Arteta asaka nyota zaidi Arsenal
Muktasari:
- Baada ya kuiongoza Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22 msimu uliopita, Arteta amesema lengo lao ni kuendelea kuboresha kikosi ili kutetea taji hilo kwa mafanikio.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema mabingwa hao wa Ligi Kuu England hawana mpango wa kutulia katika dirisha la usajili, akisisitiza klabu hiyo itaendelea kuimarisha kikosi kwa usajili wa wachezaji wenye ubora ili kuongeza ushindani wa ndani.
Baada ya kuiongoza Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22 msimu uliopita, Arteta amesema lengo lao ni kuendelea kuboresha kikosi ili kutetea taji hilo kwa mafanikio.
Mpaka sasa, Arsenal imewasajili kipa Illan Meslier na mshambuliaji Christos Tzolis, huku beki Piero Hincapie akisaini mkataba wa kudumu baada ya kucheza kwa mkopo.
Aidha, Arsenal inatajwa kuwa karibu kukamilisha usajili wa kiungo wa Brazil, Bruno Guimaraes kutoka Newcastle United, huku pia ikihusishwa na nyota wa Real Madrid, Vinicius Jr.
Akizungumza baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Girona katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu mpya, Arteta amesema bado kuna mabadiliko zaidi yanatarajiwa ndani ya kikosi chake.
"Tunatarajia kutakuwa na mabadiliko katika wiki chache zijazo. Tunataka kuwa bora zaidi kama ilivyo kwa klabu nyingine, na mnaweza kuona kinachoendelea kwenye soko la usajili pamoja na wapinzani wetu," amesema Arteta.
Kocha huyo amesisitiza kuwa Arsenal haitabaki nyuma wakati timu nyingine zikiendelea kuimarisha vikosi vyao.
"Hatutakaa kimya. Tuna malengo makubwa na tunaonyesha hilo kupitia tunachokifanya. Tofauti za ushindani ni ndogo sana, hivyo tunapaswa kuendelea kuboresha kikosi na kuongeza ushindani wa ndani," amesema.
Ameongeza kuwa benchi la ufundi linaendelea kutambua maeneo yanayohitaji maboresho ili kuhakikisha Arsenal inabaki kwenye kiwango cha juu.
"Tunapaswa kuhakikisha tunapata vitu ambavyo bado hatuna ndani ya kikosi chetu. Hilo ndilo litakalotusaidia kuendelea kukua na kushindana kwa kiwango cha juu," amesema Arteta.
Arsenal itaanza msimu mpya kwa kucheza dhidi ya Manchester City katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 16, kabla ya kuikaribisha Coventry City katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu England, Agosti 21.