Arteta aingia angaa za Sir Ferguson
Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Hispania, mwenye umri wa miaka 44, anajiweka kwenye kundi la makocha wachache waliowahi kutwaa ubingwa wa England na kudumu kwa muda mrefu kwenye klabu zao.
LONDON, ENGLAND: KOCHA Mikel Arteta sasa anaingia rasmi katika kundi la makocha wenye nguvu na ushawishi mkubwa zaidi katika Ligi Kuu England, baada ya kukubaliana mkataba mpya utakaomfanya atimize miaka 10 akiwa Arsenal.
Kocha huyo raia wa Hispania, mwenye umri wa miaka 44, anajiweka kwenye kundi la makocha wachache waliowahi kutwaa ubingwa wa England na kudumu kwa muda mrefu kwenye klabu zao.
Arsene Wenger alidumu Arsenal kwa miaka 22, huku Sir Alex Ferguson akitumia miaka 27 Manchester United. Pep Guardiola alifikisha muongo mmoja Manchester City kabla ya kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita, wakati Jurgen Klopp alidumu miaka tisa Liverpool.
Sasa Arteta yuko njiani kufuata nyayo zao, huku mchambuzi wa soka na beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, hivi karibuni akimtaja kocha huyo kama mtu mwenye ushawishi mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu kwa sasa.
Carragher alisema: “Kwa sasa yeye ndiye 'don'. Yeye ndiye bingwa wa Ligi Kuu.”
Kauli hiyo ilikuja baada ya Arteta kukosoa uamuzi wa mwamuzi katika ushindi wa Arsenal wa mabao 2-0 dhidi ya Sunderland mwezi huu.
Licha ya timu yake kushinda, Arteta alisisitiza kuhusu penalti iliyotolewa kwa Sunderland, jambo lililogeuza mjadala mkubwa baada ya mchezo.
Kwa mtazamo wa Carragher, Arteta alikuwa akianza kuonyesha ushawishi aliokuwa nao Sir Alex Ferguson wakati wa utawala wake Manchester United.
“Alikuwa amedhamiria kuhakikisha ujumbe unafika kwamba jambo kama hilo lisijirudie tena kwa klabu yake. Tumeyaona haya kwa Sir Alex Ferguson na pia Jose Mourinho,” alisema Carragher.
Kwa namna ya kipekee, Sir Alex pia alihusika kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika safari ya Arteta kuelekea kuwa mmoja wa makocha wenye nguvu katika Ligi Kuu.
Arsenal ilimsajili Arteta kutoka Everton siku ya mwisho ya usajili wa majira ya kiangazi mwaka 2011, siku chache baada ya United kuichapa Arsenal mabao 8-2.
Arteta alikuwa mmoja wa wachezaji wanne waliosajiliwa na Arsenal katika siku hiyo yenye pilikapilika, na kwa miaka mitano iliyofuata alipata nafasi ya kujifunza chini ya Wenger.
Baadaye alitumia misimu mitatu kama msaidizi wa Guardiola ndani Manchester City, kabla ya kurejea Arsenal Desemba 2019 kuchukua mikoba ya ukocha.
Ushindani wake na Klopp nao ukafuata, huku wawili hao wakijikuta mara kadhaa wakikabiliana pembeni mwa uwanja, hasa katika michezo dhidi ya Liverpool.
Wakati huo Arteta alionekana kama kocha mpya aliyekuwa akijaribu kuvunja utawala wa makocha waliokuwa tayari wamejenga majina yao kwenye Ligi Kuu.
Lakini sasa ameingia kwenye kundi hilo la makocha wakubwa na anaonekana kutaka zaidi.
Mkataba mpya ni ishara nyingine ya dhamira hiyo, kama ilivyo kwa namna Arsenal ilivyoimarisha kikosi chake katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Usajili wa Arsenal ulikuwa wa aina ya kutaka mafanikio ya haraka, tofauti na falsafa ya kujenga kikosi taratibu kwa ajili ya mafanikio ya baadaye.
Wachezaji wawili waliotajwa kuwa usajili mkubwa wa Arsenal katika dirisha hilo ni Bruno Guimaraes na Ezri Konsa, waliogharimu jumla ya Pauni125 milioni.
Wote wana umri wa miaka 28 na tayari wamejijengea uzoefu katika Ligi Kuu, jambo linaloonyesha wazi kwamba Arteta hataki kusubiri muda mrefu kabla ya kuvuna matunda ya kazi yake.
Kuongeza mkataba wake pia kunatoa ujumbe kwa wachezaji waliopo Arsenal na wale ambao klabu hiyo inalenga kuwasajili.
Arsenal inataka kuwafungia mikataba mipya wachezaji muhimu kama David Raya, Declan Rice na Jurrien Timber, jambo ambalo linaweza kuwa rahisi zaidi iwapo Arteta ataendelea kuwepo Emirates.
Hali hiyo pia inaweza kusaidia katika mazungumzo na wachezaji wapya, hasa kwa kuwa Arsenal bado inalenga kuongeza mshambuliaji wa kiwango cha juu.
Mchezaji yeyote anayelengwa sasa atajua kwamba kocha anayehusika na ujenzi wa kikosi hicho amejikita kwenye klabu kwa muda mrefu.
Swali kubwa linabaki kuwa: Arteta ataendelea Arsenal kwa muda gani?
Ni vigumu kuona makocha wa kizazi cha sasa wakifikisha miaka 22 au 27 kwenye klabu moja kama Wenger na Ferguson, kutokana na ratiba ngumu na mahitaji makubwa ya soka la kisasa.
Miaka tisa ya Klopp ndani ya Liverpool au 10 ya Guardiola kwa Manchester City inaonekana kuwa mfano unaoweza kufikiwa zaidi na Arteta.
Hata hivyo, Barcelona na Paris Saint-Germain zinaweza kuwa sehemu ya mustakabali wake.
Ukarabati wa uwanja wa Camp Nou utakapokamilika, Barcelona inaweza kuwa chaguo linalovutia, huku Arteta akiwa na historia na klabu hiyo baada ya kukulia kwenye mfumo wake wa vijana.
PSG nayo si klabu ngeni kwake. Akiwa na umri wa miaka 18, Arteta alianza maisha yake ya soka la kulipwa nchini Ufaransa na alifurahia kipindi chake huko.
Changamoto kubwa kwake, hata hivyo, inaweza kuwa kupata klabu nyingine ambayo itampa kiwango cha ushawishi alichonacho Arsenal.
Guardiola alikumbana na hali hiyo. Alidumu Manchester City kwa miaka 10, lakini Barcelona kwa miaka minne pekee.
Emirates kwa sasa inaonekana kujengwa kwa falsafa ya Arteta, huku kila kitu kikifuata mtazamo wake wa soka.
Muda mfupi baada ya kupewa jukumu la kuinoa Arsenal, cheo chake kilibadilishwa kutoka kocha mkuu na kuwa meneja, na tangu hapo amekuwa na mamlaka makubwa katika ujenzi wa kikosi na mwelekeo wa klabu.
Arsenal ya sasa kwa kiasi kikubwa imejengwa kwa maono yake, jambo linalofanya kuondoka kuwa uamuzi mzito endapo siku moja ataanza kufikiria changamoto mpya.
Arteta sasa ameingia kwenye tabaka la makocha wenye heshima kubwa katika Ligi Kuu England, na mkataba mpya unaonyesha kwamba bado ana kiu ya kuendelea kujenga himaya yake Arsenal.