Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ballon d’Or 2025 namba zinazungumza

BALON Pict

Muktasari:

  • Lakini, makala haya yanaangazia viwango vya wachezaji hao katika kila mechi za michezo yote waliyocheza msimu uliopita, kupata taswira ya mshindi anavyoweza kupatikana, huku uchambuzi huu ukingatia takwimu za mtandao wa WhoScored.

PARIS, UFARANSA: MAJINA 30 ya mastaa wa soka yametajwa kwenye mchakato wa kuwania tuzo ya Ballon d’Or 2025 kwa kuzingatia ubora wa viwango vyao kwenye mechi walizocheza msimu wa 2024-25.

Nani anapaswa kutangazwa mshindi? Ni suala la kungoja, kuona itakuwaje.

Lakini, makala haya yanaangazia viwango vya wachezaji hao katika kila mechi za michezo yote waliyocheza msimu uliopita, kupata taswira ya mshindi anavyoweza kupatikana, huku uchambuzi huu ukingatia takwimu za mtandao wa WhoScored.

Kwa kuzingatia takwimu za viwango vya WhoScored, straika mpya wa Arsenal, Viktor Gyokeres, kiufundi alionekana kuwa mchezaji bora msimu uliopita.

Hata hivyo, ligi ya Ureno haipo miongoni mwa ligi tano kubwa za Ulaya, hivyo takwimu zake hazipewi kupaumbele kikubwa, licha ya kwamba zilikuwa bora.

Katika michuano yote ya klabu na timu ya taifa, alihusika katika mabao 80 kwenye mechi 58, akifunga mabao 63 na kuasisti mara 17, huku akiwa na wastani wa rating ya 8.01 kwa mechi.

Kwa wachezaji waliopo kwenye ligi tano kubwa za Ulaya kwa msimu uliopita, Lamine Yamal amekuwa na wastani mkubwa wa rating akiwa na 7.91.

Katika mechi 62 alizochezea klabu yake na timu ya taifa, staa huyo wa Barcelona, Yamal amechangia mabao 47 huku akibeba mataji matatu, ikiwamo La Liga.

Kwa kutazama kigezo cha rating, mchezaji mwenzake Yamal huko kwenye kikosi cha Barcelona, Raphinha, amekuwa mchezaji wa tatu duniani kwa kuwa na wastani mkubwa wa rating zake za msimu uliopita, akiwa na 7.69.

Mbrazili huyo alikuwa na mchango mkubwa Barcelona, hasa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambako alichangia mabao 21 katika mechi 14.

Staa wa Bayern Munich, Michael Olise anashika namba nne baada ya kufanya vyema katika msimu wake wa kwanza Ujerumani, ambako wastani wake kwenye rating ni 7.57. Lakini, wengi walishtuka juu ya Kylian Mbappe kuwa na wastani mkubwa wa rating kuwazidi Ousmane Dembele, Mohamed Salah na Harry Kane.

Wakati staa huyo wa Real Madrid akiwa hajabeba taji lolote kwa msimu wa 2024-25, lakini alikuwa na wakati mzuri katika msimu wake wa kwanza Hispania.

Alivunja rekodi ya mabao ya Cristiano Ronaldo ya kufunga mara nyingi kwenye msimu wa kwanza Real Madrid, alipotikisa nyavu mara 44 katika michuano yote.

Mchezaji mwenzake kwenye soka la kimataifa, Dembele, ana wastani wa rating 7.53, ambayo ni pungufu kwa 0.01 dhidi ya ile ya Mbappe.

Kwa mashabiki wengi wa soka, wanaamini staa huyo wa PSG, Dembele anapewa nafasi kubwa ya kushinda Ballon d’Or msimu huu, shukrani kwa mchango wake mkubwa aliotoa kwenye kikosi cha Luis Enrique kilichobeba ubingwa wa Ulaya.

Straika nyota wa Bayern Munich, Harry Kane naye ana wastani wa rating 7.53.

Nahodha huyo wa England amekuwa na msimu mtamu huko Ujerumani, alipofunga mabao 41 katika michuano yote na alibeba ubingwa wa Bundesliga.

Kuhusu supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah wastani wake wa rating kwa msimu uliopita haukuwa bora sana, huku akilingana na straika Erling Haaland.

Hata hivyo, Mo Salah alikuwa na kiwango bora kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, alipoisaidia Liverpool kubeba ubingwa, huku alifanya vizuri pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ligi.

Wachezaji Gianluigi Donnarumma, Fabian Ruiz, Denzel Dumfries na Scott McTominay ndiyo wenye wastani mdogo wa rating za mechi kuliko wengine wote walioorodheshwa kuwania Ballon d’Or 2025.