Barcelona sasa yamvutia kasi Marcus Rashford
Muktasari:
- Barca imehamia kwa Rashford baada ya kushindwa kumpata mshambuliaji wa Liverpool, Luis Diaz pamoja na Nico Williams wa Athletic Bilbao mwenye umri wa miaka 22.
MSHAMBULIAJI wa Manchester United na timu ya taifa ya England Marcus Rashford, 27, ni chaguo namba moja la Barcelona katika harakati zao za kumsajili winga wa kushoto katika dirisha hili.
Barca imehamia kwa Rashford baada ya kushindwa kumpata mshambuliaji wa Liverpool, Luis Diaz pamoja na Nico Williams wa Athletic Bilbao mwenye umri wa miaka 22.
Dili la Diaz lilifeli kwa sababu Liverpool ilihitaji kiasi kikubwa zaidi tofauti na bajeti ya Barca wakati Nico amesaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Bilbao baada ya Barca kushindwa kumhakikishia ikiwa ataingizwa kwenye mfumo.
Nico ambaye alihitaji sana kujiunga na Barca aliipa timu hiyo sharti moja la kuhakikisha anaingizwa katika mfumo wa kucheza La Liga isiwe tofauti na vile ilivyotokea kwa Dani Olmo.
Rashford ni miongoni mwa wachezaji waliopewa ruhusa ya kuondoka katika dirisha hili ikiwa ni baada ya kutoelewana na Kocha Ruben Amorim.
Msimu uliopita alicheza kwa mkopo Aston Villa ambako alionyesha kiwango bora akicheza mechi tofauti za michuano yote na kufunga mabao mawili. Mkataba wake wa sasa na Man United unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Mwenyewe amekuwa akitamani kucheza La Liga na hasa timu moja na Lamin Yamal na huenda hilo likatokea endapo Barca watakamilisha usajili wake.
Nicolas Jackson
Chelsea inahitaji Pauni 100 milioni kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wake wa kimataifa wa Senegal, Nicolas Jackson, mwenye umri wa miaka 24, katika dirisha hili. Saini ya fundi huyu inawindwa na timu mbalimbali barani Ulaya ikiwa ni pamoja na AC Milan. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2033. Alianza katika kikosi hicho cha The Blues na moto kabla ya mambo kuwa magumu na amekuwa hapati nafasi ya kutosha ya kucheza.
Jadon Sancho
Juventus imekubaliana kutoa Euro 20 milioni kwenda Manchester United kwa ajili ya kumsajili winga wa timu iyo na England, Jadon Sancho, katika dirisha hili. Sancho ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Chelsea, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026. Akiwa na Man United hakuwa na misimu mizuri na alilazimika kwenda kwa mkopo Borrusia Dortmund kabla ya kurejea na kucheza kidogo na kutoelewana na kocha na kutimkia Chelsea.
Yoane Wissa
Tottenham bado ina nia ya kumsajili staa wa Brentford na timu ya taifa ya DR Congo, Yoane Wissa, licha ya kutokuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wawakilishi wake kwa sasa. Wissa ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026, anauzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 50 milioni. Msimu uliopita alikuwa nyota muhimu wa kikosi hicho na kiwango chake kuivutia Spurs.
Johan Bakayoko
PSV Eindhoven iko tayari kumuuza winga wao wa kimataifa wa Ubelgiji, Johan Bakayoko, 22, katika dirisha hili la majira ya kiangazi na huduma yake inahitajika na Everton, Nottingham Forest,Bournemouth, RB Leipzig na Bayer Leverkusen. Bakayoko ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026 msimu uliopita alicheza alionyesha kiwango bora na sasa PSV inataka kumuuza ili ivune pesa.
James McAtee
MABOSI wa Nottingham Forest inapanga kutoa ofa ya Pauni 25 milioni pamoja na nyongeza kwa ajili ya kiungo mshambuliaji wa Manchester City na timu ya taifa ya England kwa vijana wenye umri chini ya miaka 21, James McAtee. Hata hivyo, ofa hiyo inaonekana kuwa ndogo sana tofauti na pesa ambazo Man City inazihitaji zinazoripotiwa kuwa ni pauni 40 milioni.
Giorgio Scalvini
Atalanta inataka ofa ya angalau Pauni 50 milioni kwa timu yoyote itakayohitaji huduma ya beki wao wa kimataifa wa Italia mwenye umri wa miaka 21, Giorgio Scalvini ili kuwauzia katika dirisha hili. Fundi huyu aliyeonyeha kiwango bora msimu uliopita, huduma yake inahitajika na vigogo mbalimbali barani Ulaya ikiwemo Newcastle United na Manchester United.
Marco Bizot
Aston Villa ipo karibu kukamilisha usajili wa kipa wa Brest, Marco Bizot mwenye umri wa miaka 34 katika dirisha hili. Staa huyu wa kimataifa wa Hispania anadaiwa atajiunga na Villa kwa ada ya uhamisho ya Euro 7 milioni. Mkataba wake na Brest kumalizika mwaka 2026 na inaelezwa ubora wake ndiyo ulioifanya Villa kuiwania saini yake mapema.