Arsenal kuvunja benki kwa Julian Alvarez
Muktasari:
- Alvarez amekuwa mhimili muhimu Atletico, lakini Kocha Mikel Arteta anamwona kama mchezaji anayefaa kuipa Arsenal makali zaidi katika safu ya ushambuliaji.
ARSENAL italazimika kuvunja benki kwa kutumia takriban Pauni 80 milioni ili kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid na Argentina, Julian Alvarez (25) dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Alvarez amekuwa mhimili muhimu Atletico, lakini Kocha Mikel Arteta anamwona kama mchezaji anayefaa kuipa Arsenal makali zaidi katika safu ya ushambuliaji.
Kwa sasa, kiasi kinachohitajika na Atletico ili kumuuza kinatajwa ni kikwazo na mabosi wa timu hiyo hawana presha yoyote, hivyo hawataki kujadili kuhusu bei badala yake wanataka pesa waliyotaja iwekwe mezani.
Staa huyu ambaye kabla ya kutua Atletico alikuwa akiichezea Man City ambako hakupata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza, tangu kuanza kwa msimu huu akiwa na wababe hao wa Hispania amecheza mechi 28 za michuano yote akifunga mabao 11.
Licha ya kumsajili Viktor Gyokeres katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Arteta anaamini bado timu hiyo inahitaji mshambuliai mwingine. Mkataba wa sasa wa Alvarez unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Andy Robertson
TOTTENHAM Hotspur inaendelea kufanya mazungumzo na Liverpool kwa ajili ya kuipata saini ya beki wa kushoto wa Liverpool na nahodha wa timu ya taifa ya Scotland, Andy Robertson, 31.
Inalezwa Mazungumzo hayo yanahusisha mkataba wa mkopo wa nusu msimu ambao utakuwa na kipengele cha kumnunua mazima ifikapo mwisho wa msimu.
Robertson, ambaye amekuwa mhimili wa mafanikio ya Liverpool kwa miaka kadhaa, yupo katika kipindi cha mwisho cha mkataba wake na amekuwa hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza. Baadhi ya ripoti zinadai Spurs pia inataka kuwasilisha ofa ya Pauni 5 milioni ili kumnunua mazima.
Antonee Robinson
Liverpool imefufua tena harakati zake za kumsajili beki wa kushoto wa Fulham na timu ya taifa ya Marekani, Antonee Robinson, 28.
Robinson amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu na benchi la ufundi la Liverpool linaamini atasaidia sana kuboresha safu yao ya ulinzi ambayo kwa sasa inakumbana na changamoto nyingi.
Mabingwa hao wa zamani wa England wanamwona staa huyu pia kama mbadala wa muda mrefu katika nafasi ya beki wa kushoto, ambako Andy Robertson anaweza akaondoka.
Christos Mandas
BOURNEMOUTH iko karibu kukamilisha dili la kipa wa Lazio na timu ya taifa ya Ugiriki, Christos Mandas, 24, kwa mkopo wenye thamani ya Pauni 2.6 milioni.
Mandas anatarajiwa kujiunga na klabu hiyo ya Kusini mwa England dirisha la usajili la Januari ili kuongeza ushindani kwenye nafasi ya golikipa. Mazungumzo yamefikia hatua ya mwisho, huku pande zote zikiwa na matumaini ya kumalizana hivi karibuni. Kipa huyu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Lazio.
Jonas Omlin
SUNDERLAND imeanza mawasiliano na Borussia Monchengladbach kuhusu uwezekano wa kumsajili kipa wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Uswisi, Jonas Omlin, 32.
Omlin ana uzoefu mkubwa Bundesliga na Sunderland inaamini anaweza kuwa msaada katika mpango wa kuhakikisha wanafuzu michuano ya kimataifa msimu huu kwa kumaliza nafasi za juu.
Mazungumzo bado yako hatua za awali na Monchengladbach ipo tayari kumuuza ikiwa Sunderland itawasilisha ofa nzuri.
Oleksandr Zinchenko
BEKI wa Arsenal na timu ya taifa ya Ukraine, Oleksandr Zinchenko, 29, bado yuko kwenye mazungumzo na klabu yake kuhusu uwezekano wa kuondoka na kujiunga na Ajax kwa mkataba wa moja kwa moja.
Ajax imeonyesha nia kubwa ya kumsajili mchezaji huyo ambaye kwa sasa hapewi kipaumbele katika kikosi cha washika mitutu.
Arsenal iko tayari kumwachia na inaamini itamuuza kwa ofa nzuri itakayosaidia kufanya usajili wa mastaa wengine ifikapo mwisho wa msimu.
Tim Iroegbunam
LAZIO ina nia ya kumsajili kiungo wa Everton na England, Tim Iroegbunam, 22, dirisha la usajili la Januari. Klabu hiyo ya Italia inaamini Iroegbunam yupo tayari kujiunga nao, hivyo kazi kubwa iliyopo ni kuhakikisha wanaishawishi Everton ikubali kumuuza.
Hadi sasa Everton bado haijaweka wazi msimamo wake ikiwa ipo tayari kumuuza au laa, lakini ripoti za ndani zinadai itakuwa tayari kusikiliza ofa itakayolingana na thamani ya mchezaji huyo.
Ibrahim Mbaye
CHELSEA na Aston Villa zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya winga chipukizi wa Paris St-Germain na timu ya taifa ya Senegal, Ibrahim Mbaye, 18.
Hata hivyo, PSG inamwona kinda huyu kama mradi wa baadaye, lakini presha kutoka klabu za Ligi Kuu England inaweza kuwalazimu kufikiria hatma yake ikiwa ni kumuongeza mkataba mpya au kumtoa kwa mkopo kwenda timu ambayo itampa nafasi kubwa zaidi ya kucheza.
Chelsea inahitaji huduma ya fundi huyu ikiwa ni sehemu ya mkakati wao wa kuwekeza kwa wachezaji vijana.