CAF kuzichunguza Morocco, DR Congo kisa vurugu
SHIRIKISHO la Soka Afrika (Caf) limeanzisha uchunguzi kuhusu vurugu zilizotokea baada ya mchezo kati ya Morocco dhidi ya DR Congo.
Caf inazichunguza Shirikisho la Soka Morocco FRMF na lile la Congo Fecofa kutokana na tukio hilo la baada ya mchezo ambalo maofisa wa timu ya Morocco na DR Congo walikunjana na kusukumana katika vurugu hizo na zilianza kwa kocha wa Morocco na Walid Regragui na beki wa DR Congo, Chancel Mbemba.
Video zilionyesha watu kutoka kambi zote mbili wakitoleana maneno na kusukumana baada ya mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya 1-1 huku majibizano ya awali yakianzia kwa Regragui na Mbemba.
Wachezaji na maofisa walirekodiwa wakikimbilia kwenye vyumba vya kuvalia, huku aliyerekodi video hiyo akidai polisi zaidi waliitwa uwanjani hapo.
Mwandishi wa habari mmoja aliyerekodi video hiyo alidai Regragui alimfuata Mbemba wakati beki huyo akiwa amepiga magoti akisali na kusababisha wawili hao kujibizana.
Njia ya kwenda kwenye vyumba vya kuvalia haikuwa salama kwani wachezaji waliendelea kuvutana huku wakikimbizana.
Akaunti moja ya X yenye wafuasi wengi inadai akaunti rasmi ya Fainali za Mataifa ya Afrika, imedai Regragui anachunguzwa na Shirikisho la Soka la Afrika kwa kumfanyia vitendo vya kibaguzi Mbemba.
Aidha, akaunti hiyo imedai baada ya kuisoma mienendo ya mdomo wa Regragui imebaini alikuwa anamwambia: "Hebu niangalie mimi wakati unapeana mikono nami."
Hata hivyo, haijathibitika kama akaunti hiyo ni rasmi kwa ajili ya michuano hiyo ya Afcon 2023.
Awali Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) halikueleza kama kuna uchunguzi unaofanyika na sasa inayachunguza mashirikisho ya soka ya nchi hizo.
Baada ya mechi, Mbemba, ambaye ni beki wa zamani wa Newcastle, alipokea maoni yaliyojaa chuki na ubaguzi katika moja ya akaunti zake za Instagram.
Alisema baada ya tukio hilo: "Namheshimu kocha ambaye ni mtu poa. TV zimekata vipande vya video, lakini ninazo. Sihitaji kuzirusha. Nitabaki kimya, ukimya ni jambo bora, na hivyo ndivyo nilivyo. Kila mmoja ananifahamu, namheshimu kila mmoja, sihitaji kumshuti yeyote lakini haki ya Mungu itabaki pale pale."
Regragui aliliambia gazeti la L'Equipe: "Nilimwambia Desabre (kocha wa DR Congo): "Mleteni tena kwangu, anajitia wazimu, anaongea ujinga tu. Sijalipenda jambo hilo kwa sababu limesababisha mambo mengi.
"Hivyo kama ana picha tofauti na kile tulichokiona kwenye televisheni, mwacheni azionyeshe, kwa raha zake. Na atakiona kitakachotokea. Na hicho ndicho kilichotokea... Kabla sijaenda kumpa mkono, alitukera mimi na wasaidizi wangu pembeni ya uwanjani kabla mechi haijamalizika, alitutolea maneno ya ovyo. Na Desabre anajua kuhusu hili.
Mwisho, licha ya kutufanyia yote hayo, nilienda kumpa mkono na kumwambia, "Kwa nini ulitutolea maneno machafu vile?" Na kisha akaangalia pembeni, kwamba "sitaki kukupa mkono". Nikamshika mkono wake, unaweza kuona katika picha, na akaanza kupiga makelele mahali pote pale.
"Nikasema, "Unajitukana mwenyewe!" Na akasema, "Umeniita mimi mpumbavu!" Ni sawa kama amesikia nikisema hivyo, inagawa sikusema hivyo, lakini kwa namna alivyokuwa akisema alikuwa akimaanisha kwamba maneno yangu ni ya kibaguzi, hii sio sawa kabisa. Kwa kuwa anaonekana anataja mambo ya dini katika kauli zake, basi azungumze ukweli."
Matokeo hayo yameiacha Morocco kileleni mwa kundi lao ikiwa na pointi nne baada ya mechi mbili, huku DR Congo ikiwa katika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi mbili.
Achraf Hakimi aliifungia Morocco bao la kuongoza ndani ya dakika sita lakini DR Congo ikasawazisha katika dakika ya 76 kupitia kwa Silas.