Liverpool yatua Napoli ikimtaka Beukema
Muktasari:
- Kwa sasa Napoli inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Italia (Serie A), lakini haina uhakika wa kubeba ubingwa kutokana na kuachwa mballi na Inter Milan.
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool inadaiwa kuwasilisha ofa ya Napoli ili kumnunua beki wa kati wa kimataifa wa Uholanzi, Sam Beukema (27).
Dili hilo linakadiriwa kuwa na thamani ya Pauni 32 milioni na Liverpool inapambana kuhakikisha inapata mbadala sahihi wa Van Dijk ambaye anaweza kuondoka mwisho wa msimu huu.
Inaelezwa Beukema ambaye amekuwa akipambania namba katika kikosi cha kwanza cha Napoli, kwa sasa anatamani kuondoka ili akapate changamoto mpya kwingineko.
Ingawa dili la kumnasa linaweza kuwa gumu, lakini kuna kila dalili Liverpool itafanikiwa kwani Napoli inatafuta fedha za kujazia ili kufanya usajili wa nyota kibao msimu ujao.
Kwa sasa Napoli inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Italia (Serie A), lakini haina uhakika wa kubeba ubingwa kutokana na kuachwa mballi na Inter Milan.
Anthony Gordon
INAELEZWA kuna uwezekano mkubwa winga wa Newcastle United na England, Anthony Gordon, 25, kuondoka katika klabu hiyo dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Gordon amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu Newcastle kwa muda mrefu lakini vigogo wengi Ulaya wamekuwa wakihitaji saini yake hali inayomfanya hata mchezaji mwenyewe kushawishika kuondoka.
Manchester United ni miongoni mwa timu zilizoonyesha nia ya kumsajili staa huyu ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Victor Osimhen
MKURUGENZI wa michezo wa Arsenal, Andrea Berta alisafiri hadi Istanbul Jumapili kufuatilia mchezo wa Galatasaray dhidi ya Fenerbahce ikiwa ni katika harakati za kumfuatilia mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria, Victor Osimhen, 27.
Osimhen ni mmoja wa washambuliaji bora Ulaya kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao na Arsenal inataka kumsajili dirisha lijalo ili kuboresha eneo lao ushambuliaji.
Awali mabosi wa Arsenal walikuwa na mpango wa kumsajili Julien Alvarez lakini sasa nguvu zao zinaonekana kuhamia kwa Osimhen ambaye hakuna uhakika wa asilimia 100 ikiwa Galatasaray itakuwa tayari kumwachia.
Yan Diomande
LIVERPOOL inaamini uhusiano wao mzuri na RB Leipzig unaweza kuwasaidia kumsajili mapema winga chipukizi wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yan Diomande, 19, dirisha la majira ya kiangazi.
Liverpool imekuwa ikifanya madili mbalimbali na Leipzig pia, kocha wao wa zamani Jurgen Klopp kwa sasa ni miongoni mwa viongozi wa kampuni inayomiliki timu hiyo, hivyo inaamini kuna ahueni wa asilimia kadhaa wa kukamilisha dili hilo.
Nathan Ake
EVERTON inajiandaa kumsajili beki wa Manchester United na timu ya taifa ya Uholanzi, Nathan Ake, 31, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Inaelezwa Ake anatafuta muda zaidi wa kucheza, jambo linalomfanya kufikiria kuondoka Man City ambako ushindani katika safu ya ulinzi ni mkubwa.
Kwa upande wa Everton, yenyewe inaamini uzoefu wa Ake katika Ligi Kuu England wa kucheza nafasi nyingi kwenye safu ya ulinzi utakuwa nyongeza muhimu katika kikosi chao.
Maxi Araujo
NEWCASTLE United na Aston Villa imeonyesha nia ya kumsajili mchezaji wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Uruguay, Maxi Araújo, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Araujo ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja, winga na beki wa kushoto. Klabu zote mbili zimeanza tu mazungumzo na wawakilishi wa fundi huyu lakini hadi sasa hakuna hata moja iliyowasilisha ofa rasmi kwenda kwa Lisbon kwa ajili ya kumsajili. Inaaminika wababe hao wanaweza kuhitaji zaidi ya Pauni 60 milioni ili kumuuza.
Dani Olmo
MANCHESTER City, Paris St-Germain na Arsenal zipo vitani kuiwania saini ya kiungo wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Dani Olmo, 27.
Taarifa kutoka Barca zimefuchua mabosi wa timu hiyo wapo tayari kumuuza Olmo ikiwa watapokea ofa nono mwisho wa msimu.
Olmo ambaye ni zao la akademi ya Barcelona, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030. Msimu huu amecheza mechi 44 za michuano yote.
Christian Kofane
ARSENAL inaendelea kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji kijana wa kimataifa wa Cameroon, Christian Kofane, 19, anayekipiga katika kikosi cha Bayer 04 Leverkusen.
Inaelezwa Leverkusen inahitaji hadi Pauni 60 milioni ili kumuuza mchezaji huyo dirisha la majira ya kiangazi.
Kofane kwa sasa ni mmoja kati mastaa tegemeo Leverkusen na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.