Chelsea yatua kwa Xavi Simons, Leipzig yakaza
Muktasari:
- Staa huyu mwenye umri wa miaka 22, kwa sasa anadaiwa kuwa katika mazungumzo ya maslahi binafsi na Chelsea kabla ya matajiri hao wa Jiji la London kujadiliana na Leipzig kuhusu ada ya uhamisho.
LICHA ya Chelsea kutaka kumsajili kiungo wa kimataifa wa Uholanzi, Xavi Simons, mabosi wa RB Leipzig wamemjumuisha staa huyo katika kikosi chao kitakachoingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Staa huyu mwenye umri wa miaka 22, kwa sasa anadaiwa kuwa katika mazungumzo ya maslahi binafsi na Chelsea kabla ya matajiri hao wa Jiji la London kujadiliana na Leipzig kuhusu ada ya uhamisho.
Katika dirisha hili Chelsea tayari imefanikisha usajili wa washambuliaji kadhaa ikiwa pamoja na Joao Pedro, Liam Delap, Estevao Willian, na Jamie Gittens lakini bado Simons yupo katika mipango yao.
Mabosi wa Chelsea bado wanahitaji kuongeza nguvu zaidi kwenye safu yao ya ushambuliaji hususani baada ya kuondoka kwa Noni Madueke.
Matajiri hawa wanaamini kumpata Simons sio jambo gumu sana kwani anasimamiwa na wakala wa aliyekuwa mchezaji wao, Madueke.
Katika msimu uliopita staa huyu alifunga mabao 11 na kutoa asisti nane kwenye mechi 33 za michuano yote na Chelsea inamhitaji sana kwa sababu mbali ya uwezo mkubwa wa kufunga alionao pia anaweza kutoa asisti.
Simons amekuwa akitajwa kwa muda mrefu kama moja ya wachezaji wenye vipaji vikubwa barani Ulaya tangu alivyoibuka katika akademi maarufu ya La Masia ya Barcelona, kabla ya kujiunga na Paris Saint-Germain na kisha RB Leipzig. Mkataba wake unamalizika mwaka 2027.
Jorrel Hato
CHELSEA imeingia katika vita dhidi ya Arsenal ili kuipata huduma ya beki wa kati wa Ajax na timu ya taifa ya Uholanzi, Jorrel Hato, mwenye umri wa miaka 19.
Inaelezwa baada ya wawakilishi wa Arsenal kusafiri mwanzoni mwa mwezi huu kwenda Uholanzi kwa ajili ya kufanya mazungumzo zaidi juu ya beki huyu, Chelsea nao wamefanya hivyo hivi karibuni kuhakikisha wanaipata huduma yake.
Benchi la ufundi la Arsenal linapambana kuboresha kikosi chao kuhakikisha wanafanya vizuri kwa msimu ujao. Hato ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Ajax.
Jacob Ramsey
NOTTINGHAM Forest bado inapambana kuhakikisha inaipata saini ya kiungo wa Aston Villa, Jacob Ramsey, mwenye umri wa miaka 24, katika dirisha hili.
Ramsey ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri katika msimu uliopita ambapo amecheza mechi 46 za michuano yote.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Forest inahitaji huduma ya fundi huyu wa kimataifa wa England kwa ajili ya kuboresha kikosi chao kuelekea michuano ya kimataifa msimu ujao.
Seth Ridgeon
FULHAM inaamini itaweza kumbakiza kiungo wake wa kati, Seth Ridgeon, katika dirisha hili licha ya Manchester United, Liverpool na Chelsea kuonyesha nia ya kumsajili.
Seth ambaye anaichezea timu ya taifa ya England kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, amekuwa akifuatiliwa na maskauti wa timu nyingi tangu msimu uliopita na zote zilivutiwa na kiwango ambacho amekuwa akikionyesha.
Mabosi wa Fulham wapo tayari kupambana na kumbakisha lakini ikiwa watapokea ofa nono hawatosita kumuuza.
Ederson
MABOSI wa Manchester City wamekataa ofa ya Galarasaray waliyoiwasilisha hivi karibuni ili kumpata kipa wao wa kimataifa wa Brazil, Ederson, 31, katika dirisha hili.
Ederson ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao anahitajika sana na Galatasaray ambayo iliwasilisha ofa ya Pauni 3 milioni hivi karibuni.
Inadaiwa Man City imekataa ofa hiyo kwa sababu ni ndogo na bado kocha Pep Guardiola anamhitaji kuelekea msimu ujao.
Facundo
BORUSSIA Dortmund imeonyesha nia ya kumsajili kiungo wa Brighton mwenye umri wa miaka 20, Facundo Buonanotte ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Leicester City.
Mkataba wake umebakisha miaka mitatu kabla ya kumalizika lakini ameshawaambia mabosi wa Brighton kwamba hataki kukosa nafasi hiyo ya kwenda Dortmund.
Mchezaji huyu wa kimataifa wa Argentina anadaiwa kuuzwa kwa kiasi kisichopungua Euro 30 milioni. Msimu uliopita alicheza mechi 35 za michuano yote. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Igor Paixao
MPANGO wa mabosi wa Marseille kutaka kumsajili winga wa Feyenoord, Igor Paixao unadaiwa kusimama baada ya ofa ya klabu hiyo ya Ufaransa kukataliwa.
Marseille iliwasilisha ofa Pauni 24 milioni kwa ajili ya staa huyu wa kimataifa wa Brazil na imekataliwa kwa sababu haifikii thamani ambayo Feynoord inaihitaji.
Kushindwa kwa Marseille kumeipa matumaini makubwa Leeds United ambayo inafanya mazungumzo na kwa ajili ya staa huyo mwenye umri wa miaka 25.
Hakan Calhanoglu
LICHA ya timu kibao kutaka kumsajili kiungo wa kati wa Inter Milan na timu ya taifa ya Uturuki, Hakan Calhanoglu, katika dirisha hili, staa huyo amegoma kuondoka na kusisitiza kwamba bado anahitaji kuendelea kupambania nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Inter. Staa huyu mwenye umri wa miaka 31, mkataba wake wa sasa unamalizika mwaka 2027.