Arteta amtisha straika Gyokeres
Muktasari:
- Gyokeres, 27, amefunga mabao matatu tu tangu alipojiunga na Arsenal kutokea Sporting Lisbon na kabla ya mechi ya Jumamosi, alitoka patupu kwenye mechi sita alizochezea The Gunners.
LONDON, ENGLAND: KOCHA Mikel Arteta amemwonya straika wake Viktor Gyokeres angechagua kwenda kujiunga na timu nyingine endapo kama atashindwa kuendana na presha ya kufunga mabao inayomkabili kwa sasa kwenye Ligi Kuu England.
Gyokeres, 27, amefunga mabao matatu tu tangu alipojiunga na Arsenal kutokea Sporting Lisbon na kabla ya mechi ya Jumamosi, alitoka patupu kwenye mechi sita alizochezea The Gunners.
Alitoka kapa kwenye mechi nyingine mbili alizochezea timu ya taifa ya Sweden, huku ikifahamika wazi saini yake iliigharimu Arsenal, Pauni 63.5 milioni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Hata hivyo, Kocha Arteta hana wasiwasi Gyokeres atatulia na kuonyesha ubora wake kwenye kufunga mabao, aliposema: “Nafurahishwa na huduma anayopatiwa kwenye timu.
Nilimwambia kabla ya mkutano huu kwamba Namba 9 ninayemtaka ni Namba 9 ambaye kama anashindwa kufunga kwenye mechi sita au nane, anapaswa akubaliane na hiyo presha. Kama huwezi, yakipasa kwenda kwingineko. Hivyo, kama unavaa jezi Namba 9 ya Arsenal, unapaswa kuwa na uwezo wa kusema, ‘Ok, mechi sita, sijafunga. Je, mimi ni mchezaji tofauti? Je, naweza kuanza katika njia tofauti? Nataka aendelee kufanya zaidi na zaidi.
Arteta, ambaye ni kocha namba 10 aliyedumu kwa muda mrefu kwenye Ligi Kuu England, alibainisha pia kuhusu nahodha wa timu hiyo, kiungo Martin Odegaard, ataendelea kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti.