Arsenal? ubingwa bado sana Magwiji wafunguka vikwazo vinavyoitesa
Muktasari:
- Arsenal imemaliza nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo kwenye Ligi Kuu England, lakini imefanya maboresho kwa kusajili mastaa wa maana kwenye dirisha hili ili kwenda kubeba taji hilo la Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: MAGWIJI wa soka la England, Gary Lineker na Alan Shearer wanaamini Arsenal itaangukia pua tena kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Arsenal imemaliza nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo kwenye Ligi Kuu England, lakini imefanya maboresho kwa kusajili mastaa wa maana kwenye dirisha hili ili kwenda kubeba taji hilo la Ligi Kuu England.
Straika mpya, Viktor Gyokeres ni ingizo muhimu sana kwenye kikosi hicho cha Emirates baada ya kusajiliwa akitokea Sporting CP. Msimu uliopita, Arsenal ilicheza bila ya kuwa na straika asilia na hilo lilidaiwa moja ya sababu kubwa iliyowanyima taji la ubingwa wa Ligi Kuu.
Martin Zubimendi ni ingizo jingine kwenye sehemu ya kiungo, huko kocha Mikel Arteta akiwanasa pia Cristhian Mosquera, Christian Norgaard na Noni Madueke kuja kuboresha makali ya kikosi hicho.
Hata hivyo, Lineker na Micah Richards wanaamini Arsenal itakwama tena kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England kwa sababu mbili.
Alipoulizwa kuhusu nafasi ya Arsenal kubeba ubingwa, Richards alikumbushia mawazo yake ya msimu uliopita: “Hii ni ngumu kwa sababu nilisema msimu uliopita Man City ingebeba ubingwa kama wachezaji wake wangekuwa fiti. Kama Man City itapata majeruhi, basi mambo yatakuwa tofauti.
“Ujio wa Gyokeres ni kitu kikubwa Arsenal. Na hii si kwamba ni mshambuliaji mwenye jina kubwa. Ni kwa sababu ya mikimbio yake na kama wanavyozungumziwa mastraika bora wa muda wote. Havertz ni mzuri sana, tumekuwa shabiki wa Havertz, lakini acheze Namba 10, atengeneze nafasi na sio kuongoza mashambulizi.
Nafahamu Havertz ana mikimbio mizuri anapocheza Namba 10, lakini hana hisia za kuwa straika. Hilo ndilo linalonifanya niamini Gyokeres utakuwa usajili bora.
“Lakini, bado sijui kama hilo linatosha kubeba ubingwa. Ninachojua, wakipata majeruhi mmoja au wawili tu, wanarudi kulekule msimu uliopita. Ninachoweza kusema watashindana, lakini sio kuwa mabingwa.”
Gwiji wa Ligi Kuu England, Alan Shearer naye anaamini Arsenal itaendelea na hadithi yake ileile.
“Nakubaliana na wewe. Nadhani watashindana, lakini hawatachukua ubingwa,” alisema Shearer na kuongeza. “Nimependa usajili wao. Nadhani ni aina ya wachezaji iliyokuwa ikiwataka. Na sidhani kama wamemaliza kusajili kwa sababu kuna wachezaji wataondoka.
“Wataweza kutinga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini siwaoni kuwa na nguvu ya kubeba ubingwa. Bado sana.”
Wakati huo huo, Lineker naye amekubaliana na wachambuzi wenzake kwamba Arsenal bado haina kiwango cha kwenda kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England licha ya kufurahishwa na kiwango cha Gyokeres alichokionyesha kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Athletic Bilbao. Lakini, alichodai ni Arsenal itakabiliwa na wakati mgumu mbele ya Liverpool, ambayo pia imefanya usajili wa mastaa wengi wa maana kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.