Bayern Munich yamtaka Ibrahima Konate fasta
Muktasari:
- Beki huyo alihusishwa sana na mpango wa kuhamia Real Madrid dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kabla ya miamba hiyo ya Hispania kuvamia Liverpool na kunasa huduma ya beki wa kulia Trent Alexander-Arnold kwa uhamisho wa bure.
MUNICH, UJERUMANI: BAYERN Munich imeingia kwenye mbio za kumfukuzia beki wa kati wa Liverpool, Ibrahima Konate baada ya kutambua Mfaransa huyo atapatikana bure sokoni mwishoni mwa msimu huu.
Beki huyo alihusishwa sana na mpango wa kuhamia Real Madrid dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kabla ya miamba hiyo ya Hispania kuvamia Liverpool na kunasa huduma ya beki wa kulia Trent Alexander-Arnold kwa uhamisho wa bure.
Kylian Mbappe ni mchezaji mwingine aliyesajiliwa na Los Blancos kwa uhamisho wa bure na ilikuwa imemweka kwenye mipango yao beki Konate.
Hata hivyo, ripoti kutoka Ujerumani kwenye gazeti la Bild limefichua Bayern imefanya mawasiliano na mawakala wa Konate kwa ajili ya kutimiza mpango wao wa kumvuta beki huyo kwenda kukipiga Bundesliga, mahali ambako alijitengenezea jina kubwa alipokuwa RB Leipzig kabla ya kujiunga na Liverpool.
Uhamisho wake unaibua mashaka juu ya hatima ya Dayot Upamecano endapo kama ataendelea kubaki Allianz Arena. Upamecano, kama Konate, mkataba wake utakwenda kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu.
Real Madrid kwenye mabeki wake kuna mastaa kama Eder Militao, David Alaba na Antonio Rudiger, lakini bado inataka kuboresha kwenye eneo hilo kwa kumsajili Konate.
Mwaka jana, Liverpool yenyewe ilijikuta kwenye wakati mgumu baada ya wachezaji wake muhimu Mohamed Salah na Virgil van Dijk mikataba yao kufika mwisho kwa wakati mmoja, ilipambana kuwaongezea dili jipya, lakkini mkali mwingine Alexander-Arnold hakuongeza mkataba na kuamua kutimkia Bernabeu.
Konate, ambaye aliigharimu Liverpool Pauni 36 milioni kwenye usajili wake na kuitumikia timu hiyo kwenye mechi 147 amekuwa kwenye wakati mgumu msimu huu kutokana na miamba hiyo ya Anfield kuruhusu mabao kirahisi.