Arsenal, Man City kuna mtu anaachwa!
Muktasari:
- Hadi hapa ilipo kwa sasa, Arsenal inapewa nafasi kubwa ya kwenda kunyakua taji hilo mwisho wa msimu.
LONDON, ENGLAND: MWAKA Mpya 2026 umeshafika na sasa ni suala la kuhesabu tu miezi kabla ya Ligi Kuu England kufika mwisho na bingwa mpya kutangazwa.
Lakini, hadi sasa swali kubwa mezani ambalo linahitaji majibu, ni timu gani itakwenda kunyakua taji hilo?
Hadi hapa ilipo kwa sasa, Arsenal inapewa nafasi kubwa ya kwenda kunyakua taji hilo mwisho wa msimu.
Kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kimekuwa na wakati mzuri kwelikweli kwenye msimu huu wa 2025-26, kikijaribu kuusaka ubingwa huo baada ya kukaribia kuubeba kwenye misimu mitatu mfululizo, kilipomaliza kwenye namba mbili, mara mbili dhidi ya Manchester City na moja dhidi ya Liverpool, msimu uliopita.
Ushindi wao wa mabao 4-1 dhidi ya Aston Villa umeifanya Arsenal kuongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi nne. Na kama itapambana kubaki kwenye kilele cha msimamo wa ligi hadi Mei, basi hapo itakuwa imetimiza lengo la kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England ambao imekuwa ikiusubiri kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
Hata hivyo, kwenye kulifikia hilo kuna kigingi kimoja mbele yao, Manchester City. Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England imekuwa kawaida yao.
Lakini, ilipigwa kikumbo kwenye kuibana Arsenal kileleni baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Sunderland katika mchezo wao wa kwanza iliocheza 2026 katika Ligi Kuu England na hivyo kuifanya kuachwa nyuma kwa pointi nne na Arsenal katika vita hiyo.
Hali ilivyo kwenye mchakamchaka huo wa kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England kila wiki kunaonekana kuwa na tukio na inavyoonekana mambo yataendelea kuwa hivyo hadi mwisho.
Hakuna timu yenye uhakika wa kushinda kila mechi na hilo linafanya vita hiyo ya ubingwa wa Ligi Kuu England kuwa na mvuto wa hali ya juu. Je, ratiba ya timu hizo ikoje Januari?
ARSENAL
Licha ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Ligi na Kombe la FA ratiba yake kuonekana kama kuongeza mzigo kwa Arsenal, lakini bila shaka miamba hiyo ya Emirates kipaumbele kitakuwa kwenye kubeba taji la Ligi Kuu England. Mechi yao ya kwanza 2026 ni ile ya ugenini dhidi ya Bournemouth.
Kisha itarudi nyumbani kucheza na Liverpool, ambayo imekuwa haipo kwenye ubora wake sana licha ya kuwa mabingwa watetezi.
Itafuatia mechi ya ugenini Nottingham Forest na baadaye Emirates kuikabili Manchester United, huku Arsenal itafunga Januari kwa mechi ya ugenini huko Elland Road kuwakabili Leeds United.
Ratiba ya EPL ya Arsenal Januari:
-Januari 3 vs Bournemouth (ugenini)
-Januari 8 vs Liverpool (nyumbani)
-Januari 17 vs Nottingham Forest (ugenini)
-Januari 25 vs Man-United (nyumbani)
-Januari 31 vs Leeds United (ugenini)
MAN CITY
Mechi ya ugenini huko Stamford Bridge bila ya shaka itakipa kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola mwanga wa kufahamu hatima yao kwenye mbio hizo za ubingwa. Lakini, uzuri ni kwamba Chelsea haitakuwa na kocha wake mkuu baada ya Enzo Maresca kuondoshwa. Man City itaendelea na ratiba inayohitaji ujanja mwingi ili kuendelea kuwa kwenye mbio za ubingwa, kwani ikimalizana na The Blues itacheza na Brighton kisha itaenda Old Trafford kukabiliana na Man United. Baada ya hapo, itarudi nyumbani kucheza na Wolves kabla ya kuwa na kipute dhidi ya Tottenham, ambao wamekuwa wakiwapa wakati mgumu uwanjani, Februari 1.
Ratiba ya EPL ya Man City Januari:
-Januari 4 vs Chelsea (ugenini)
-Januari 7 vs Brighton (nyumbani)
-Januari 17 vs Man United (ugenini)
-Januari 24 vs Wolves (nyumbani)
Kwa ratiba ya Januari ya miamba hiyo miwili inayoonekana kupigana vipushi kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, nani atatoboa? Nani mwenye mechi ngumu? Ngoja tuone.