Arteta, Arsenal picha linaendelea
Muktasari:
- Hali siyo nzuri pale mitaa ya Islington, kutokana na matokeo hayo na ndiyo kwanza msimu upo raundi ya tano, mashabiki wa Arsenal wameanza kumkalia kichwani Arteta, wanataka aondoke. Wengi wanasema hana uwezo wa kuwawezesha kuchukua ubingwa.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imecheza mechi ya tano Ligi Kuu England, imeshinda tatu sare moja na kufungwa moja na katika msimamo ipo katika nafasi ya pili. Ina utofauti wa alama tano dhidi ya vinara Liverpool.
Hali siyo nzuri pale mitaa ya Islington, kutokana na matokeo hayo na ndiyo kwanza msimu upo raundi ya tano, mashabiki wa Arsenal wameanza kumkalia kichwani Arteta, wanataka aondoke. Wengi wanasema hana uwezo wa kuwawezesha kuchukua ubingwa.
Huu ni mwaka wa tano wa Arteta katika viunga vya Emirates, sehemu aliyowahi kuhudumu kama mchezaji kabla ya kurejea kama kocha. Katika miaka hiyo mitano amechukua taji moja tu la FA msimu wa 2019/20 ingawa pia amewahi kushinda ngao ya jamii mara mbili.
Mashabiki wa Arsenal wanamwona ni mtu ambaye hakuna mahali anaweza kuwafikisha. Msimu uliopita ulikuwa ni wa tatu kwa Arsenal kumaliza nafasi ya pili na moja kati ya mambo iliyosemakana yanawakwamisha ni eneo la ushambuliji.
Raheem Sterling aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka Chelsea hakuonyesha kiwango kilichotarajiwa, pia Gabriel Jesus hakuwa anapatikana muda mwingi kutokana na hali yake ya majeraha.
Msimu huu Arteta alifanikiwa kusajili mshambuliaji akimchukua Viktor Gyokeres ambaye hadi sasa bado hajaonyesha makali yake aliyokuwa anayaonyesha akiwa na Sporting Lisbon.
Wakati ambao Mhispania huyu akihitaji kuaminiwa zaidi kwa ajili ya kuendelea kuifanya timu hiyo kuwa shindani zaidi, mioyo ya mashabiki imeshakata tamaa.
Mashabiki wanaonekana wameshiba sana na kile ambacho amewapa, sasa wanataka vinywaji baridi vya kushushia.
Historia inaonyesha tangu msimu wa 2005/06, ikiwa chini ya Arsen Wenger pamoja na Unai Emery, Arsenal haijawahi kuwa na rekodi nzuri kama ilivyo sasa.
Kuanzia wakati huo, ni Arteta pekee ndio ameiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi yapili kwa misimu mitatu mfululizo jambo ambalo halijawahi kufanywa kwa muda tajwa hapo juu.
Changamoto kubwa pengine inayomkumba Mhispania huyu ni kutokuwa tu na imani. Mashabiki wengi wanataka aondoke na jibu kubwa la swali lao ni amemaliza misimu mitatu katika nafasi ya pili hawezi kuwapa chochote.
Arteta hakuamka usingizini na kumaliza nafasi hiyo, kocha huyu alikuwa katika wakati mgumu sana kwenye misimu yake mitatu ya kwanza. Mashabiki hawakuwa wanataka kusikia chochote kuhusu yeye.
Pengine kilichomsaidia kwa wakati huo ilikuwa ni kushinda taji la FA ingawa hilo pia halikuwa geni sana kwao kwani walishashinda sana chini ya Wenger lakini iliwapoza kwa kuona huenda kuna ishara njema mbele.
Kocha huyu alihitaji misimu mitatu ya kujichanga kabla ya kumaliza nafasi ya tatu katika misimu mitatu iliyofuatia na katika hiyo misimu mitatu ya kwanza mmoja aliikuta timu ikiwa katikati.
Sio kweli Arteta ameshindwa kuipa Arsenal ubingwa, lakini ni ukweli wamechoka kusubiri zaidi.
Jurgen Klopp alihitaji misimu mitano kabla ya kuipa Liverpool ubingwa wake wa kwanza baada ya takribani miaka 30.
Muda mwingine ni ngumu kuamini Arsenal inacheza vibaya, ndiyo maana inakosa ubingwa. Wataalam wa mambo wanasema licha ya kwamba mpira siku zote ni sayansi, pia ndani yake lazima kuwe na bahati na muda.
Arteta amefanya kila linalowezekana kwa upande wa sayansi, lakini kuna nyakati anakosa bahati. Nani aliwaza Gyokeres aliyeimeza ligi ya Ureno angekuwa na mwenendo wa kusuasua kama anaouonyesha kwa sasa? Inawezekana muda wa Arsenal kuchukua ubingwa ni karibu kuliko wanavyofikiria, lakini je watakuwa tayari kusubiri kufa na kiu haliyakuwa wameshashiba.
Inaweza mashabiki wa Manchester United wenye njaa wanatamani hata asilimia 70 ya kiwango ambacho kinaonyeshwa na Arsenal kionyeshwe na timu yao lakini hiyo yote ni kwa sababu wana njaa.
Arteta alianza na msingi na ameshachora ramani sijui kama kocha atakayeajiriwa baada ya yeye ataweza kujenga katika hiyo ramani au atataka kujenga vya kwake na ikifikia wakati huo, hiki chakula ambacho kimewajaa tumboni kitakuwa hakipo na pengine watatamani hata kula bila maji lakini muda hautokuwa rafiki.
Wiki iliyopita kulikuwa na mechi pale Emirates, Manchester City ya mwalimu wa Arteta, Pep Guardiola ilikuwa na wakati mgumu, katika hali isiyotarajiwa, kocha huyo anayehusudu sana soka la kushambulia na kumiliki mpira muda wote alilazimika kuzuia muda mwingi wa mchezo.
Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kocha huyo kufanya hivyo, takwimu za mwisho wa mchezo zilionyesha alikuwa na umiliki wa asilimia 32, haijawahi kutokea.
Timu kubwa na ndoto sasa zinaliona dimba la Emirates kama sehemu tishio.
Hakuna anayependa kuweka mguu wake katika nyasi za Uwanja huo. Muda unahitajika zaidi, pengine baada ya msimu mmoja au miwili huenda akawafikisha nchi ya ahadi lakini je watavumili? acha sinema liendelee.