Dili la Mbeumo, Man United yapewa siku mbili

Muktasari:
- Mazungumzo bado yanaendelea baina ya timu hizo lakini Brentford imeweka wazi kuwa hii ni wiki ya mwisho ya kujadiliana na Man United juu ya dili hilo na ikishindikana mchezaji atatakiwa kuwasili kambini Jumatatu wiki ijayo kwa maandalizi ya msimu mpya.
BRENTFORD imetoa siku mbili kwa Manchester United na imekataa kushusha bei ya mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon, Bryan Mbeumo kufikia walau pauni 63 milioni ambazo Man United ipo tayari kutoa.
Mazungumzo bado yanaendelea baina ya timu hizo lakini Brentford imeweka wazi kuwa hii ni wiki ya mwisho ya kujadiliana na Man United juu ya dili hilo na ikishindikana mchezaji atatakiwa kuwasili kambini Jumatatu wiki ijayo kwa maandalizi ya msimu mpya.
Man United ilishafanya makubaliano binafsi na Mbeumo muda mrefu na straika huyo ameshaiambia hadi Tottenham iliyokuwa ikimhitaji kuwa ameichagua Man United. Mabosi wa Man United wanajaribu kufanya mazungumzo ili kupunguziwa bei kwa sababu hawana bajeti kubwa
Anthony Elanga
NEWCASTLE United imeongeza ofa kufikia Pauni 55 milioni kwa ajili ya kuipata saini ya winga wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya Sweden, Anthony Elanga, 23, katika dirisha hili. Inaelezwa, Forest ipo tayari kumuuza kwa kiasi hicho tu cha pesa. Elanga ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Forest na kiwango alichoonyesha tangu msimu uliopita kimezivutia timu nyingi.
Marco Asensio
FENERBAHCE imetuma ofa ya Euro 15 milioni PSG kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo, Mhispania Marco Asensio katika dirisha hili. Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Asensio anataka kusubiri na kusikiliza ofa za timu zote zinazomtaka kabla hajafanya uamuzi wa timu atakayoichezea kwa msimu ujao. Huduma yake pia inahitajika AC Milan na Villarreal.
Malik Tillman
BAYER Leverkusen ipo katika hatua nzuri ya kumsajili kiungo wa PSV Eindhoven na timu ya taifa ya Marekani, Malik Tillman, 23, katika dirisha hili la usajili Ulaya kwa ada ya uhamisho ya Euro 35 milioni. Inaelezwa kwamba mabosi wa Leverkusen wanamwangalia mchezaji huyo kama mbadala sahihi wa Florian Wirtz ambaye wamemuuza kwenda Liverpool katika dirisha hili.
Rodrygo
KOCHA wa Real Madrid, Xabi Alonso amewaambia vigogo wa timu hiyo kuwa wanaweza kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Rodrygo, 24, ikiwa watapata ofa watakayoona ni nzuri. Inaelezwa Rodrygo ambaye anahusishwa na Arsenal hayupo katika mipango ya Alonso ambaye ameanza kulionyesha hilo mapema kuanzia kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu.
Gabriel Martinelli
AL-Nassr inafikiria kuhamishia nguvu kwa winga wa Arsenal na timu ya taifa ya Brazil, Gabriel Martinelli, 24, baada ya mchakato wa kuipata saini ya mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Colombia, Luis Diaz, 28, kuwa na ugumu. Licha ya kutoonyesha kiwango bora hivi karibuni haionekani kama itakuwa rahis kwa Arsenal kumwachia Martinelli.
Antonio Silva
BEKI kisiki wa Benfica, Antonio Silva, 21, ameripotiwa kukataa ofa nono kutoka Al-Hilal ya Saudi Arabia iliyotaka kumsajili katika dirisha hili kwani bado anatamani kuendelea kucheza soka la ushindani Ulaya. Licha ya kukataa ofa ya Al-Hilal taarifa zinaeleza hataendelea kusalia Benfica katika dirisha hili na badala yake atajiunga na moja ya timu za ligi tano Ulaya.
Denzel Dumfries
BEKI wa Inter Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Denzel Dumfries, 29, ana kipengele cha kuondoka cha Euro 21.5 milioni katika dirisha hili kitakachotamatika katikati ya mwezi huu. Dumfries ambaye ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Inter huduma yake inahitajika Barcelona na kipengele hicho kinaipa nguvu zaidi timu hiyo kumpata wakati utakapofika.