LeBron akienda Warriors, NBA inabadili ratiba
Muktasari:
- Wakala wa LeBron, Rich Paul, amesema timu yenye LeBron na Curry ingeifanya NBA kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya mechi zitakazoonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni za kitaifa kutokana na hamasa kubwa ya mashabiki.
NEW YORK, MAREKANI: LIGI ya NBA inaweza kulazimika kufanya mabadiliko makubwa kwenye ratiba ya msimu ujao iwapo nyota mkongwe LeBron James ataamua kujiunga na Golden State Warriors, huku mvuto wa kushirikiana kwake na Stephen Curry ukitajwa kuwa mkubwa kuliko kawaida.
Wakala wa LeBron, Rich Paul, amesema timu yenye LeBron na Curry ingeifanya NBA kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya mechi zitakazoonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni za kitaifa kutokana na hamasa kubwa ya mashabiki.
Akizungumza kwenye podikasti ya Game Over, Paul amesema kwa utani kuwa Warriors wangestahili kupewa karibu mechi 60 za matangazo ya kitaifa, ingawa anaamini hata kama haitakuwa hivyo, angalau zaidi ya nusu ya ratiba yao itaonyeshwa.
"NBA italazimika kuwapa mechi 60 za kitaifa. Natania kidogo, lakini naamini watapata angalau nusu ya mechi zao zikirushwa moja kwa moja," amesema Paul.
Alifananisha mvuto wa timu hiyo na enzi ambazo Warriors walikuwa na Stephen Curry, Klay Thompson na Draymond Green, huku upande mwingine ukiwa Cleveland Cavaliers ya LeBron James, Kyrie Irving na Kevin Love, ambazo zilivutia watazamaji wengi duniani.
Kauli hiyo imekuja wakati Kamishna wa NBA, Adam Silver, akimhimiza LeBron kufanya uamuzi wake haraka ili ligi ikamilishe ratiba ya msimu wa 2026/27.
Silver amesema mahali ambapo LeBron atacheza msimu ujao kutakuwa na athari kubwa katika upangaji wa mechi za ufunguzi wa msimu, siku ya Krismasi na michezo mingine mikubwa inayovutia watazamaji.
"Tunahitaji kukamilisha ratiba na timu ambayo LeBron atachezea itaathiri namna tutakavyopanga mechi za ufunguzi, Krismasi na nyingine muhimu. Tunahitaji afanye uamuzi," amesema Silver.
Ratiba kamili ya msimu mpya wa NBA kwa kawaida hutangazwa katikati ya Agosti, huku mechi za ufunguzi na za Krismasi zikitangazwa mapema.
Hadi sasa, LeBron bado hajatangaza uamuzi wake tangu aondoke Los Angeles Lakers, licha ya kuhusishwa na klabu kadhaa zikiwemo Golden State Warriors, Cleveland Cavaliers, Miami Heat, Philadelphia 76ers na Minnesota Timberwolves.
Nyota huyo mwenye miaka 41 alikataa kuweka wazi hatma yake alipoulizwa kwenye kipindi cha moja kwa moja cha Mind the Game wakati wa tamasha la Fanatics Fest, jambo lililoendelea kuongeza msisimko kuhusu hatua yake inayofuata.
Iwapo ataungana na Curry Warriors, uhamisho huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni ya NBA na unaweza kubadili kabisa mvuto wa msimu ujao wa ligi hiyo.