Arteta: Mastaa wangu watatu wagonjwa
Muktasari:
- Eberechi Eze ndiye aliyefunga bao pekee katika mechi hiyo, alipowaadhibu waajiri wake wa zamani kuisaidia Arsenal kushindi 1-0 uwanjani Emirates.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amethibitisha wachezaji wake watatu kupata majeraha kwenye mechi ya ushindi dhidi ya Crystal Palace kwenye Ligi Kuu England, jana Jumapili, Oktoba 26.
Eberechi Eze ndiye aliyefunga bao pekee katika mechi hiyo, alipowaadhibu waajiri wake wa zamani kuisaidia Arsenal kushindi 1-0 uwanjani Emirates.
Lakini, ushindi huo uligubikwa na majeraha ya wachezaji Declan Rice, William Saliba na Riccardo Calafiori, ambao wote walilazimika kutolewa uwanjani.
Wachezaji hao watatu wamekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Arsenal katika msimu huu, hivyo jambo hilo ni pigo kubwa kwa kocha Arteta. Arteta amesema: “William Saliba aliumia. Declan (Rice) naye aliumia pia.
“Wa kwanza alikuwa Willy (Saliba) kuumia. Na Ricci (Calafiori) pia.
“Sifahamu ukubwa au chanzo cha maumivu yao, sio kwamba sitaki kuwaambia, lakini sifahamu.
“Kwa Willy, kuna vitu viwili vilivyosababisha kutolewa kwake. Kuhusu Declan sina uhakika kama ni kigimbi au ni msuli wa kisigino.”
Rice alitolewa uwanjani kwenye mechi iliyopita pia dhidi ya West Ham United ilipojaribiwa kumnusuru kupata maumivu zaidi baada ya kulalamika kuumwa mgongo.
Tatizo la mguu wa kulia lilimfanya atolewe uwanjani katika dakika za mwisho dhidi ya Palace. Saliba alitolewa uwanjani wakati wa mapumziko na Mfaransa huyo alikosa mechi moja kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.