Bruno Guimaraes hataki kwenda popote
Muktasari:
- Katika mkataba huo mpya, Guimaraes pia hana mpango wa kuomba mshahara mkubwa sana ambao unaweza kusababisha makubaliano yasifikiwe.
INAELEZWA kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes, 28, hafikirii hata kidogo kuondoka katika klabu hiyo kwa sasa na yupo tayari kuanza mazungumzo ya kusaini mkataba mpya utakaomwezesha kusalia katika viunga hivyo kwa muda mrefu zaidi.
Katika mkataba huo mpya, Guimaraes pia hana mpango wa kuomba mshahara mkubwa sana ambao unaweza kusababisha makubaliano yasifikiwe.
Hivi karibuni kumekuwa na tetesi kwamba Guimaraes ambaye kwa sasa ni kapteni wa Newcastle anaweza akasajiliwa na Man United inayotafuta mbadala wa Casemiro anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu.
Kutoonyesha shauku ya kutaka kuondoka kwa Guimaraes inaweza kuwa pigo kubwa kwa Man United ambayo hadi sasa bado haijapata hasa mchezaji anayeweza kuziba pengo la Casemiro licha yakuwa na orodha kubwa ya wachezaji inaohitaji kuwasajili. Mkataba wa nyota huyo unatarajiwa kumalizika 2028 na awali ilielezwa kwamba, ikiwa Newcastle ingetaka kumuuza, ingehitaji takribani Pauni 100 milioni kama ada yake ya uhamisho.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Bruno amecheza mechi 35 za michuano yote.
Wesley Franca
ARSENAL imezidisha juhudi katika harakati zao za kutafuta beki wa kulia na inadaiwa staa wa AS Roma na timu ya taifa ya Brazil, Wesley Franca mwenye umri wa miaka 22, ni miongoni mwa wachezaji inaotaka kuwasajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Fofana ambaye kwa sasa ni mmoja kati ya mastaa tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Roma, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2030. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 25 za michuano yote na kufunga mabao manne.
Eduardo Camavinga
LIVERPOOL inaripotiwa kuwa ndio inaongoza katika mbio za kuiwaniansaini ya kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Eduardo Camavinga mwenye umri wa miaka 22. Kwa mujibu wa tovuti ya Caught Offside, mabosi wa Liverpool wamekutana na wawakilishi wa Camavinga mara mbili na hadi kufikia sasa mazungumzo yapo katika hatua nzuri. Licha ya kuonyesha nia ya kumsajmili, mabosi wa Madrid hawaonekani kuwa tayari kumwachia kiungo huyo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029.
Marcus Rashford
BAADA ya ripoti zilizodai kwamba Manchester United imegoma kumtoa tena kwa mkopo Marcus Rashford kwenda Barcelona ifikapo msimu ujao baada ya mkataba wa sasa wa mkopo kumalizika, kocha wa wababe hao kutoka viunga vya Nou Camp, Hansi Flick ameweka wazi kwamba hadi sasa hata yeye hajui nini kitatokea kwa Rashford.
Barca ina kipengele kinachowapa nafasi ya kumsajili mazima Rashford kwa Pauni 26 milioni, lakini kiasi hicho cha pesa kinaonekana kuwa kikubwa kwao, hivyo imekuwa ikiomba ipunguziwe lakini Man United imegoma na ikaomba ipewe tena staa huyo kwa mkopo msimu ujao bado mashetani wekundu wakagoma.
Raphinha
WINGA wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Raphinha mwenye umri wa miaka 29, amesisitiza kuwa hana mpango wa kuondoka katika viunga hivyo vya Nou Camp katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya tetesi zinazodai kuwa huenda akatimkia Saudi Arabia baada ya kumalizika kwa msimu huu. Raphinha ni miongoni mwa mastaa kadhaa wenye majina makubwa barani Ulaya wanaowindwa sana na matajiri wa Saudia ambao wapo tayari kutoa ofa nono kuhakikisha wanavunja mikataba yao.
Erling Haaland
LICHA ya ripoti zinazodai kwamba Barcelona na Real Madrid zinatamani kumsajili straika wa Manchester City, Erling Haaland, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, tovuti ya Football Insider, imeweka wazi kwamba Man City haina mpango wa kumwachia staa huyo hata yeye mwenyewe akiwa tayari kuondoka. Mabosi wa juu wa Man City wanaamini Haaland ni hazina yao na taswira ya timu, hivyo wanataka kufanya kila linalowezekana kuhakikisha anaendelea kuvaa jezi yao na kuwatumikia.
Antonio Rudiger
JUVENTUS inaangalia uwezekano wa kumsajili beki kisiki wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ujerumani, Antonio Rudiger mwenye umri wa miaka 33. Mkataba wa sasa wa beki huyu unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa bado hajafikia makubaliano yoyote na Man United juu ya mkataba mpya. Hali hiyo imeanza kuivuta Juventus ambayo inaamini inaweza kumpata bure kabisa ikiwa mambo yataendelea kuwa hivi yanavyoendelea kati ya beki huyo na Madrid.
Ederson
ATLETICO Madrid imetuma ofa ya Pauni 30 milioni pamoja na nyongeza ya Pauni 4 milioni kwenda Atalanta kwa ajili ya kumsajili kiungo wa klabu hiyo, Ederson, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Ederson ambaye amekuwa akiwindwa na vigogo kadhaa Ulaya tangu mwaka jana, anatamani sana kuondoka Atalanta na kutua timu itakayokuwa na ushindani zaidi uwezo wa kushinda mataji makubwa pamoja na kumpa mshahara mnono tofauti na ule anaupokea kwa sasa.