Arsenal, Spurs zazidi kujisogeza kwa Eze
Muktasari:
- Eze mwenye umri wa miaka 27, katika mkataba wake kuna kipengele ambacho kinaeleza ikiwa timu yoyote inahitaji kuuvunja itatakiwa kulipa kiasi hicho cha pesa.
ARSENAL inatarajiwa kuwasiliana na Crystal Palace kujadili iwapo inaweza kukubali ofa yao ya kumsajili winga wa timu hiyo na England, Eberechi Eze, kwa ofa ya chini ya Pauni 68 milioni dirisha hili.
Eze mwenye umri wa miaka 27, katika mkataba wake kuna kipengele ambacho kinaeleza ikiwa timu yoyote inahitaji kuuvunja itatakiwa kulipa kiasi hicho cha pesa.
Hata hivyo, Arsenal ambayo inapambana kubana bajeti haitaki kulipa kiasi chote hicho na badala yake inataka kujadili kuona kama italipa chini ya hapo.
Katika msimu uliopita alicheza mechi 43 za michuano yote, akafunga mabao 14 na kutoa asisti 11.
Mbali ya Arsenal, saini yake pia inawindwa na Tottenham lakini mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya kujiunga na washika mitutu badala ya timu nyingine yoyote.
Taarifa zinaeleza Palace haina mpango wa kushusha bei ya Eze, pia haina haraka ya kumuuza kwa sasa, hivyo timu yoyote inayomhitaji itatakiwa kuwasilisha kiasi cha pesa kilichopo katika mkataba wake.
Mbali ya kiwango bora ambacho amekionyesha akiwa na Palace, Eze pia amekuwa bora pia akiwa na timu ya taifa ya England kuanzia michuano iliyopita ya Euro na mechi kadhaa za nyuma ya hapo na huko ndiko alijitambulisha zaidi na kusababisha timu nyingi zianze kumfuatilia.
Kama ilivyo kwa Arsenal, mabosi wa Spurs pia hawataki kulipa kiasi cha Pauni 68 milioni kinachohitajika na Palace hivyo wao pia wanataka kuishawishi timu hiyo ipunguze bei.
Jean-Philippe Mateta
TOVUTI ya Footmercato imefichua Liverpool imekutana na mshambuliaji wa Crystal Palace, Jean-Philippe Mateta, 28, pamoja na wakala wake jijini Paris ili kufanya mazungumzo ya kumsajili dirisha hili. Katika kikao hicho cha siri, Mateta na wakala wake wote walivutiwa na mipango ya Liverpool na wapo tayari kufanya nao kazi. Hata hivyo, baada ya kumalizana na mchezaji mwenyewe Liverpool inapanga ratiba ya kukutana na wawakilishi wa Palace kujadili masuala ya ada ya uhamisho.
Bryan Mbeumo
BAADA ya majadiliano ya muda mrefu, hatimaye kwa Manchester United na Brentford zinadaiwa kufikia makubaliano ya ada ya uhamisho juu ya Bryan Mbeumo katika dirisha hili. Staa huyu wa kimataifa wa Cameroon mwenye umri wa miaka 25, amekuwa katika rada za Man United kwa muda mrefu na licha ya kufikia makubaliano ya masilahi yake binafsi kwa muda mrefu changamoto kubwa iliyokuwa inakwamisha dili hilo ilikuwa ni ada ya uhamisho. Kwa mujibu wa ripoti Man United imekubali kutoa takribani pauni 65 milioni.
Omari Hutchinson
BRENTFORD inafanya majadiliano ya ndani kwa ndani kuona ikiwa kuna ulazima wa kuwasilisha ofa kwenda Ipswich Town kwa ajili ya kumsajili winga wa timu hiyo na timu ya taifa ya vijana ya England chini ya miaka 21, Omari Hutchinson, mwenye umri wa miaka 21, dirisha hili. Benchi la ufundi la timu hii linamwangalia Omari kama mbadala sahihi wa Bryan Mbeumo ambaye amatarajiwa kujiunga na Manchester United katika dirisha hili.
Joao Felix
BENFICA inaendelea kufanya mazungumzo na Chelsea kuhusu uhamisho wa moja kwa moja wa Joao Felix aliyecheza kwa mkopo kwenye kikosi chao msimu uliopita. Awali Benfica ilikuwa ikihitaji kumsainisha mkataba mwingine wa mkopo wa msimu mmoja lakini maombi hayo yalitupiliwa mbali na Chelsea iliyosisitiza inataka kumuuza. Staa huyu wa kimataifa wa Ureno, 25, kiwango chake msimu uliopita kilikuwa cha kuvutia na kuishawishi Benfica.
Benoit Badiashile
BEKI wa Chelsea na timu ya taifa ya Ufaransa, Benoit Badiashile, mwenye umri wa miaka 24, ambaye amekuwa katika rada za timu mbalimbali barani Ulaya hususani Marseille, amesisitiza hana mpango wa kuondoka dirisha hili na msimu ujao atacheza kwenye kikosi hicho kwa msimu mmoja zaidi kwani anaamini atabadilisha kila kitu na kuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo kwa msimu ujao.
Harvey Elliott
WEST Ham imemwongeza katika orodha yao ya usajili mshambuliaji wa Liverpool, Harvey Elliott na kiungo mkabaji wa Liverpool Tyler Morton na inahitaji kuwasajili dirisha hili. Mastaa hawa ambao wote wana umri wa miaka 22, wamekuwa wakihusishwa kuondoka tangu dirisha lililopita la majira ya baridi lakini timu zinazohitaji kuwasajili hazijafikia bei ambayo Liverpool inaihitaji.
Corentin Tolisso
MANCHESTER United imewasiliana na Olympique Lyon kuuliza upatikanaji wa kiungo wa timu hiyo, Corentin Tolisso, 30, dirisha hili. Man United ilikuwa na matumaini makubwa ya kumsajili staa huyu dirisha hili hususani kipindi ambacho Lyon imepewa adhabu ya kushushwa daraja lakini sasa mambo yamebadilika baada ya timu hiyo kushinda rufaa yao.