Bruno Guimaraes atua kambini Newcastle, dili la Arsenal lapamba moto
Muktasari:
- Kiungo huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 28 anatarajiwa kufanya mazungumzo na kocha mpya wa Newcastle, Matthias Jaissle, ili kueleza wazi nia yake ya kutaka kuondoka katika dirisha hili la usajili.
Nahodha wa Newcastle United, Bruno Guimaraes, anatarajiwa kujiunga na kambi ya mazoezi ya timu hiyo nchini Hispania huku tetesi za kuhamia Arsenal zikiendelea kushika kasi.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 28 anatarajiwa kufanya mazungumzo na kocha mpya wa Newcastle, Matthias Jaissle, ili kueleza wazi nia yake ya kutaka kuondoka katika dirisha hili la usajili.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Guimaraes hana mpango wa kuendelea kubaki St James' Park baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Eddie Howe, pamoja na mastaa wenzake Anthony Gordon na Sandro Tonali.
Wakati huo huo, Arsenal inaelezwa kuwa ipo tayari kuwasilisha ofa ya zaidi ya pauni milioni 75 (takribani Sh267.05 bilioni) kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo.
Licha ya Guimaraes kuwa na mkataba wa kuendelea kuitumikia Newcastle hadi mwaka 2029, inaelezwa kuwa anatamani kufanya kazi chini ya kocha Mikel Arteta na kuwa sehemu ya kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu England.
Kwa sasa, Arsenal na Newcastle zinaendelea na mazungumzo kuhusu ada ya uhamisho, huku kila upande ukisaka makubaliano yatakayokamilisha moja ya dili kubwa zaidi katika dirisha la usajili la kiangazi.