Chelsea yaendelea kupambana kumnasa Alejandro Garnacho
Muktasari:
- Garnacho amekubali kutua Chelsea na kusaini mkataba wa miaka mitano. Man United inahitaji takribani Pauni 45 milioi ili kumuuza.
CHELSEA ambayo imefikia makubaliano binafsi na Alejandro Garnacho, imeongeza kasi ya mazungumzo na Manchester United kuhusu suala la ada ya uhamisho ya staa huyo aliyewaeleza wawakilishi wake hiyo ndiyo timu pekee anayotaka kujiunga nayo katika dirisha hili.
Garnacho amekubali kutua Chelsea na kusaini mkataba wa miaka mitano. Man United inahitaji takribani Pauni 45 milioi ili kumuuza.
Tovuti ya The Athletic iliripoti Juni kuwa Garnacho alikuwa miongoni mwa wachezaji watano wa United waliopata ruhusa ya kurudi mazoezini baada ya hapo awali kuripotiwa Kocha Ruben Amorim aliwaambia watafute klabu mpya.
Chelsea imezidisha juhudi zaidi kwa Garnacho baada ya kuona Man United imefikia makubaliano na RB Leipzig kwa uhamisho wa mshambuliaji Benjamin Sesko.
Chelsea imekuwa na nia ya muda mrefu kumsajili Garnacho kwa sababu kocha wao Enzo Maresca anaamini ataendana vizuri na mifumo yake pia umri ake unaendana na mpango wa klabu wao wa kuunda kikosi cha wachezaji wenye umri mdogo chenye ushindan.
Rodri
MANCHESTER City ina wasiwasi wa kumpoteza kiungo wao wa kimataifa wa Uhispania, Rodri, 29, dirisha hili kwani bado hajasaini mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2027. Hivi karibuni Real Madrid imeripotiwa kuwa katika harakati za kumuwinda Rodri ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo Man City. Msimu uliopita hakupata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza kutokana na majeraha.
Jack Grealish
EVERTON imefanya mazungumzo zaidi na Manchester City kuhusu uwezekano wa kumsajili kwa mkopo winga wa timu hiyo, Jack Grealish, mwenye wa umri wa miaka 29. Taarifa zinaeleza Man City inahitaji ada ya mkopo isiyopungua Pauni 12 milioni ili kumuuza staa huyo aliyesajiliwa na kwa ada iliyovunja rekodi ya Pauni 100 milioni mwaka 2021 akitokea Aston Villa. Mkataba wa Grealish na Man City unamalizika mwaka 2027.
Malick Thiaw
NEWCASTLE imefikia makubaliano na AC Milan kulipa Euro 40 milioni na kumsajili beki wa kimataifa wa klabu hiyo, Malick Thiaw, 24, dirisha hili. Milan imelazimika kumuuza staa huyu kutokana na uhitaji wake wa kutaka kuondoka ili kutafuta changamoto mpya pamoja na ofa ambayo Newcastle imeiweka mezani. Staa huyu amekuwa beki tegemeo Milan tangu mwaka 2022 alipotua akitokea Schalke 04 ya Ujerumani.
Marc Guehi
LIVERPOOL inatajwa kuwa kinara wa mbio za kumsajili beki wa Crystal Palace, England Marc Guehi, 25, katika dirisha hili. Guehi ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa akademi ya Chelsea, amekuwa akihusishwa kuondoka tangu kuanza dirisha hili na Palace ipo tayari kumwachia lakini changamoto imekuwa ni kiasi cha pesa inachohitaji kuwa kikubwa. Msimu uliopita alicheza mechi 44 za michuano yote.
Xavi Simons
CHELSEA bado inaendelea kufanya mazungumzo na RB Leipzig, ili kumsajili kiungo wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Uholanzi, Xavi Simons, 22, dirisha hili. Simons, aliyewahi kucheza PSG na PSV, amelivutia sana benchi la ufundi la Chelsea kutokana na kiwango chake alichoonyesha msimu uliopita. Mkataba wa Simons unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu uliopita alicheza mechi 33 za michuano yote na kifunga mabao 11.
Kingsley Coman
AL Nassr ya Saudi Arabia imepanga kutoa ofa ya takribani Euro 30 milioni Bayern Munich ili kumsajili winga wao, Kingsley Coman, 29, dirisha hili. Coman ambaye mwenyewe inadaiwa kutamani sana kutimkia Saudi Arabia kutokana na ofa nono ambayo imewekwa mezani, mkataba wake unamalizika mwaka 2027.
Giovanni Leoni
AC Milan imeingia katika vita dhidi ya Inter Milan na Liverpool ili kuipata huduma ya beki chipukizi wa Italia, anayeichezea Parma , Giovanni Leoni, 18, dirisha hili. Parma imeonyesha nia ya kumuuza lakini wawakilishi wa beki huyu hawana haraka kwani wanataka Leoni ajiunge na timu itakayompa nafasi ya kucheza kwa ajili ya maendeleo ya kipaji chake na pesa sio chaguo lao.