Yamal afunga, Barca ikitoka nyuma mara tatu dhidi ya Club Brugge
Muktasari:
- Wenyeji walidhani wameibuka na ushindi katika dakika za majeruhi baada ya Romeo Vermant kumzidi ujanja Wojciech Szczesny na kufunga, lakini bao hilo likafutwa na mwamuzi msaidizi wa video (VAR) kwa kosa la kumchezea vibaya kipa.
BRUGGE, UBELGIJI: Lamine Yamal alifunga bao maridadi huku Barcelona ikitoka nyuma mara tatu na kulazimisha sare ya 3-3 dhidi ya Club Brugge katika mchezo wa kusisimua wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa Uwanja wa Jan Breydel usiku wa Novemba 5, 2025.
Wenyeji walidhani wameibuka na ushindi katika dakika za majeruhi baada ya Romeo Vermant kumzidi ujanja Wojciech Szczesny na kufunga, lakini bao hilo likafutwa na mwamuzi msaidizi wa video (VAR) kwa kosa la kumchezea vibaya kipa.
Club Brugge ilitangulia kufunga dakika ya sita kupitia Nicolo Tresoldi aliyemalizia pasi ya Carlos Forbs, ambaye alikimbia kwa kasi upande wa kulia kabla ya kutoa krosi ya chini.
Lakini ndani ya dakika mbili tu, Barca ilisawazisha kupitia shuti la kwanza la Ferran Torres lililotokana na krosi ya Fermin Lopez.
Fermin kisha alipiga shuti lililogonga mwamba, moja kati ya mara tatu ambazo Barcelona waligonga nguzo au mwamba wa goli.
Ghafla wakajikuta nyuma tena baada ya Brugge kupenya safu ya juu ya Barca kirahisi, Christos Tzolis akampasia Forbs, ambaye alitulia na kufunga ndani ya boksi.
Barca waligonga mwamba tena mara mbili, kwanza kupitia Jules Kounde na baadaye kombora kali la Eric Garcia kutoka umbali wa zaidi ya yadi 30.
Kisha Yamal akafanya yake akiwapita mabeki wawili kwa ustadi mkubwa, akacheza “one-two” na Dani Olmo kabla ya kumpita beki mwingine na kufunga kwa utulivu.
Forbs, ambaye alichezea Wolves kwa mkopo msimu uliopita, alipoteza nafasi ya wazi, lakini muda mfupi baadaye alijirekebisha kwa kupokea pasi murua ya Hans Vanaken na kumtesa kipa Szczesny.
Brugge walidhani wamepata penalti ya kufanya matokeo kuwa 4–2 baada ya mwamuzi Anthony Taylor kuamuru mkwaju huo kufuatia takolini ya Alex Balde dhidi ya Forbs, lakini VAR ikabatilisha uamuzi huo.
Barcelona ilitumia nafasi hiyo kujiokoa, Yamal akipiga krosi ambayo iligonga kichwa cha Tzolis na kuingia wavuni kama bao la kujifunga.
Katika dakika za mwisho, Szczesny aliyekuwa anachelewesha mpira alinusurika kisanga baada ya VAR kumsaidia kufuta bao ambalo Vermant alikuwa amefunga kwa kumpokonya mpira.