Ligi Kuu England, balaa ni lile lile!
Muktasari:
- Ukiweka kando vita ya kukabana koo kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo, shughuli ni pevu pia kwenye kunasa nafasi ya kuwamo ndani ya Top Four.
LONDON, ENGLAND: HABARI ni ileile, jichanganye uchanganywe. Hivyo, ndivyo ilivyo kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, wakati vita ikiwa kali ya kujaribu kupanda juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Ukiweka kando vita ya kukabana koo kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo, shughuli ni pevu pia kwenye kunasa nafasi ya kuwamo ndani ya Top Four.
Jumanne, zitapigwa mechi ambazo huenda zikaleta mabadiliko makubwa kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku nyingine zikitarajiwa kuchezwa Jumatano na kitu kinacholeta mvuto mkubwa katika mikikimikiki hiyo ya kibabe kabisa kwenye ligi za Ulaya.
Arsenal itahitaji ushindi ili kuendelea kung’ang’ania kileleni na kutinga Mwaka Mpya 2026 ikiwa hapo, kuchagiza harakati zake za kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya kukukaribia kuubeba kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita.
Lakini, shughuli inayowakabili ni pevu, mbele yao wamesimama Aston Villa, ambao pia wapo kwenye mbio za ubingwa, huku wakiwa wameshinda mechi zao 11 mfululizo.
Kingine, Aston Villa inanolewa na kocha wa zamani wa Arsenal, Unai Emery, ambaye amekuwa na kawaida ya kukitesa kikosi hicho cha Emirates. Arsenal itahitaji kushinda ili isijali matokeo ya timu nyingine.
Rekodi zinaonyesha, mechi tano zilizopita, Aston Villa imeshinda tatu, sare moja na Arsenal imeambulia ushindi mara moja tu. Balaa hilo.
Aston Villa ikishinda, itafikia pointi za Arsenal na kwamba miamba hiyo ya Emirates itaendelea kuwa kileleni kwa tofauti ya mabao tu.
Wapinzani wengine wa Arsenal kwenye kugombania kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England ni Manchester City, ambao wao watasubiri Jumatano, ambapo watakipiga na Sunderland ugenini.
Kwa vyovyote, Man City ya Pep Guardiola itahitaji ushindi bila ya kujali matokeo ya wapinzani wake katika mbio za ubingwa ili kuzidi kuleta presha kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Vita nyingine tamu ipo kwenye Top Four, ambapo wanaochuana kwenye hilo wote wataingia mzigoni Jumanne. Liverpool iliyopo kwenye nafasi ya nne kwa sasa, itahitaji kushinda uwanjani Anfield dhidi ya Leeds United ili kubaki Top Four, kinyume cha hapo, itajiweka kwenye hatari ya kuporomoshwa.
Pointi za Liverpool zinaweza kufikiwa na Manchester United iliyopo kwenye nafasi ya sita katika msimamo huo, hivyo kichapo au sare kwa Arne Slot na kikosi chake, kitampa nafasi Ruben Amorim na jeshi lake kumshusha kwenye msimamo endapo kama kitafanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Wolves uwanjani Old Trafford. Mambo ni moto.
Lakini, vita hiyo ya kuisaka Top Four inawahusu pia Chelsea, ambao kwa sasa wanashika namba tano katika msimamo na watakuwa na kibarua kizito cha kuwakabili Bournemouth uwanjani Stamford Bridge. Ni shida juu ya shida.
Chelsea itahitaji ushindi katika mechi hiyo baada ya kutokea kuchapwa na Aston Villa katika mchezo uliopita, huku Man United ikiamini inaweza kufanya vizuri baada ya kupata mzuka kwa kuichapa Newcastle United katika mechi iliyopita. Itakuwaje? Ngoja tuone.
Mechi nyingine za Jumanne, Burnley itakipiga na Newcastle United, Nottingham Forest na Everton, wakati West Ham United itacheza na na Brighton kabla ya Jumatano, kushuhudia mechi za Crystal Palace dhidi ya Fulham na Brentford itamaliza ubishi na Tottenham Hotspur.