Barca yampiga stop Lewandowski kufunga
Muktasari:
- Lewandowski, 37, alijiunga na Barca mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 42.5 milioni akitokea Bayern Munich, ambako alitumikia miamba hiyo ya Bundesliga kwa miaka minane.
BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA imeripotiwa kumwomba straika Robert Lewandowski asifunge tena mabao wakati wa msimu wake wa kwanza kwenye kikosi hicho cha La Liga.
Lewandowski, 37, alijiunga na Barca mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 42.5 milioni akitokea Bayern Munich, ambako alitumikia miamba hiyo ya Bundesliga kwa miaka minane.
Lewandowski alitua Nou Camp katika kipindi kigumu cha kiuchumi. Katika msimu wake wa kwanza, staa huyo wa kimataifa wa Poland aliisaidia Barca kushinda ubingwa wa La Liga, huku akifunga mabao 23 katika mechi 34.
Lakini, katika ripoti yake iliyotolewa na kitabu cha Lewandowski, kinachoitwa ‘Lewandowski: the real one’, ambacho kimechapishwa na kuandikwa na mwandishi Sebastian Staszewski: Ilidaiwa kwamba straika huyo aliombwa asifunge tena mabao katika mechi mbili za mwisho za msimu wa 2022-23. Kitabu hicho kilieleza kwamba Lewandowski aliwekwa kikao na wajumbe wa bodi, akiwamo rais wa klabu Joan Laporta.
Na kwenye kikosi hicho, straika huyo wa zamani wa Borussia Dortmund aliombwa asifunge tena hadi msimu umalizike. Kipindi hicho, Barca tayari ilishajinyakulia kombe, hiyo ilitaka kukwepa kuilipa Bayern bonasi ya Pauni 2.2 milioni, ambayo wangelipwa endapo kama Lewandowski angefikisha mabao 25 msimu huo.
Kitabu hicho kilifichua: “(Barcelona ilimtaka Lewandowski): ‘Robert, tunataka uache kufunga mabao katika mechi za mwisho’.”
Lewandowski alimaliza mechi mbili za mwisho katika msimu huo bila kufunga bao, lakini idadi yake ya mabao tayari ilitosha kumfanya ashinde tuzo ya mfungaji bora kwenye La Liga.