Cobham chimbo la pesa Chelsea
Muktasari:
- Katika misimu minne iliyopita, Chelsea imeingiza zaidi ya pauni milioni 300 kutokana na mauzo ya wachezaji waliotoka katika akademi yake ya Cobham.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA akademi imeendelea kuthibitisha ubora wake, si kwa kuzalisha wachezaji wanaofika kikosi cha kwanza pekee, pia kuipatia klabu mapato makubwa kupitia mauzo ya vijana wake.
Katika misimu minne iliyopita, Chelsea imeingiza zaidi ya pauni milioni 300 kutokana na mauzo ya wachezaji waliotoka katika akademi yake ya Cobham.
Chelsea FC imeendelea kutumia mfumo huo huku wachezaji kama Trevoh Chalobah na Tyrique George wakiwa miongoni mwa waliotangulia kuondoka Stamford Bridge baada ya muda mrefu ndani ya mfumo wa klabu hiyo.
Tangu kampuni ya BlueCo ichukue umiliki wa Chelsea kutoka kwa Roman Abramovich, biashara ya wachezaji imeongezeka kwa kasi, lakini kutumia akademi kama chanzo cha mapato si jambo jipya. Abramovich pia aliwahi kutumia mfumo huo, huku Chelsea ikiwanunua na baadaye kuwauza wachezaji kama Tammy Abraham na Fikayo Tomori kwa ada kubwa.
Kwa muda mrefu, Chelsea imekuwa na utamaduni wa wachezaji bora pekee wanaotoka Cobham ambao wanaweza kuwa na nafasi ya muda mrefu katika kikosi cha kwanza. Wengine huuzwa ili wakajenge taaluma zao katika klabu nyingine. Mfumo huo kwa kiasi kikubwa umekubalika na klabu pamoja na wachezaji.
Hata hivyo, Chelsea inapaswa kuwa makini. Akademi ni sehemu muhimu ya utambulisho wa klabu hiyo na mashabiki wake, hasa wakati ambapo baadhi yao wamekuwa wakilalamika kuwa klabu imepoteza uhusiano wake wa kihisia na mashabiki kutokana na matumizi makubwa ya fedha katika usajili.
Baadhi ya mashabiki wanahisi hawana uhusiano mkubwa na wachezaji wanaosajiliwa kwa fedha nyingi na kupewa jukumu la kuiwakilisha klabu uwanjani.
Wakati huohuo, wanakumbuka siku ambazo wachezaji waliotoka akademi walikuwa wakipewa nafasi na kung'ara katika kikosi cha kwanza, kama ilivyokuwa wakati Frank Lampard alipokuwa kocha.
Chalobah alikuwa mfano halisi wa mchezaji aliyekuwa na utambulisho wa Chelsea. Licha ya kupitia nyakati ngumu katika msimu uliopita na katika kipindi cha taaluma yake Stamford Bridge, alikuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa wakichukuliwa kuwa “Chelsea halisi”, kitu ambacho kina thamani kubwa katika soka la kisasa.
Alijiunga na Chelsea akiwa na umri wa miaka minane na kutumia jumla ya miaka 18 ndani ya klabu hiyo. Kutoka kuwa beki chipukizi aliyekuwa akipelekwa kwa mkopo mara kadhaa, Chalobah alifanikiwa kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza katika Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akitwaa pia taji la Ligi ya Mabingwa akiwa na Chelsea.
Hata hivyo, safari yake Stamford Bridge haikuwa rahisi kila wakati. Mwaka 2024 alitengwa na kikosi cha kwanza wakati Chelsea ikitafuta klabu ya kumnunua. Alinyang'anywa namba ya jezi na pia hakupelekwa katika ziara ya maandalizi ya msimu.
Baada ya kushindwa kupata uhamisho wa kudumu, Chelsea ilimpeleka kwa mkopo Crystal Palace. Alifanya vizuri katika Ligi Kuu kabla ya Chelsea kumrudisha kutokana na majeraha yaliyowakumba mabeki wa kikosi hicho.
Chalobah alipambana kurejea katika kikosi cha kwanza na hakulalamika, jambo lililoonyesha kiwango chake cha weledi.
Kwa sasa, Reece James na Levi Colwill ni miongoni mwa mifano ya wachezaji wanaowakilisha kizazi cha vipaji vinavyoendelea kuzalishwa Cobham.
Vijana kama Shim Mheuka, Mahdi Nicoll-Jazuli, Ryan Kavuma-McQueen, Tayo Suboloye na Jesse Derry nao wana matumaini ya kufanikiwa Chelsea, licha ya klabu kuendelea kutumia fedha nyingi kusajili vipaji vingine kutoka nje.
Hata hivyo, wao pamoja na mawakala wao wanatambua kwamba ni wachezaji wachache tu kati yao watakaofanikiwa kuwa wachezaji wa kudumu wa kikosi cha kwanza Stamford Bridge.