Arteta awatishia watu Gyokeres
Muktasari:
- Gyokeres, 27, alikuwa mmoja wa mastaa wa usajili wa pesa nyingi uliofanyika dirisha la majira ya kiangazi lililopita, aligharimu Pauni 64 milioni aliponaswa kutoka Sporting Lisbon na kuhitimisha ndoto za msako wao wa straika.
LONDON, ENGLAND: KOCHA Mikel Arteta amewaonya wapinzani wa Arsenal kwenye mbio za ubingwa straika wake butu kwa sasa, Viktor Gyokeres atawasha moto kwenye mzunguko wa pili msimu huu.
Gyokeres, 27, alikuwa mmoja wa mastaa wa usajili wa pesa nyingi uliofanyika dirisha la majira ya kiangazi lililopita, aligharimu Pauni 64 milioni aliponaswa kutoka Sporting Lisbon na kuhitimisha ndoto za msako wao wa straika.
Lakini, straika huyo wa kimataifa wa Sweden, Gyokeres amekosa makali, akifunga mabao manne tu kwenye Ligi Kuu England. Mabao hayo alifunga dhidi ya Leeds United, Nottingham Forest na Burnley, klabu tatu zinapambana kuhakikisha zinabaki.
Gyokeres alitolewa uwanjani dakika 81 katika mechi ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Wolves uwanjani Emirates, akiwa amepiga shuti moja tu katika mechi hiyo dhidi ya timu inayoburuza mkia.
Lakini, kocha Arteta anaamini straika huyo wa zamani wa Coventry City atakuwa moto kwenye mzunguko wa pili wa ligi kwa sababu atahitaji muda wa kutosha wa kuzoeana na wachezaji wenzake.
Katika kuelekea mechi ya ugenini dhidi ya Everton iliyofanyika Jumamosi usiku, Arteta alisema: "Kila mtu alifurahia tulipomleta kwenye timu. Tulifanya hivyo. Tulimsajili mchezaji aliyekuwa hodari kwa kufunga ambaye pia atazoea mazingira ya ligi. Hakuwa na pre-season. Wiki za kwanza zilikuwa ngumu kwake kwa sababu hakuwa na fiziki ya kutosha inayohitajika kuwa naye mchezaji kwenye ligi hii. Kisha akaanza kutulia, lakini nadhani alikuwa mzuri hadi hapo alipopata majeraha. Sasa amerudi. Nimeona vitu vinavyovutia katika mechi mbili zilizopita. Nadhani tunahitaji kumpa sapoti."
Alipoulizwa kama mashabiki watamshuhudia Gyokeres kwenye kiwango tofauti kabisa mwaka 2026, kocha huyo wa Arsenal alisema: "Nadhani, ni hivyo."
Kocha Arteta amewataka wachezaji wenzake kwenye kikosi cha Arsenal kuhakikisha wanamsaidia Gyokeres anatimiza wajibu wake wa kufunga mabao kwa kumtengenezea nafasi za kutosha.