Madrid yajiondoa dili la Guehi, Liver, Bayern zaachiwa Uwanja
Muktasari:
- Inaelezwa Madrid imeachana na mpango wa kutaka kumsajili staa huyu kutokana na kiasi kikubwa cha pesa anachohitaji ambacho ni mjumuisho wa mshahara wake pamoja na bonasi ya kusajili.
REAL Madrid imejiondoa katika harakati za kutaka kumsajili beki kisiki wa Crystal Palace, Marc Guehi, 25, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Inaelezwa Madrid imeachana na mpango wa kutaka kumsajili staa huyu kutokana na kiasi kikubwa cha pesa anachohitaji ambacho ni mjumuisho wa mshahara wake pamoja na bonasi ya kusajili.
Hata hivyo, ripoti kutoka tovuti ya AS ya Hispania zinaeleza Bayern Munich na Liverpool zimeonyesha kuwa tayari kumpa Guehi anachohitaji na bado zinapambana kuhakikisha zinamsajili.
Madrid inaonekana kupanga mkakati wa kuhamia kwa beki wa Liverpool, Ibrahim Konate ambaye inaamini mahitaji yake sio makubwa sana kama ilivyo kwa Guehi.
Guehi ambaye ni nahodha wa Palace, dirisha lililopita la usajili wa majira ya kiangazi alikaribia kujiunga na Liverpool kabla ya dili kufeli katika dakika za mwisho baada ya kocha wake kuzuia.
Vyanzo mbalimbali vinadaiwa Guehi anataka mshahara wa takribani Pauni 300,000 kwa wiki na bonasi ya usajili ya zaid ya Pauni 8 milioni kwa mwaka.
Givairo Read
TIMU kibao kutoka Ligi Kuu England zinapigana vikumbo katika vita ya kuiwania saini ya beki wa kulia wa Feyenoord na timu ya taifa ya Uholanzi, Givairo Read kuelekea dirisha lijalo. Hata hivyo, wanadaiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa Bayern Munich ambayo inahitaji huduma ya fundi huyu pia. Inaelezwa Bayern ndiyo ilikuwa ya kwanza kuonyesha nia ya kumsajili Givairo baada ya maskauti wake kupendekeza hilo tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Konstantinos Koulieraki
TOTTENHAM na Liverpool zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya beki kisiki wa Wolfsburg na timu ya taifa ya Ugiriki, Konstantinos Koulieraki, 21, dirisha lijalo la majira ya baridi. Mabosi wa Wolfsburg wapo tayari kumuuza fundi huyu lakini wanahitaji kiasi kisichopungua Euro 40 milioni ili kufanya hivyo. Liverpool inatamani sana kumpata Januari mwakani ili kuboresha safu yao ya ulinzi inayoonekana kuwa na mapungufu tangu kuanza kwa msimu huu.
Marcus Rashford
BARCELONA ipo tayari kimsainisha mkataba wa moja kwa moja mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, 28, katika dirisha lijalo lakini haina uwezo wa kulipa Pauni 25.5 milioni ili kumnunua. Inadaiwa Rashford tayari ameshakubali hadi kupunguziwa mshahara ili abaki katika viunga hivyo lakini changamoto kuwa sasa inaonekana kuwa ni kiasi ambacho Man United inakihitaji.
Kenan Yildiz
JUVENTUS imepanga kuanza mazungumzo na wawakilishi wa mshambuliaji wao wa kimataifa wa Uturuki, Kenan Yildiz ambaye vigogo mbalimbali Ulaya, Liverpool, Chelsea na Arsenal zote zinahitaji saini yake. Dirisha lililopita, mabosi wa Juventus walikataa ofa mbalimbali kutoka kwa timu zilizomhitaji mshambuliaji huyu na wakasisitiza hauzwi lakini bado timu hizo hazionekani kukata tamaa.
Joshua Zirkzee
ROMA inajiandaa kuwasilisha ofa kwenda Manchester United ili kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo, Joshua Zirkzee kwa mkopo wa nusu msimu dirisha lijalo la usajili. Zirkzee ni miongoni mwa wachezaji walioomba kuondoka Old Trafford Januari mwakani kwa sababu hapati nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza cha mashetani hao wekundu.
Mateo Kovacic
ASTON Villa, AC Milan na West Ham bado zinapigana vikumbo ili kuipata saini ya kumsajili kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Croatia, Mateo Kovacic, mwenye umri wa miaka 31. Kovacic amekuwa haoati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Manchester City kwa muda sasa na anatamani kuondoka hara kwa mkopo ili kupata timu itakayompa nafasi ya kucheza.
Fundu huyu aliyesajiliwa na Man City kutoka Chelsea mwaka 2023, amekuwa na wakati mgumu tangu wasajiliwe Matheus Nunes na Marco Lewis ambao ndio wanaoneka kupewa nafasi kubwa zaidi ya kucheza.
Marc Andre Ter Stegen
LEEDS United ni miongoni mwa timu za England zinazopanga kumsajili kwa mkopo kila wa Barcelona, Marc Andre Ter Stegen dirisha lijalo la majira ya baridi. Staa huyu, 33, amekuwa na panda shuka nyingi kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na majeraha ya mara kwa mara. Kwa sasa haonekani kuwa na nafasi ya kwanza katika kikosi cha wababe hao wa Nou Camp.