Emiliano bado awachanganya vigogo Manchester United
Muktasari:
- Man United imekuwa ikihusishwa na huduma ya fundi huyu kwa muda mrefu kutokana na madhaifu ambayo kipa wao Andre Onana ameyaonyesha tangu ajiunge nao.
MANCHESTER United bado inafanya majadiliano ya ndani kwa ajili ha kumsajili kipa wa Aston Villa na timu ya taifa ya Argentina, Emiliano Martinez dirisha hili, lakini wanarudishwa nyuma na ada ya uhamisho ya Pauni 40 milioni ambayo Aston Villa inaihitaji ili kumwachia kipa huyo.
Man United imekuwa ikihusishwa na huduma ya fundi huyu kwa muda mrefu kutokana na madhaifu ambayo kipa wao Andre Onana ameyaonyesha tangu ajiunge nao.
Martinez alionekana kuaga katika mechi ya mwisho ya msimu uliopita hali iliyoanza kuibua tetesi anaweza akaondoka dirisha hili.
Tangu kuisha kwa msimu uliopita amekuwa akiwindwa na vigogo mbalimbali barani Ulaya, lakini Man United ndiyo inayoonekana kuwekeza nguvu zaidi.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizikª mwaka 2029 na timu nyingi zimekuwa zikikataa kutoa Pauni 40 milioni zinazohitajika kutokana na umri wake.
Man United inapamba kuona ikiwa Villa itakubali kumwachia kwa kiasi kisichozidi Pauni 25 milioni na hata kwa kiasi hicho itangoja kwanza ikimuuza Sancho ndio imnunue yeye.
Inaelezwa Martinez mwenyewe anatamani sana kujiunga na mashetani hao wekundu kwa sababu ya ofa nono ambayo wameiweka mezani ambayo iandaiwa kuwa ni mshahara unaofikia Paunj 200,000 kwa wiki.
James Trafford
NEWCASTLE United iko hatarini kupitwa na Manchester City katika juhudi zao za kumnunua kipa wa Burnley na England, James Trafford, mwenye umri wa miaka 22 katika dirisha hili. Inaelezwa benchi la ufundi la Man City linamwona kipa huyu kama mbadala sahihi wa Ederson ambaye kuna uwezekano akaondoka dirisha hili na timu nyingi ikiwemo Galatasaray na Fenerbahce zinaonekana kuwa katika vita kali kwa ajili ya kumpata. Trafford anadaiwa kutamani zaidi kwenda Man City katika dirisha hili.
Tino Livramento
INAELEZWA Newcastle inataka kumpa mkataba mpya beki wao Tino Livramento dirisha hili ili kuzima tetesi na harakati za Manchester City inayohitaji saini yake pia. Tovuti ya The Times inadai Man City iko tayari kulipa Pauni 65 milioni kwa ajili ya beki huyo wa pembeni wa England, 22. Tino ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Newcastle na alionyesha kiwango bora sana msimu uliopita akiwa na wababe hao. Kocha Eddie Howe hatamani kabisa kuona akiondoka kwa sababu yupo katika mipango yake kwa msimu ujao.
Marc Guehi
TOTTENHAM imepanga kuingia vitani na Chelsea kuhakikisha inaipata saini ya beki wa kati wa Crystal Palace, Marc Guehi, 25. Ripoti kutoka tovuti ya Star, zinadai Palace haipo tayari kumuuza staa huyu dirisha hili lakini inaweza kuamua kufanya hivyo ikiwa itapata ofa nono kutoka timu zinazohitaji saini yake. Guehi ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 anatamani sana kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Nicolas Jackson
MATUMAINI ya Manchester United kumsajili mshambuliaji wa Chelsea, Nicolas Jackson yameongezeka baada ya staa huyo, 24, kukataa ofa za AC Milan na Napoli kwa sababu bado anataka kubaki Ligi Kuu England msimu ujao. Jackson inadaiwa kutaka kuondoka Chelsea kwa sababu anataka kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza. Chelsea inadaiwa kuwa tayari kumuuza katika dirisha hili ikiwa itapata ofa sahihi.
Jadon Sancho
MABOSI wa Juventus wamepanga kuzidisha juhudi zao za kumsajili winga wa Manchester United , Jadon Sancho, 25, dirisha hili ikiwa watamuuza winga wao raia wa Ubelgiji, Samuel Mbangula, 21, na mshambuliaji wao wa kimataifa wa Marekani Timothy Weah, 25. Benchi la ufundi la Juventus linadawa haliridhishwi na viwango vya Mbangula na Weah na Sancho ndio chaguo lao.
Alejandro Garnacho
ASTON Villa, Chelsea na Tottenham zinamfuatilia winga wa Manchester United, Alejandro Garnacho, 21, ambaye inaaminika anaweza kupatikana kwa Pauni 40 milioni dirisha hili. Garnacho ni miongoni mwa wachezaji ambao kocha wa Man United, Ruben Amorim amewapa ruhusa ya kuondoka dirisha hili kwa sababu hayupo kwenye mipango yake.
Xavi Simons
Chelsea imejitosa katika harakati za kumsajili kiungo wa kati wa RB Leipzig, Xavi Simons,22, lakini huenda wakalazimika kuuza baadhi ya wachezaji. Simons anahusishwa na timu kadhaa za Ligi Kuu England lakini nyingi zimeshindwa kumsaili hadi sasa kutokana na kiasi kikubwa cha pesa ambacho Leipzig inakihitaji kama ada yake ya uhamisho.