Bifu la Trump, Lebron limenoga
Muktasari:
- LeBron James, mwenye umri wa miaka 41, alitangaza kupitia taarifa ndefu kwamba alifikiria kwa uzito kustaafu mchezo wa mpira wa kikapu baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, lakini akaamua kuendelea kwa sababu anaamini bado ana uwezo mkubwa wa kuchangia ndani ya uwanja.
LOS ANGELES, MAREKANI: RAIS wa Marekani, Donald Trump, ameibua mjadala mkubwa baada ya kumshambulia nyota wa NBA, LeBron James, kwa kumuita " mbaguzi," saa chache tu baada ya mkongwe huyo kuthibitisha kuwa ataendelea kucheza msimu mwingine kwa kujiunga na Philadelphia 76ers.
LeBron James, mwenye umri wa miaka 41, alitangaza kupitia taarifa ndefu kwamba alifikiria kwa uzito kustaafu mchezo wa mpira wa kikapu baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, lakini akaamua kuendelea kwa sababu anaamini bado ana uwezo mkubwa wa kuchangia ndani ya uwanja.
Kwa mujibu wa ESPN, James anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya dola 8 milioni na Philadelphia 76ers, tofauti kubwa na karibu dola 53 milioni alizolipwa msimu uliopita akiwa Los Angeles Lakers.
Baada ya kuthibitishwa kuwa James ataanza msimu wake wa 24 katika NBA, Trump aliulizwa maoni yake kuhusu nani ndiye mchezaji bora zaidi wa mpira wa kikapu kuwahi kutokea.
Trump hakusita kumtaja Michael Jordan.
"Michael Jordan ni rafiki yangu. Tumewahi kucheza gofu pamoja. Ni mtu mzuri sana," amesema Trump.
Kisha akaongeza kauli iliyozua gumzo kubwa:
"Nafikiri LeBron... huenda ni mbaguzi, au labda hampendi Trump, sijui. Mimi napenda watu wanaonipenda, kwa hiyo kwangu Michael Jordan ndiye bora kabisa."
Kauli hiyo imeongeza sura mpya katika uhasama wa muda mrefu kati ya Trump na LeBron James, ambao ulianza mwaka 2017 baada ya James kumuita Trump "bum" (mtu asiye na maana) kupitia mtandao wa kijamii.
UHASAMA WA MIAKA MINGI
LeBron amekuwa mmoja wa wanamichezo waliotumia umaarufu wao kuzikosoa hadharani siasa za Trump.
Ameunga mkono wagombea wa Chama cha Democratic katika uchaguzi mbalimbali nchini Marekani na pia ameanzisha kampeni za kuhamasisha wananchi kupiga kura.
Mwaka 2017, mgogoro wao ulianza wazi baada ya Trump kufuta mwaliko wa Ikulu kwa Golden State Warriors kufuatia Stephen Curry kusita kuhudhuria sherehe hiyo.
LeBron alimkingia kifua Curry na kumjibu Trump kupitia X (zamani Twitter):
"Wewe ni bum. Steph Curry tayari amesema haendi, hivyo hakuna mwaliko wowote. Kwenda White House ilikuwa heshima kubwa hadi ulipoingia madarakani."
Mwaka uliofuata, Trump alitangaza kuwa Cleveland Cavaliers na Golden State Warriors hawangealikwa Ikulu baada ya Fainali za NBA.
LeBron hakuyumba na kujibu:
"Kushinda ubingwa ni jambo kubwa zaidi kuliko kualikwa White House, hasa ikiwa yeye ndiye yuko humo."
Baadaye mwaka huo, James aliiambia ESPN kuwa alikuwa akihuzunishwa na namna Trump alivyoiongoza Marekani.
"Haelewi nguvu aliyonayo kama kiongozi wa taifa hili. Haelewi jinsi watoto wa kila rangi wanavyomtazama Rais wa Marekani kama mfano wa uongozi na matumaini. Hilo ndilo linaloniumiza zaidi kuliko kitu kingine."
ALIMUUNGA MKONO HILLARY CLINTON
Upinzani wa kisiasa wa LeBron dhidi ya Trump ulianza hata kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016.
