Arsenal yamgeukia Victor Osimhen
Muktasari:
- Arsenal kwa sasa iko katika mazungumzo na Galatasaray, ikijaribu kuwapunguza baadhi ya wachezaji katika kikosi chake, akiwamo Ethan Nwaneri na Gabriel Martinelli.
LONDON, ENGLAND: Arsenal inataraji kukutana na upinzani katika harakati zake za kumsajili mshambuliaji wa Galatasaray, Victor Osimhen, iwapo itaamua kuendelea na mpango wa kumnasa nyota huyo.
Arsenal kwa sasa iko katika mazungumzo na Galatasaray, ikijaribu kuwapunguza baadhi ya wachezaji katika kikosi chake, akiwamo Ethan Nwaneri na Gabriel Martinelli.
Jina la Osimhen linadaiwa pia kujitokeza katika mazungumzo hayo kati ya klabu hizo mbili.
Hata hivyo, Galatasaray imeweka wazi msimamo wake wa kutaka kumbakiza mshambuliaji huyo na haionekani kuwa tayari kumuuza.
Klabu hiyo ya Uturuki tayari ilikataa ofa ya pauni milioni 111 kutoka kwa klabu ambayo haikutajwa jina msimu huu wa kiangazi, huku ikiaminika kuwa ofa hiyo ilitoka kwa Al-Hilal ya Saudi Arabia.
Hivyo, Arsenal itakuwa na kazi kubwa kubadili msimamo wa Galatasaray, ingawa inaweza kupata matumaini kutokana na kilichowahi kutokea kwa Newcastle kuhusu Bruno Guimaraes.
Osimhen ni mchezaji ambaye Arsenal imekuwa ikimfuatilia kwa muda mrefu, ikiwamo kipindi ambacho Edu alikuwa mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alifunga mabao 22 katika mashindano yote msimu uliopita na kuisaidia Galatasaray kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uturuki.
Arsenal iko sokoni kusaka mshambuliaji wa kiwango cha juu msimu huu wa kiangazi, baada ya kushindwa katika harakati za kumsajili Morgan Rogers na Vinicius Junior.
Arsenal pia inajaribu kupunguza idadi ya wachezaji katika kikosi chake, huku Martinelli na Nwaneri wakiwa miongoni mwa wanaoweza kuondoka.
Galatasaray imeonyesha utayari wa kulipa takribani pauni milioni 38 kwa ajili ya Martinelli, ingawa bado haijafahamika kama winga huyo wa Brazil atakuwa tayari kuhamia Uturuki.
Nwaneri, mwenye umri wa miaka 19, anadaiwa kupendelea kuhamia Ujerumani iwapo ataondoka Arsenal, huku Borussia Dortmund na RB Leipzig zikiwa na nia ya kumsajili.
Dortmund imekuwa ikimfuatilia kiungo huyo kwa muda mrefu na ilionyesha nia ya kumsajili msimu uliopita kabla ya Nwaneri kusaini mkataba wa miaka mitano na Arsenal.
Arsenal pia inataka kumuuza mshambuliaji Gabriel Jesus, huku Napoli ikiwa miongoni mwa klabu zinazopigiwa upatu kumsajili Mbrazil huyo.
Kiungo Fabio Vieira anataka kurejea Hamburg baada ya kutumia msimu uliopita kwa mkopo katika klabu hiyo, lakini pande hizo bado hazijaafikiana kuhusu ada ya uhamisho.
Winga Reiss Nelson naye analengwa na West Ham United, ambayo ina matumaini ya kukamilisha dili hilo licha ya klabu hiyo kushiriki Championship msimu huu.