Arteta azidi kumtetea Gyokeres
Muktasari:
- Arsenal ililazimisha sare ya bao 1-1 nyumbani kwenye Uwanja wa Emirates ikichomoa bao dakika za jioni lililofungwa na Gabriel Martinelli na kutuliza presha baada ya kuwa nyuma kwa zaidi ya dakika 80.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya Victor Gyokeres kuonyesha kiwango cha chini katika mchezo mgumu wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City, Kocha wa miamba hiyo ya London amemtetea, huku akiitaka timu kuendelea kumsaidia.
Arsenal ililazimisha sare ya bao 1-1 nyumbani kwenye Uwanja wa Emirates ikichomoa bao dakika za jioni lililofungwa na Gabriel Martinelli na kutuliza presha baada ya kuwa nyuma kwa zaidi ya dakika 80.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden aliyeigharimu Arsenal Pauni 64 milioni dirisha lililopita, katika mchezo huo, alishindwa kufunga wala kutengeneza nafasi za hatari jambo lililowatia hofu mashabiki wa timu hiyo.
Akicheza dakika zote 90, takwimu zinaonyesha Gyokeres aligusa mpira mara 24 tu, ikiwa ni mchezaji aliyefanya hivyo mara chache zaidi uwanjani na alipoteza mipira mara 13 na kushindwa kukokota mipira, huku akipiga pasi sahihi kwa asilimia 62 pekee.
Licha ya kushindwa huko kuonyesha makali yake kama alivyokuwa Sporting Lispon ya Ureno, Arteta alimlinda kwa kusema bado anatakiwa apewe nafasi zaidi na kumsaidia acheze kwa nguvu ili afunge.
“Kweli, kulikuwa na mipira mingi mizuri eneo la hatari, nakumbuka mitatu aliyokuwa karibu kufunga, hakika anajitahidi kadri awezavyo na sisi lazima tumpe zaidi nafasi, nafasi zilikuwepo lakini hakukuwa na pasi za mwisho kwenda kwake.”
Gyokeres ameshindwa kutamba katika mechi ngumu za Arsenal na mabao yake matatu aliyofunga hadi sasa ligi kuu ni dhidi ya Leeds United iliyopanda daraja hivi karibuni na Nottingham Forest inayoonekana kuchechemea tangu kuanza kwa msimu na hilo limekuwa likionyesha wasiwasi kutokana na pesa nyingi iliyotolewa kuinasa huduma yake.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Arteta inaonyesha bado ana imani na mchezaji huyo na atazidi kuimarika katika michezo ijayo ikiwamo wa Ligi Kuu dhidi ya Newcastle United ugenini. Huenda pia akawepo katika mchezo wa Kombe la Carabao utakaopigwa Jumatano, Septemba 24 na Arsenal itacheza dhidi ya Port Vale.