Chelsea wamalizana na kipa Martinez
Muktasari:
- Usajili huo unakuja baada ya Chelsea kuanza kuwa na wasiwasi kuhusu kiwango cha kipa wake Robert Sanchez, huku Aston Villa ikiwa tayari kumuachia Martinez baada ya kumsajili kipa wa Japan, Zion Suzuki, kutoka Parma kwa takriban Pauni 30 milioni.
Chelsea imekubaliana na Aston Villa kumsajili kipa wa Argentina, Emiliano Martinez, kwa ada ya Pauni 7.5 milioni (takriban Sh27 bilioni), huku kipa huyo, 33, akitarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya jijini London.
Usajili huo unakuja baada ya Chelsea kuanza kuwa na wasiwasi kuhusu kiwango cha kipa wake Robert Sanchez, huku Aston Villa ikiwa tayari kumuachia Martinez baada ya kumsajili kipa wa Japan, Zion Suzuki, kutoka Parma kwa takriban Pauni 30 milioni.
Kuwasili kwa Martinez ni mabadiliko makubwa katika mipango ya Chelsea, ambayo awali ilitarajiwa kuendelea kumtumia Sanchez kama kipa wake namba moja.
Hata hivyo, Martinez sasa anatarajiwa kuleta ushindani katika nafasi hiyo na huenda akampoka Sanchez nafasi ya kuanza.
Uamuzi wa Chelsea umechochewa zaidi na makosa ya Sanchez katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Fulham na alikosolewa baada ya kushindwa kuuzuia vizuri mpira uliopigwa na Josh King na kuacha upenyeze.
Chelsea imeamua kuchukua hatua licha ya Sanchez kuwa sehemu ya mipango ya timu, huku ikivutiwa pia na gharama ndogo ya kumsajili Martinez, ambaye atawasili kwa Pauni 7.5 milioni pekee.
Kwa upande wa Aston Villa, usajili wa Suzuki kwa karibu Pauni 30 milioni mapema mwezi huu umefungua mlango wa kumuachia Martinez.
Martinez anaondoka Villa akiwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa klabu hiyo tangu alipojiunga akitokea Arsenal mwaka 2020.
Ameichezea Villa mechi 256, akisaidia klabu hiyo kutwaa Ligi ya Europa mwezi Mei na pia kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Amad Diallo
Aston Villa imewasilisha ofa rasmi ya kumsajili winga wa Manchester United, Amad Diallo, kwa mujibu wa ripoti. Thamani ya ofa hiyo haijawekwa wazi na bado haijajulikana kama United imekubali au kuikataa. Amad mwenye miaka 24 ana mkataba na United hadi 2030, huku klabu ikiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Omari Hutchinson
AC Milan imeripotiwa kufikia makubaliano na Nottingham Forest kuhusu kumsajili winga Omari Hutchinson, ambaye hakuwamo kwenye kikosi cha Forest kilichotoka sare ya mabao 2-2 na Liverpool. Hutchinson anatarajiwa kujiunga na Milan kwa mkopo hadi mwisho wa msimu, huku klabu hiyo ikiwa na sharti la kumnunua moja kwa moja baadaye.
Daniel Munoz
Nottingham Forest imefikia makubaliano na Crystal Palace kuhusu kumsajili beki Daniel Munoz, ambaye atarejea kufanya kazi chini ya kocha Oliver Glasner katika Uwanja wa City Ground. Forest pia inahitaji kuongeza kipa na imewasilisha ofa kwa Dean Henderson. Hata hivyo, Palace inatarajiwa kuikataa, ingawa thamani ya ofa hiyo haijawekwa wazi hadi sasa pia.
Alexander Sorloth
Manchester United imepewa nafasi ya kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid, Alexander Sorloth, ambaye yupo tayari kuondoka. Atletico iko tayari kumuuza iwapo itapata mshambuliaji wa kuchukua nafasi yake. Sorloth, 30, ana uzoefu England akiwa Crystal Palace na amefunga mabao 32 katika mechi 67 akiwa Atletico Madrid Hispania.
Karl Etta Eyong
Sunderland imeingia kwenye kinyang’anyiro cha kumsajili mshambuliaji wa Levante, Karl Etta Eyong dirisha hili la usajili kwa ada iliyo chini ya Pauni 26 milioni. Kiasi hicho ndicho kilichowekwa kwenye mkataba wake kama kiwango cha kuvunja mkataba. Mazungumzo yanaendelea huku Sunderland ikitafuta kuimarisha safu yake ya ushambuliaji.
Pape Matar Sarr
Juventus imeanza mazungumzo na Tottenham Hotspur kuhusu kumsajili kwa mkopo kiungo wa Senegal, Pape Matar Sarr, ikiwa na uwezekano wa kumnunua moja kwa moja, kwa mujibu wa Nico Schira. Endapo uhamisho huo utakamilika, Sarr mwenye miaka 23 anaweza kusaini mkataba hadi mwaka 2031. Juventus pia inafuatilia uwezekano huo kwa karibu sasa.
Sofyan Amrabat
Kiungo wa Morocco, Sofyan Amrabat, amejiunga na Ajax kwa uhamisho wa bure baada ya Fenerbahce kuvunja mkataba wake. Mchezaji huyo, 30 amesaini mkataba wa miaka miwili na kupewa jezi namba nne. Amrabat alilelewa Utrecht, kisha akachezea Feyenoord, Fiorentina, Manchester United na Fenerbahce kabla ya kurejea Uholanzi.
Jonathan David
Atletico Madrid imeanza mazungumzo na wawakilishi wa mshambuliaji wa Juventus, Jonathan David, kuhusu uwezekano wa kumsajili siku za mwisho za usajili. Mazungumzo yanaendelea na Juventus, huku Atletico ikichunguza gharama na masharti ya uhamisho huo. David ni miongoni mwa washambuliaji watatu wanaolengwa na Diego Simeone.
Matteo Bahoya
Hull City inaendelea na mazungumzo na Eintracht Frankfurt kuhusu kumsajili winga Jean-Matteo Bahoya siku za mwisho za usajili, kwa mujibu wa Florian Plettenberg. Hadi sasa hakuna makubaliano wala ofa rasmi iliyowasilishwa, huku pande hizo zikijadili thamani ya uhamisho huo kupitia mazungumzo ya mdomo kabla ya hatua kuchukuliwa.