IFFHS yamfuta machozi Messi
Muktasari:
- IFFHS imesema uamuzi huo umetokana na mfumo wake maalumu wa tathmini unaotegemea takwimu za kina za utendaji wa wachezaji katika mashindano yote.
NEW YORK, MAREKANI: LICHA ya Argentina kupoteza katika fainali ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Hispania na kiungo Rodri kutwaa tuzo rasmi ya Mchezaji Bora 'Golden Ball ya FIFA', Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka (IFFHS) limemtangaza Lionel Messi kuwa Mchezaji Bora wa Mashindano.
IFFHS imesema uamuzi huo umetokana na mfumo wake maalumu wa tathmini unaotegemea takwimu za kina za utendaji wa wachezaji katika mashindano yote.
Kwa mujibu wa shirikisho hilo, tuzo hiyo hutolewa kupitia IFFHS Overall Performance Index, mfumo unaochambua kwa uzito tofauti kiwango cha mchezaji katika kila mechi, mabao aliyofunga, pasi za mabao (asisti) pamoja na mchango wake katika hatua za mtoano.
"Baada ya uchambuzi wa kina wa kila kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji katika Kombe la Dunia la 2026, hitimisho ni wazi kabisa," ilisema IFFHS.
TAKWIMU ZA MESSI ZAMWEKA KILELENI
IFFHS imeeleza kuwa Messi alifunga mabao nane na kutoa asisti nne katika mechi nane alizoichezea Argentina, huku akipata wastani wa alama 8.33 kwa kila mchezo.
Shirikisho hilo limesisitiza kuwa kiwango hicho hakikutokana na ubora wa mechi chache pekee, bali ni uthabiti aliouonyesha kuanzia hatua ya makundi hadi fainali.
"Uthabiti huo chini ya presha ndio unaomtenganisha mshindi halali na wale waliocheza vizuri tu," ilieleza taarifa hiyo.
ALING'ARA ZAIDI HATUA ZA MTOANO
IFFHS imeongeza kuwa mfumo wake huweka uzito mkubwa kwa mchango wa mchezaji katika hatua za mtoano, ambako makosa yanaweza kuiondoa timu kwenye mashindano.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, Messi alikuwa na mchango mkubwa katika safari ya Argentina hadi fainali, huku akiongoza orodha ya wachezaji wote kwa alama za jumla zilizokusanywa kupitia vigezo mbalimbali vya tathmini.
"Jopo la IFFHS, likiongozwa kikamilifu na ushahidi wa takwimu na rekodi za utendaji, limefikia hitimisho hili kwa kujiamini kabisa. Lionel Messi ndiye Mchezaji Bora wa Kombe la Dunia wa IFFHS, si kwa sababu ya hisia au jina lake kubwa, bali kwa sababu takwimu zimethibitisha hilo," ilihitimisha taarifa ya shirikisho hilo.