Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Amorim: Bora nimchezeshe kocha wa makipa lakini siyo Rashford

Muktasari:

  • Si unajua kwamba fowadi huyo Mwingereza kwa sasa anapigishwa tu mazoezi, lakini kwenye mechi anawekwa jukwaani kabisa? Na mara yake ya mwisho kuitumikia timu hiyo ilikuwa Desemba mwaka jana?

MANCHESTER, ENGLAND: BALAA hilo. Mambo yameanza kuchangamka huko Manchester United juu ya sakata la mchezaji Marcus Rashford na kocha wake Ruben Amorim.

Si unajua kwamba fowadi huyo Mwingereza kwa sasa anapigishwa tu mazoezi, lakini kwenye mechi anawekwa jukwaani kabisa? Na mara yake ya mwisho kuitumikia timu hiyo ilikuwa Desemba mwaka jana?

Basi kocha wao, Amorim ameibuka na kupiga nyundo nyingine kali zaidi baada ya kusema kwamba ni bora amweke benchi kocha wake wa makipa kama mchezaji wake wa akiba kuliko mshambuliaji Rashford.

Fowadi huyo, Rashford aliwekwa kando na kocha Amorim kwa mara nyingine kwenye mechi ya jana Jumapili wakati Man United ilipoichapa Fulham 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu England, shukrani kwa bao pekee la beki wa kati, Lisandro Martinez uwanjani Craven Cottage.

Kocha huyo Mreno alisema Rashford haonyeshi juhudi zozote mazoezini na kusema kwamba kocha wa makipa mwenye umri wa miaka 63, Jorge Vital anastahili zaidi kuwekwa kwenye benchi kama mchezaji wa akiba kuliko fowadi huyo Mwingereza.

Alipoulizwa kuhusu kukosekana kwa Rashford, Amorim alisema: "Nitamweka Vital kwenye benchi mbele ya mchezaji ambaye kila siku hana juhudi zozote. Sitabadilika kwenye hilo eneo. Siku zote itakuwa sababu ileile. Sababu ni mazoezini. Kwa namna ninavyoona mchezaji anavyofanya mazoezini, kwenye maisha yake, kila siku. Kama vitu havibadiliki, basi nami sitabadilika.

"Kitu hicho kipo kwa kila mchezaji — kama unafanya ziada, kama unafanya vitu sahihi, tutamtumia huyo mchezaji. Unaweza kuona kwenye benchi letu hapa. Tulihitaji kasi, kujaribu kuweka udhibiti wa mipira ya kutenga — hivyo ndivyo nilivyoamua."

Rashford amekuwa kwenye mipango ya kunaswa kwa mkopo na klabu za Borussia Dortmund, Monaco na AC Milan, licha ya kwamba mwenyewe anapendelea zaidi kwenda kukipiga kwa miamba ya Nou Camp, Barcelona.

Mara ya mwisho Rashford kuichezea Man United ilikuwa Desemba 12 kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Viktoria Plzen na hajawahi kuwa kwenye kikosi tangu kwenye mechi ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Newcastle United, Desemba 30 mwaka jana.

Baada ya ushindi wa juzi Jumapili, Rashford aliposti kwenye ukurasa wake wa Instagram aliposema: "Hongera kwa ushindi vijana."

Bao la mpira wa kubabatiza la beki Martinez katika dakika 78 liliisaidia Man United kupanda hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Lakini, mashabiki walimgeukia mmiliki mwenza wa timu hiyo, bilionea Sir Jim Ratcliffe, ambaye alikuwapo jukwaani Craven Cottage walipokuwa wakiimba: "Ni kama Glazer tu, Jim Ratcliffe ni ...".

Tajiri Ratcliffe amepandisha bei ya tiketi uwanjani Old Trafford kwa Pauni 66, Desemba  — ikiwamo ya watoto. Bilionea Ratcliffe anajaribu kupandisha mapato ya Man United ili kwenda sawa na kanuni za mapato na matumizi endelevu. Na kuhusu usajili, kocha Amorim alisema "nahitaji msaada kuboresha timu".

Wakati Amorim akimweka mbali kabisa na kikosi chake mchezaji Rashford, matumaini yake kwenye wachezaji wa safu ya ushambuliaji ipo kwa Joshua Zirkzee na Rasmus Hojland. Kwenye mchezo wa Fulham, Amorim alianza na Hojlund.

Staa huyo wa zamani wa Atalanta ameichezea Man United kwenye mechi 48 za Ligi Kuu England tangu aliponaswa kwa Pauni 64 milioni mwaka 2023. Lakini, alishindwa kufunga bao kwenye mechi 36 za ligi, ikiwa ni karibu mechi za msimu mzima. Na kwenye mechi ya Fulham hakufunga, wala kulenga goli.

Aligusa mpira mara 17 na moja tu ndiyo ilikuwa ndani ya boksi la Fulham. Na hapa kwenye pasi hakuwa vizuri kabisa, ambapo fowadi huyo alipiga pasi sahihi sita tu kati ya nane kabla ya kutolewa kwenye dakika ya 58.

Hojlund alipotoka, akaingia Zirkzee, ambaye pia ameshindwa kuonyesha ubora mkubwa tangu aliponaswa kwa Pauni 36.5 milioni akitokea Bologna.

Mdachi huyo amefunga mabao matatu ya ligi msimu huu kama ilivyo kwa Rashford. Zirkzee naye anahusishwa na mpango wa kuondoka.

Lakini, fowadi huyo bado hajaanza kuwekwa benchi na kocha Amorim akiendelea kupewa nafasi ili kuonyesha ubora wake. Lakini, kwa mchezo huo wa Fulham, Zirkzee alikuwa na kiwango cha hovyo kuliko hata Hojlund. Hakupiga shuti hata moja, hata kugusa mpira ndani ya boksi la Fulham alishindwa.

Zirkzee alipiga pasi tano tu, moja ilishindwa kufika kwa mtu aliyemkusudia. Jambo hilo linamfanya Amorim kusugua kichwa kupata fowadi mpya.