Arsenal yaanza kwa Coventry City
Muktasari:
- Kikosi cha Mikel Arteta tayari kimeanza msimu kikiwa na taji baada ya kuifunga Manchester City mabao 3-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii Jumapili iliyopita. Mshambuliaji Riccardo Calafiori alifunga ndani ya dakika ya kwanza, kabla ya Kai Havertz na Martin Odegaard kukamilisha ushindi huo wa kuvutia.
LONDON, ENGLAND: MABINGWA Arsenal itaanza kampeni yake ya kutetea taji la Ligi Kuu England leo, Ijumaa usiku kwa kuikaribisha Coventry City, iliyopanda daraja msimu huu, kwenye Uwanja wa Emirates.
Kikosi cha Mikel Arteta tayari kimeanza msimu kikiwa na taji baada ya kuifunga Manchester City mabao 3-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii Jumapili iliyopita. Mshambuliaji Riccardo Calafiori alifunga ndani ya dakika ya kwanza, kabla ya Kai Havertz na Martin Odegaard kukamilisha ushindi huo wa kuvutia.
Kwa Coventry, huo ni mtihani mzito zaidi katika kurejea kwake Ligi Kuu baada ya kukaa miaka 25 nje ya mashindano hayo. Kikosi cha Frank Lampard kilitwaa ubingwa wa Championship msimu uliopita baada ya kumaliza pointi tisa mbele ya Ipswich, huku kikihakikisha ubingwa ikiwa imesalia michezo miwili.
Coventry pia inataka kuvunja mwenendo mbaya wa mabingwa watatu waliopita wa Championship ambao wote walishuka daraja msimu uliofuata. Hata kama haitapata pointi Emirates, kiwango kizuri dhidi ya Arsenal kinaweza kuwa ishara ya matumaini kwa Lampard na vijana wake.
Arsenal itaingia kwenye mchezo huo ikiwa bado inawakosa William Saliba na Jurrien Timber kutokana na majeraha. Saliba hana tarehe maalum ya kurejea, wakati Timber bado anahitaji wiki kadhaa kabla ya kuwa tayari kucheza licha ya kuanza mazoezi.
Cristhian Mosquera, aliyefanya vizuri akicheza sambamba na Gabriel katika ushindi dhidi ya City, anatarajiwa kuendelea kupewa nafasi katikati ya ulinzi, huku Ben White na Calafiori wakicheza pembeni.
Katikati ya uwanja, Arteta ana uchaguzi mgumu baada ya Myles Lewis-Skelly na Bruno Guimaraes kufanya vizuri dhidi ya City. Hata hivyo, Guimaraes alionekana akiwa amewekewa barafu kwenye paja baada ya kutolewa, jambo linaloweza kuibua hofu kuhusu hali yake ya mwili.
Coventry nayo inajiandaa kwa msimu huo ikiwa na matumaini baada ya kumaliza maandalizi kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Monaco, katika mchezo ambao Ellis Simms na Loum Tchaouna walifunga.
Lampard ameongeza uzoefu kwenye kikosi chake kwa kumsajili mshambuliaji Taiwo Awoniyi kutoka Nottingham Forest, ambaye amefunga mabao 21 katika mechi 90 za Ligi Kuu.
Haji Wright bado ni shaka kutokana na jeraha la paja, wakati Jack Rudoni alikuwa akiendelea kurejesha utimamu wa mwili kabla ya mchezo dhidi ya Monaco.
Coventry si timu inayotarajiwa kukaa nyuma na kusubiri kushambuliwa. Msimu uliopita ilifunga mabao 97 katika Championship, angalau 15 zaidi ya timu nyingine yoyote, huku mfumo wa 4-2-3-1 wa Lampard ukiipa timu hiyo kasi na soka la moja kwa moja.
Pia ina uwezo mkubwa katika mipira iliyokufa baada ya kufunga mabao 29 kutokana na mipira hiyo bila kuhesabu penalti msimu uliopita.
Arsenal inatarajiwa kutawala umiliki wa mpira, lakini Coventry inaweza kuwa tishio kupitia mashambulizi ya kushtukiza na mipira iliyokufa, hasa kutokana na Arsenal kukosa Saliba na Timber.
SHERIA MPYA
Ligi Kuu inaanza na majaribio ya sheria mpya inayolenga kuzuia makipa kutumia majeraha kama njia ya kusimamisha mchezo, kupunguza kasi ya wapinzani au kupata nafasi ya kupewa maelekezo ya kiufundi.
Endapo mchezo utasimamishwa au kuanza kuchelewa kutokana na jeraha la kipa, kocha atakuwa na sekunde 10 kumteua mchezaji mwingine atakayetoka nje kwa dakika moja baada ya mchezo kuanza tena.
Iwapo kocha hatamteua mchezaji ndani ya sekunde hizo 10, nahodha atalazimika kutoka nje kwa dakika moja. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha majeraha ya makipa yanakuwa ya kweli badala ya kutumiwa kama mbinu ya kuvuruga kasi ya mchezo.
Pia, mchezaji anayebadilishwa atakuwa na sekunde 10 kuondoka uwanjani. Akizidisha muda huo, mchezaji anayekuja kuchukua nafasi yake hataruhusiwa kuingia hadi kusimama kwa kwanza kwa mchezo baada ya dakika moja kupita.