataki tena kujiunga na klabu hiyo.
Hata hivyo, mwanzoni Barcelona ilitoa ofa ambazo zilikuwa chini ya kiwango cha Pauni 68 milioni ambacho Manchester City ilikuwa ikihitaji. Mazungumzo yaliendelea hadi Barcelona kufikia thamani iliyowekwa na City.
Rodri alisafiri kwenda Hispania Jumatatu jioni na sasa anatarajiwa kukamilisha taratibu za mwisho kabla ya kuwa rasmi mchezaji wa Barcelona.
Kiungo huyo alirejea Manchester kutoka mapumzikoni Alhamisi, baada ya kushinda Kombe la Dunia, akisafiri kwa ndege ya Ryanair kutoka Madrid hadi Liverpool. Hata hivyo, hakuhusika katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao City ilipoteza dhidi ya Arsenal.