Anderson achimba mkwara akitua Etihad
Muktasari:
- Anderson mwenye umri wa miaka 23 amesaini mkataba wa miaka mitano utakaomuweka Etihad hadi mwaka 2031, huku akiwa mchezaji wa pili wa Uingereza kusajiliwa kwa gharama kubwa zaidi katika historia.
MANCHESTER, ENGLAND: MARA tu baada ya kiungo wa kimataifa wa England, Elliot Anderson kusaini mkataba wa miaka mitano kuitumikia Manchester City, amewatupia kijembe wapinzani wao wa jani, Manchester United.
Man City ilitangaza rasmi kumsajili Anderson kutoka Nottingham Forest kwa ada ya Pauni 116 milioni.
Baada ya kutambulishwa rasmi Man City, Anderson hakupoteza muda kuwachokoza wapinzani wao hao akisema City ndiyo “Wafalme wa Manchester.”
“Hii ni moja ya dabi kubwa zaidi duniani. Kwa muda wote ambao nimeifahamu Manchester, City ndiyo Wafalme wa Manchester. Itakuwa mechi kubwa sana na siwezi kusubiri kushiriki katika mchezo wa aina hiyo,” amesema Anderson.
Anderson mwenye umri wa miaka 23 amesaini mkataba wa miaka mitano utakaomuweka Etihad hadi mwaka 2031, huku akiwa mchezaji wa pili wa England kusajiliwa kwa gharama kubwa zaidi katika historia.
Uhamisho wake kwenda Man City ulikubaliwa Julai 2 na ulitarajiwa kumfanya kuwa mchezaji wa England aliyesajiliwa kwa ada kubwa zaidi kuwahi kutokea, akivunja rekodi ya Pauni 115 milioni ambazo Real Madrid ililipa kumsajili Jude Bellingham mwaka 2023.
Hata hivyo, dili hilo liliahirishwa hadi baada ya Kombe la Dunia na Anderson aliisaidia England kumaliza nafasi ya tatu na kutwaa medali ya shaba.
Katika kipindi hicho, Chelsea ilikamilisha usajili wa Morgan Rogers kutoka Aston Villa kwa Pauni 117 milioni, jambo lililomfanya Anderson kubaki kuwa mchezaji ambaye alikuwa karibu kuweka rekodi ya uhamisho mkubwa zaidi wa Muingereza lakini hakufanikiwa na sasa anashika nafasi ya pili.
Katika maisha ya Anderson, Man City kweli imekuwa na mafanikio makubwa kuliko Man United, ikitwaa mataji 26 tangu mwaka 2002, wakati United ikiwa na 24, ukiijumuisha Community Shield.
Klabu ya Newcastle United, ambayo ilimuuza Anderson kwenda Nottingham Forest kwa Pauni 35 milioni mwaka 2024 kutokana na kanuni za PSR, haina kipengele cha kupata asilimia ya mauzo yajayo. Hivyo Nottingham Forest itanufaika kwa faida ya takribani pauni milioni 81 kutokana na dili hilo.
Anderson aliiongoza England kutwaa ubingwa wa Ulaya kwa timu ya chini ya miaka 21 mwaka jana kabla ya kupandishwa katika kikosi cha wakubwa chini ya kocha Thomas Tuchel.
Kwa sasa amekuwa mchezaji muhimu wa England akiwa ameichezea timu hiyo mara 17 na alicheza katika mechi zote za Three Lions kwenye Kombe la Dunia la mwaka huu.
Msimu uliopita aliichezea Nottingham Forest mechi 50 katika mashindano yote, akichangia timu hiyo kubaki Ligi Kuu England na kufika hatua ya nusu fainali ya Europa League.
Akizungumzia uamuzi wake wa kujiunga na Manchester City amesema:
“City ni moja ya klabu kubwa zaidi duniani na kikosi chao ni bora sana. Mara niliposikia wananitaka, nilihakikisha nafanya kila linalowezekana kuja hapa.”
“Kama mchezaji unataka kujipima katika kiwango cha juu kabisa. Kuwa City kunanipa nafasi hiyo. Kutoka nje unaweza kuona jinsi klabu hii inavyowajali wachezaji wake na kuweka mazingira bora ya kufanikiwa. Nina furaha sana na siwezi kusubiri kuichezea klabu hii.”
“Mafanikio ambayo wameyapata ndani ya miaka 10 hadi 15 iliyopita ni ya kipekee. Ni heshima kubwa kupata nafasi ya kuwa sehemu ya historia hiyo.”
“Hawa ni washindi. Hawachoki kupambana na ndiyo aina ya timu ambayo nilitaka kuchezea. Kwa zaidi ya miaka 10 wamekuwa wakitawala, ndiyo maana nilitaka kujiunga nao.”
“Nitakaporudi Manchester baada ya mapumziko nitafanya kila kitu kuhakikisha najijenga ndani ya kikosi hiki.”
“Hii ni klabu iliyojengwa kushinda mataji na kupambana katika kiwango cha juu kabisa. Hilo linanivutia sana na nina dhamira ya kulipa imani waliyonionesha.”
Takwimu zinaonyesha Anderson alikuwa na mguso mwingi zaidi wa mpira (3,300), alishinda mipambano mingi zaidi (297) na kurejesha umiliki wa mpira mara nyingi zaidi (306) katika Ligi Kuu England msimu uliopita.
Kiungo huyo amesema pia mfumo wa kocha Enzo Maresca unalingana na uwezo wake.
“Sikuwahi kuacha kuamini kwamba nitafika hapa. Sasa nimefika lakini bado nina mengi ya kuboresha. Nina miaka 23 tu na naamini bado sijafikia kiwango changu bora.”
“Nimekuwa nikifuatilia timu za Maresca kwa miaka kadhaa na nimezungumza na baadhi ya wachezaji waliowahi kufanya naye kazi. Wote wanamheshimu sana.”
“Ninapenda kucheza kwa kasi, nguvu na presha kubwa uwanjani pamoja na kuwapa mashabiki sababu ya kushangilia. Nafikiri tutalingana vizuri.”
Mkurugenzi wa soka wa Manchester City, Hugo Viana, amesema Anderson ni mmoja wa viungo bora chipukizi duniani kwa sasa.
“Elliot ni mmoja wa vipaji bora kabisa duniani katika nafasi ya kiungo. Ana nguvu, anafanya kazi kubwa uwanjani na ana uwezo wa kipekee wa kupiga pasi.”
“Maendeleo yake katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa makubwa sana. Akiwa na miaka 23 bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kukua na tunaamini anaweza kuwa kiungo kamili.”
“Manchester City ndiyo sehemu sahihi kwake kuendelea kuimarika na tunafurahi kwamba yeye pia anaamini hivyo. Tuna hamu kubwa ya kumuona akifanya kazi nasi kuelekea msimu mpya.”
Anderson anatarajiwa kuwa mapumzikoni kwa wiki tatu kabla ya kujiunga rasmi na kikosi cha Maresca mwishoni mwa maandalizi ya msimu mpya.