Amorim kupata kazi Man United mchakato matata
Muktasari:
- Unambiwa hivi, wakati huu mashabiki wa Man United wakiwa wanatofautiana maoni wakimjadili kocha Amorim kama anatosha au hatoshi kwenye kikosi hicho, mabosi wa Old Trafford wamekaa kimya hawasemi kitu, kwa sababu wanafahamu jinsi walivyompata.
MANCHESTER, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Kumbe ishu ya Ruben Amorim kupata kazi ya kuinoa Manchester United kibarua chake hajakipata kirahisi, mchakato wake ulikuwa matata.
Unambiwa hivi, wakati huu mashabiki wa Man United wakiwa wanatofautiana maoni wakimjadili kocha Amorim kama anatosha au hatoshi kwenye kikosi hicho, mabosi wa Old Trafford wamekaa kimya hawasemi kitu, kwa sababu wanafahamu jinsi walivyompata.
Man United iliweka ubaoni majina ya makocha sita wakati ilipokuwa ikimtafuta bosi mpya wa kuja kurithi mikoba ya Erik ten Hag ilipomfuta kazi karibu mwaka mmoja uliopita.
Kwenye orodha hiyo ya makocha sita, walikuwamo Thomas Tuchel na Graham Potter, lakini ni Amorim ndiye aliyewaaminisha mabosi wa Man United na kuamua kumpatia kazi.
Ten Hag alifutwa kazi baada ya Man United kuanza msibu vibaya na kipindi hicho, Amorim alikuwa huko kwenye kikosi cha Sporting Lisbon na hakuwa kwenye mipango ya mabosi wa Old Trafford kwa kipindi hicho.
Man United baada ya ushindi wa taji la Kombe la FA mwaka 2024 ilianza mchakato wa kutafuta kocha mpya kwa sababu Ten Hag tayari alikuwa amekalia kuti kavu licha ya ushindi wa taji hilo uwanjani Wembley. Tuchel kwa kipindi hicho alikuwa hana kazi baada ya kuachana na na Bayern Munich na alikwenda kukutana na mabosi wa Man United huko Monaco, lakini kocha huyo Mjerumani alitaka muda wa kupumzika kidogo.
Potter alikuwa anatokea kwenye wakati mgumu huko Chelsea, hivyo kulikuwa na maswali mengi kama anaweza kwenda kumudu presha ya kuinoa Man United. Lakini, bado kulikuwa na imani kubwa angeteuliwa ili akabidhiwe mikoba hiyo.
Roberto de Zerbi, Mauricio Pochettino, Thomas Frank na Marco Silva ni miongoni mwa makocha wengine waliokuwa wamewekwa kwenye orodha ya waliokuwa wakisakwa na Man United ili wakamrithi Mdachi Ten Hag huko Theatre Of Dream.
Mkurugenzi wa soka wa Man United, Jason Wilcox alikwenda kuzungumza na Amorim na alivutiwa, lakini awali ilidhaniwa kwamba kutoka Sporting kwenda kufanya kazi Old Trafford kulihitaji ujasiri mkubwa kutokana na timu hiyo kuwa na malengo makubwa.
Kinachoelezwa ni kwamba ofa ilipelekwa kwa kocha De Zerbi, ambaye kwa wakati huo alikuwa ameachana na Brighton, lakini kocha huyo alikataa kutokana na sababu za kiuchumi na tayari Marseille ilikuwa kwenye nafasi ya kumchukua na ofa yao ilikuwa nzuri.
Frank na Silva walionekana nafasi ya kupata kibarua cha Old Trafford kuwa kubwa hasa kwa kipindi hicho walikuwa wakifanya kazi kwenye klabu za Brentford na Fulham mtawalia na zilikuwa zikifanya vizuri.
Lakini, hakuna aliyetua Old Trafford. Frank aliondoka Brentford kwenda Tottenham, wakati Silva alibaki Fulham. Thiago Motta, ambaye alikuwa akifanya vizuri Bologna aliamua kwenda kujiunga na Juventus, ambaye alionekana kama kocha anayekuja juu kwa kasi kama ilivyo kwa Amorim.
Na uamuzi wa kumfuta kazi Ten Hag ulipofikiwa, wakati timu ikiwa kwenye nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi baada ya kushinda mechi tatu tu kati ya tisa ilizokuwa imecheza Ligi Kuu England, mabosi wa Man United wakaamua kutua kwa Amorim.
Amorim alikuwa na rekodi tamu huko Sporting, ambapo aliisaidia timu hiyo kushinda mataji ya ligi, mataji matatu ya makombe ya ndani na alikuwa na wastani wa ushindi wa asilimia 71, ambao uliwashawishi mabosi wa Man United kwenda kunasa huduma yake.
Man United ilifanya naye kikao kwa saa tano huko Seville, Hispania, Oktoba 18. Amorim alionyesha kusitasita mara kadhaa kukubali kibarua hicho kwa sababu msimu ulikuwa umeshaanza na hakutaka kuanzia kati, lakini mabosi walimhakikishia usalama wake.
Wakati sasa Amorim akiwa kwenye usukani wa klabu hiyo, timu ikiwa na matokeo ya kupanda na kushuka, bosi kubwa, Sir Jim Ratcliffe, ambaye ni mmiliki mwenza alisema kocha huyo anahitaji miaka mitatu ili kuifanya Man United kuwa bora tena uwanjani. Hiyo ina maana, kocha huyo Mreno bado yupo salama kwenye kibarua chake huko Old Trafford bila ya kujali matokeo ya sasa.
MECHI ZIJAZO ZA MAN UNITED
-Novemba 8 vs Tottenham (ugenini)
-Novemba 24 vs Everton (nyumbani)
-Novemba 30 vs Crystal Palace (ugenini)
-Desemba 4 vs West Ham (nyumbani)
-Desemba 8 vs Wolves (ugenini)
-Desemba 13 vs Bournemouth (nyumbani)
-Desemba 21 vs Aston Villa (ugenini)
-Desemba 26 vs Newcastle (nyumbani)
-Desemba 30 vs Wolves (nyumbani)