Mwisho wa mechi 831 za Anthony Taylor
Muktasari:
- Taylor (47), ambaye alikuwa miongoni mwa waamuzi wawili waliowakilisha England katika fainali hizo pamoja na Michael Oliver, amefika mwisho wa safari yake baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miaka 16 katika kiwango cha juu cha soka.
LONDON, ENGLAND: MWAMUZI mashuhuri wa Ligi Kuu England (Premier League), Anthony Taylor, ametangaza kustaafu rasmi kazi ya uamuzi, siku chache baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia 2026.
Taylor (47), ambaye alikuwa miongoni mwa waamuzi wawili waliowakilisha England katika fainali hizo pamoja na Michael Oliver, amefika mwisho wa safari yake baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miaka 16 katika kiwango cha juu cha soka.
Mchezo wake wa mwisho ulikuwa hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia 2026 kati ya Hispania na Ureno mechi iliyochezwa jijini Dallas, Marekani. Katika pambano hilo, Hispania iliibuka na ushindi wa mabao 1-0 baada ya Mikel Merino kufunga bao la dakika za mwisho na kuipeleka timu yake robo fainali.
Katika kipindi chote cha kazi yake, Taylor amechezesha jumla ya mechi 831, zikiwemo 668 nchini England na 432 za Ligi Kuu England. Pia alisimamia fainali zote kubwa za ndani, ikiwemo FA Cup za mwaka 2017 na 2020.
Kimataifa, Taylor alihudumu kwa miaka 14 akiwa mwamuzi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), akichezesha Kombe la Dunia la 2022 na 2026, pamoja na michuano ya Euro 2020 na Euro 2024.
Licha ya kutajwa katika orodha ya waamuzi waliokuwa wakifikiriwa kuchezesha fainali ya Kombe la Dunia 2022, Taylor aliondolewa kutokana na historia ya kisiasa kati ya England na Argentina kuhusu visiwa vya Falklands.
Akizungumzia uamuzi wake wa kustaafu, Taylor alisema kufikia kiwango cha juu kabisa cha uamuzi imekuwa heshima kubwa kwake, lakini alikiri presha na uchunguzi wa karibu kwa waamuzi wa kiwango hicho ni mkubwa.
“Kuchezesha katika kiwango cha juu imekuwa heshima ya kipekee, lakini presha na uchunguzi wa kila wakati ni mkubwa. Nimeona huu ndio wakati sahihi wa kuhitimisha safari hii na kuanza ukurasa mpya wa maisha yangu,” alisema Taylor.
Aliwashukuru wasaidizi wake Gary na Adam, waamuzi wenzake, pamoja na familia na marafiki kwa sapoti waliompa katika kipindi chote cha kazi yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Waamuzi wa Professional Game Match Officials Limited (PGMOL), Howard Webb, alimpongeza Taylor kwa mchango wake mkubwa katika soka la England na dunia.
“Anthony amekuwa mtumishi bora wa mchezo huu kwa miaka mingi. Ameaminiwa kuchezesha mechi kubwa zaidi duniani na amekuwa mfano wa kuigwa kutokana na weledi wake na namna alivyowalea waamuzi chipukizi,” alisema Webb.
Katika maisha yake ya uamuzi, Taylor aliwahi kuwa sehemu ya matukio yaliyotikisa soka la England, likiwemo ugomvi maarufu kati ya makocha Antonio Conte na Thomas Tuchel baada ya mchezo wa Chelsea dhidi ya Tottenham mwaka 2022.
Barani Ulaya, pia alijikuta katikati ya mjadala mkubwa baada ya aliyekuwa kocha wa AS Roma, Jose Mourinho, kumsubiri katika eneo la maegesho ya wageni maalumu (VIP) baada ya fainali ya Europa Ligi 2023 dhidi ya Sevilla.
Mourinho alimshambulia kwa maneno makali, akimuita “aibu” na kuhoji maamuzi yake katika mchezo huo, jambo lililosababisha baadaye kuchukuliwa hatua na UEFA kwa matumizi ya lugha ya kumdhalilisha mwamuzi.
Kabla ya kuwa mmoja wa waamuzi bora barani Ulaya, Taylor aliwahi kuwa mwamuzi msaidizi katika Super Cup ya UEFA 2014, fainali ya Europa League 2015, pamoja na fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya 2016 na Euro 2016.
Kwa kustaafu kwake, soka la England linaaga mmoja wa waamuzi walioacha alama kubwa ndani na nje ya uwanja. kwa sasa bado haiajafahamika atakwenda wapi lakini inaelezwa kuwa anaweza kujiunga na timu cha televisheni.