Katika makala aliyoiandika kwenye gazeti la nyumbani kwao, Akron Beacon Journal, James alimtangaza wazi Hillary Clinton kuwa chaguo lake la urais.
Akizungumzia maisha yake ya kukulia katika familia ya mzazi mmoja, amesema Clinton ndiye aliyekuwa anaelewa changamoto za watoto wanaotoka katika mazingira magumu na akamsifu pamoja na aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama, kwa kupigania maslahi ya watoto.
SAFARI MPYA PHILADELPHIA
Mbali na mjadala wa kisiasa, LeBron sasa anaelekeza nguvu zake kwenye changamoto mpya akiwa Philadelphia 76ers.
Kupitia ujumbe mrefu aliouchapisha kwenye X, alieleza kuwa alifikiri msimu uliopita ulikuwa wa mwisho kwake.
"Nilidhani nimekwisha baada ya msimu kuisha. Sikuwa tayari kutangaza hilo kwa sababu nilihitaji muda wa kutafakari. Nilikuwa karibu kabisa kuamini kuwa nilikuwa nimecheza mchezo wangu wa mwisho."
Aliendelea kusema:
"Bado ninaipenda sana mchezo huu na bado nina mengi ya kutoa. Wiki chache zilizopita zimekuwa za kipekee kwangu. Nilipata muda wa kutafakari maisha na mustakabali wangu pamoja na watu ninaowapenda."
James amesisitiza kuwa uamuzi wake haujachochewa na fedha wala sababu za kifamilia.
"Huu ndio uamuzi wangu wa mwisho. Sichezi kwa ajili ya pesa. Sichezi kwa ajili ya familia. Ninacheza kwa sababu bado nataka kujitoa, kufanya kazi kwa bidii, kushindana na kupata nafasi ya kushinda ubingwa mwingine."
Nyota huyo anaamini anaweza kuifanya Philadelphia 76ers kuwa timu ya ubingwa.
"Ninaamini ninaweza kusaidia kuifanya Philadelphia 76ers kuwa bingwa na ninafurahia sana kuanza safari hii mpya pamoja na mashabiki wapya. Asante Los Angeles. Miami nitawapenda milele, na Northeast Ohio daima itakuwa nyumbani."
ALIAGA LAKERS
Ripoti zinaeleza kuwa mapema kipindi hiki cha kiangazi LeBron aliwaarifu Los Angeles Lakers kuwa hangerudi kwa msimu ujao.
Kabla ya kufanya uamuzi huo, alihusishwa na uwezekano wa kurejea Cleveland Cavaliers, Miami Heat pamoja na kujiunga na Golden State Warriors.
Hata hivyo, Philadelphia 76ers ndiyo imefanikiwa kupata saini yake baada ya juhudi kubwa zilizofanywa na viongozi wa klabu pamoja na nyota wao Tyrese Maxey.
The Athletic iliripoti kuwa Maxey na viongozi wengine wa Philadelphia walifanya kila juhudi kumshawishi LeBron kujiunga nao, huku usajili mkubwa wa Jaylen Brown ukiongeza mvuto wa kikosi hicho.
CHANGAMOTO MPYA
LeBron anaungana na kikosi kinachowajumuisha Joel Embiid, Jaylen Brown na Tyrese Maxey katika harakati za kutafuta ubingwa wa tano wa NBA katika maisha yake.
Philadelphia 76ers haijatwaa ubingwa wa NBA tangu mwaka 1983 na haijafanikiwa kuvuka hatua ya pili ya mchujo wa Kanda ya Mashariki tangu mwaka 2001.
Mashabiki wa timu hiyo wana matumaini kuwa LeBron ataivunja laana hiyo kama alivyofanya Cleveland Cavaliers mwaka 2016, alipoiwezesha kushinda ubingwa wa kwanza baada ya kusubiri kwa miaka 52.
LeBron, ambaye atatimiza miaka 42 mwezi Desemba, anajiandaa kuanza msimu wake wa 24 katika NBA, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na mchezaji mwingine.
Pia ndiye kinara wa muda wote wa wafungaji katika historia ya NBA, akiwa ametwaa mataji manne ya ubingwa: mawili akiwa Miami Heat, moja Cleveland Cavaliers na moja Los Angeles Lakers.